Tuesday, December 6, 2016

DKT KALEMANI AWAAHIDI WAKAZI LYAMKENA KUSHEREHEKEA KRISMAS WAKIWA NA UMEME

Meneja wa Mradi wa Umeme wa Makambako – Songea, Didas Lyamuya (katikati), akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani (kulia) na Mbunge wa Makambako, Deo Sanga (kushoto), kuhusu maendeleo ya Mradi huo wakati wa ziara ya Naibu Waziri mkoani Njombe hivi karibuni
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lyamkena kilichopo Makambako mkoani Njombe hivi karibuni, wakati akiwa katika ziara kukagua miradi ya umeme.
Wananchi wa Kijiji cha Lyamkena, Wilaya ya Makambako mkoani Njombe, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani (hayupo pichani), wakati wa ziara yake mkoani humo hivi karibuni, kukagua miradi ya umeme.
Wananchi wa Kijiji cha Lyamkena, Wilaya ya Makambako mkoani Njombe, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani (hayupo pichani), wakati wa ziara yake mkoani humo hivi karibuni, kukagua miradi ya umeme.



Na Veronica Simba - Makambako

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani ametoa ahadi kwa wakazi wa Kijiji cha Lyamkena kilichopo Makambako mkoani Njombe, kuwa watasherehekea sikukuu ya Krismas hapo Desemba 25 mwaka huu wakiwa na umeme. 


Dk Kalemani aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi husika jana kijijini hapo, mbele ya Mbunge wa Makambako Deo Sanga, akiwa katika ziara kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.Naibu Waziri alimwagiza Meneja anayesimamia Mradi wa Umeme wa Makambako – Songea, Didas Lyamuya, kuhakikisha kazi ya kutandaza nyaya inafanyika usiku na mchana ili umeme uwake katika eneo hilo kufikia Desemba 25.

“Tumekubaliana na Meneja, amejipanga kuanzia wiki ijayo wataanza kutandaza nyaya na watakamilisha ndani ya siku 10,” alifafanua.Aidha, Dk Kalemani alimwagiza Meneja huyo kuviingiza katika Mradi huo mkubwa wa umeme, vijiji vya Kihumba na Katani ambavyo vilisahaulika, ili vipatiwe umeme sambamba na maeneo mengine yote kama yalivyoainishwa katika Mradi.

Awali, akitoa taarifa ya maendeleo ya Mradi husika kwa Naibu Waziri, Lyamuya aliahidi kukamilisha kazi yote na kukabidhi rasmi Mradi ifikapo mwezi Juni mwakani ambayo ni miezi mitatu kabla ya muda uliopangwa yaani Septemba 2018.Kufuatia ahadi hiyo, Naibu Waziri alimpongeza kwa kufanya kazi kwa bidii na kumtaka aendelee na ari hiyo ili wananchi wa Mikoa ya Njombe na Ruvuma wapate umeme utakaowasaidia kuendesha shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kuinua uchumi wao.

Kwa upande wake, Mbunge wa Makambako, Deo Sanga, alimshukuru Naibu Waziri Kalemani kwa niaba ya Serikali kwa jitihada ambazo Wizara yake imekuwa ikizifanya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu ya umeme. Aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ili azma ya wananchi wake kupatiwa umeme itimizwe kama ilivyopangwa.

No comments: