Thursday, December 1, 2016

MADIWANI MERU WAMKATAA MKURUGENZI

Na Woinde Shizza, Globu ya Jamii - Arusha 

BARAZA la madiwani Halmashauri ya Meru mkoani Arusha wamkaanga Mkurugenzi wao kwa kusema hana uwezo wa kuongoza Halmashauri hiyo.


Akitoa maazimio ya kikao cha baraza kilichokaa siku mbili kwa kuwajumuisha madiwani, wakuu wa idara mbalimbali na wataalam, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Willy Njau Alisema wametafakari kwa kina utendaji wa Mkurugenzi na kubaini kuwa hafai. "Tumejadili ajenda ya utendaji usioridhisha wa Mkurugenzi wetu na tumeona kuwa haufai kutokana na mambo mengi anayoyafanya yanakiuka kanuni na taratibu za Halmashauri"alisema Njau.

Aidha Njau alisema Mkurugenzi huyo ameonekana kukata mawasiliano na Mwenyekiti wa Halmashauri jambo alilosema siyo sahihi. pia ameweza kukata mawasiliano na madiwani wa Halmashauri hiyo pamoja na kusababisha hata wakuu wa idara kutokuwa na mawasiliano na madiwani jambo linalorudisha maendeleo nyuma.
Aliongeza kuwa Mkurugenzi huyo ameshindwa kukusanya makusanyo ya pesa kiasi cha milioni 150 kilichokusudiwa kukusanywa tangu Julai hadi Septemba mwaka huu jambo alilosema linaweza kusababisha Halmashauri kutopewa ruzuku kutoka serikalini kwasababu ya uzembe.


" Tumejiridhisha kuwa uwezo wa Mkurugenzi kuiongoza Halmashauri yetu kama Mkurugenzi Mtendaji ni mdogo hivyo hafai anadidimiza maendeleo ya Halmashauri ya meru" alisema Njau. Na kuongeza "Tumeamua kuiomba mamlaka yake na Uteuzi ichukue hatua stahiki za kumuwajibisha ili kunusuru maendeleo ya Halmashauri ya Meru".



Vilevile alisema kuwa Mkurugenzi huyo amekuwa akidharau maagizo yanayotolewa na kamati mbalimbali za baraza hilo na Kushindwa kuzitekeleza, ambako ni kuvunja kanuni na taratibu za Halmashauri. Hata hivyo alisema kitendo cha Mkurugenzi kukata posho za madiwani ni kinyume na utaratibu kwani ziliwekwa kisheria ambapo alisema Kama kuna tatizo la kukatwa posho ni lazima sheria hiyo ingebadilishwa kwanza. "Mwenye dhamana ya kutangaza kuwa posho zinabadilika ni Waziri mwenye dhamana hiyo lakini siyo Mkuu wa Mkoa, Wilaya au Mkurugenzi" alisema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Christopher Kazer akijibu hoja za Madiwani katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo.


Naye Diwani wa Kikatiti Elisa Mungure ambaye ni Mwenyekiti wa madiwani alisema Mkurugenzi huyo amekuwa akiendesha Halmashauri kisiasa jambo ambalo halifai. "Ninasikitishwa na uongo unaoelezwa na Mkurugenzi ambaye kateuliwa na Mheshimiwa Rais hii ni ajabu haiwezekani kuendelea kumuamini mtu wa aina hii" alisema Mungure.

Alisema Mkurugenzi huyo amekuwa akiwahamisha watendaji wa kata bila kufuata taratibu huku akishinikiza ofisi ya kata ya Kikatiti kuwa ni ya CCM huku ikiwa ni ofisi ya wananchi wala siyo ya chama chochote. Kwa upande wake Mkurugenzi Huyo, Christopher Kazer alisema anafuata maagizo ya mkuu wa nchi na hawezi kuwanyima watu kufikiri wanavyofikiri. "Maelekezo ya kupunguza matumizi yasiyolazima kutoka kwa mkuu wa nchi ninayafuata pia ndio maana nimepunguza matumizi mengi" alisema.

Alisema hawezi kuzuia maamuzi yanayotolewa na baraza hilo maana kwa namna moja au nyingine wamekaa wakatengeneza maamuzi hivyo hawezi kuwalazimisha kutofanya maamuzi.
baadhi ya madiwani wakifuatailia.


Aidha pia alibainisha kuwa anaamini kabisa madiwani hawa wanataka halmashauri iendeshwe kisiasa wanataka iendeshwe kama wao wanavyotaka kitu ambacho hatakubali kwani sio hakutumwa kufanya kazi ya siasa bali alitumwa kufanya kazi ya kuwasaidia wananchi na serikali kwa ujumla 

Alisema kuwa anaamini haya yote yanatokea kutokana na madiwani hawa kukatwa fedha za posho na usafiri ambao walikuwa wamejiwekea bila kufuata taratibu


"Hivi jamani ndugu waandishi mtu anatoka hapo Usa River anataka alipwe nauli elfu 80 ni haki kweli wengine wanatoka hapa hapa wakija kikao kikichelewa kuisha wanataka walipwe fedha za kulala laki laki sasa mimi hayo yote nimeyatoa, sasa hivi wanalipwa elfu 40 tu na mshahara wao upo pale pale sasa wao ndio maana wananipiga zegwe. mimi nasema nitasimamia ilani ya chama ambacho kinaongoza serikali pia nitafata sera ya Mheshimiwa Rais ya kubana matumizi sitakubali wafanye vitu ovyo na ninyamaze walifikia hatua wakataka hata kunigombanisha na watendaji wangu ila mimi nimeajiriwa na serikali mimi sio mwanasiasa na nitafanya kazi kama nilivyoaidi siku niliyoapishwa "alisema Mkurugenzi Kazer.

No comments: