Thursday, December 15, 2016

MAKALA: Miundombinu kwa Manufaa yetu wote

Na Biseko Lisso Ibrahim, MWUUM

JUKUMU kubwa la Serikali ni kuwa na miundombinu imara ili miundombinu hiyo itumike kurahisisha huduma mbalimbali zinazotolewa na hatimaye kuinua pato kwa Taifa na wananchi kwa ujumla, hii inaweza kutekelezwa kwa kutumia fedha za ndani ambazo zinatokana na kodi zinazokusanywa lakini pia kwa kupata fedha kutoka kwa wahisani wa maendeleo.

Kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017 kwenye eneo la Miundombinu inayojumuisha barabara, reli, nyumba, bandari, viwanja vya ndege, mawasiliano. Serikali imetenga zaidi ya shilingi Trilioni 2 ili kuhakikisha miundombinu inayojengwa katika maeneno mbalimbali nchini inakuwa imara na bora na ya manufaa kwa wananchi wa Tanzania.
Makala hii itajikita kwenye eneo la reli ambapo Serikali imetenga takribani shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya Reli ya kisasa ambayo itarahisisha usafiri wa reli hapa nchini.

Katika uboreshaji, ujenzi na ukarabati Serikali inategemea kujenga reli mpya ya kisasa ambayo inajulikana kama Standard Gauge pamoja na mpango huo kabambe pia kuna mipango mbalimbali ya kupunguza msongamano wa magari barabara kwa kuhakikisha jiji la Dar es Salaam linakuwa na treni zaidi ya moja ili iwe inawatoa wananchi kutoka sehemu kwenda sehemu nyingine na kurahisisha shughuli zao za kila siku.

Mpaka sasa jitihada zilizofanyika katika kutekeleza hilo ni kuanzisha treni ya kutoka Stesheni hadi Ubungo maarufu kama treni ya Mwakyembe, treni ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wakazi wanakaa maeneo ya kuanzia stesheni mpaka ubungo.
Wiki ya kwanza ya mwezi wa Agosti, 2016, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alizindua treni nyingine yenye mabehewa 16 inayofanya safari zake kutoka Stesheni Dar es Salaam mpaka Pugu ikiwa ni utekelezaji wa ahadi za Serikali katika msongamano wa magari barabarani.

Treni hiyo iliyozinduliwa ilianza safari zake kwa kuwa na mabehewa 15 ambapo kila behewa moja kwa safari moja linabeba abiria 100 na hivyo kwa behewa hizo kwa safari moja hubeba abiria zaidi ya 1400 kwa safari moja na kupunguza mabasi zaidi ya 40 barabarani ambayo kwa wastani hubeba abiria 30 kwa safari moja na hivyo kupunguza wingi wa mabasi barabara yanayofanya safari zake kutokea Pugu kuelekea Posta.

Pamoja na kuanzishwa kwa treni hiyo Shirika la Reli (TRL) ambao ndio waendeshaji wa huduma hiyo wamekuwa wakifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazokabili treni hiyo ikiwemo upungufu wa mabehewa kwani mahitaji ya mabehewa ni makubwa ukilinganisha na wingi wa abiria, pia changamoto ya feni na ukatishaji wa tiketi imekuwa ikifatiliwa kwa karibu na uongozi wa TRL.

Pamoja na Serikali kutekeleza ahadi zake kwa wananchi kwa kuzindua treni hiyo kuna Wananchi wachache ambao wamekuwa wakirudisha nyuma jitihada hizo kwa kuhujumu miundombinu ambayo Serikali imewekeza fedha nyingi.
Tangu kuanza kutolewa kwa huduma hiyo tayari kumeripotiwa matukio ya uhujumu wa miundombinu ya reli likiwemo la kurusha mawe kwenye vioo vya treni hiyo ambapo tukio la kwanza liliripotiwa tarehe 24 Oktoba mwaka huu kwa mfanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Mustapha Omari kupigwa jiwe lililorushwa kutokea nje ya treni na kumjeruhi katika pua yake majira ya saa tatu usiku wakati treni hiyo ikipita katika eneo la karakata.

Tarehe 28 Oktoba katika eneo la Gongo la Mboto, lilirushwa tena jiwe wakati treni hiyo ikifanya moja ya safari zake za kila siku na tukio lingine la namna hiyo hiyo lilitokea tarehe 24 novemba majira ya saa 1.25 katika eneo la karakata lilirushwa jiwe kutokea nje na kumjeruhi mtoto mmoja aliyekuwa ndani ya treni hiyo.

Katika hali ya kawaida usafiri unaotumiwa na wakazi zaidi ya 17,000/- kila siku kutoka sehemu moja na kuelekea sehemu nyingine na kurahisisha shughuli zao na wakati huo huo wakawepo wananchi wachache ambao wanahujumu miundombinu hiyo kwa mtazamo wa kawaida wahujumu hao hawana nia njema na maendeleo yanayofanywa na Serikali yao.

Vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa vikiendelea kufanya sehemu yao katika kuhakikisha usalama wa abiria na
miundombinu unakuwepo pamoja lakini na wananchi wana sehemu ya kufanya kuhakikisha usalama unakuwepo.

Si jambo la busara kuendelea kuihujumu miundombinu hiyo kwani kwa kufanya hivyo tunaifanya Serikali iendelee kutumia fedha nyingi katika ukarabati wa miundombinu hiyo wakati fedha hizo zingetumika katika kuendeleza miundombinu hiyo na kuifanya kuwa bora zaidi.

Wakati unahujumu miundombinu kwa kurusha mawe kwenye mabehewa na kupasua vioo vya madirisha ya treni hiyo fikiria wale wananchi wanaotumia usafiri huo pia abiria wanaotumia usafiri huo wanapopata majeraha kwa sababu ya uhujumu huo au pia ikifika sehemuTRL kusimamisha huduma hiyo ilikukarabati mabehewa yaliyohujumumiwa na kurudisha kero ya usafiri kwa wananchi wanaotumia usafiri huo itakua si jambo jema na wananchi hawa hawatakuwa wametendewa haki.

Pamoja na TRL kuhakikisha inatatua changamoto zilizopo pia mipango iliyopo mwaka huu ni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa njia mpya za reli Jijini Dar es Salaam, zikiwemo zile za kwenda maeneo ya Pugu, Mbagala/Chamazi, Luguruni/Kibaha na Bunju/Bagamoyo na ujenzi wa mchepuo wa njia ya reli kutoka “Ilala block post” hadi Stesheni ili kuepusha mwingiliano wa treni ya abiria kutoka Stesheni kwenda Ubungo na ile ya mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaamsasa ni vyema wananchi wakaelewa ni kubwa ya Serikali yao katika kuimarisha miundombinu.

Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo na kuwa na miundombinu itakayowawezesha kufika mahala popote kwa usafiri ulio rahisi.

Ni wakati sasa kwa wananchi wanaokaa pembezoni mwa reli kulinda miundombinu na kutokubaliana na mwananchi yoyote wanayemuona akihujumu miundombinu aidha iwe kwa kurusha mawe lakini pia hata wakati mwingine kuchukua kokoto au namna yoyote ile ya uhujumu, kila mwananchi akumbuke kuwa miundombinu hii inatengenezwa kwa kutumia kodi za wananchi na kwa sasa nguvu kubwa imeelekezwa kutatua changamoto zilizojitokeza tangu kuanzishwa kwa usafiri huo.

No comments: