Friday, November 25, 2016

WAZIRI MWIGULU AWAONYA MADEREVA WANAOACHA MITI NA MAWE BARABARANI.


Na Nathaniel Limu- Singida.

Waziri wa mambo ya ndani Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (mb), ameliagiza jeshi la polisi nchini,kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria  madereva wanaoacha mawe na matawi ya miti barabarani.

Nchemba ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Iramba mkoani Singida, ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye kikao cha 38 cha bodi ya barabara mkoa kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa mjini hapa.

Amesema baadhi ya madereva wa magari na hasa yale makubwa,hutumia mawe kuzuia magari yao kutembea wakati wakiyafanyia matengenezo ya dharura.

“Wakiisha maliza kuyafanyia matengenezo magari yao, madereva hao huyaacha barabarani mawe na matawi ya miti ambayo hutumika kutoa tahadhari kwa vyombo vingine vya moto. Kitendo hicho kinahatarisha maisha na mali za watumiaji wengine wa barabara kwa vile yanaweza kusababisha ajali”, amesema Mwigulu.

Kwa hali hiyo amesema jeshi la polisi linapaswa kuimarisha mawasiliano ili waweze kuwathibiti na kuwakamata madereva wanaoacha mawe na matawi ya miti barabarani.

Katika hatua nyingine, waziri huyo amesema upo umuhimu mkubwa wa wananchi na hasa wale wanaoishi kando kando ya barabara kuelimishwa juu ya matumizi bora ya barabara zinazojengwa kwa fedha nyingi ili waweze kuacha kupitisha mifugo yao na mikokoteni barabarani.

Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya barabara na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew John Mtigumwe ameagiza kuwa fedha zinazotolewa na serikali na wafadhili mbalimbali wa miradi ya barabara matumizi yake yasimamiwe kikamilifu, ili zitumike kwa miradi iliyokusudiwa.

“Ujenzi wa miradi hiyo ya barabara ufanane na thamani halisi ya fedha zilizotumika. Pia kazi za ujenzi wa barabara za ngazi zote wapewe wakandarasi bora na wenye uwezo wa kutekeleza miradi ikakamilika kwa wakati. Nasisitiza kuimarishwa kwa usimamizi na ukaguzi wa mara kwa mara wa miradi ya barabara ili ziwe za kiwango kinachokusudiwa”,amesema.

Wakati huo huo, mhandisi Mtigumwe ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa alikuwa meneja TANROADS mkoa, ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa TANROADS mkoa wa Singida chini ya meneja wake Mhandisi Leonard Kapongo kwa kazi nzuri ya usimamizi na ukaguzi uliopelekea miradi ya barabara kujengwa kwa ubora unaofafana na fedha zilizotumika.
 Waziri wa Mambo ya ndani Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba akiwa katika kikao cha 38 cha bodi ya barabara ya Mkoa wa Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida na Mwenyekiti wa Bodi ya barabara Mkoani hapa Mhandisi Mathew John Mtibumwe akiendesha kikao cha 38 cha bodi ya barabara ya Mkoani hapa, Kulia kwake ni Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Mhe, Martha Mlata.
 Meneja wa TANROADS Mkoani Singida Mhandisi Leonard Kapongo akijibu baadhi ya hoja katika kikao cha 38 cha bodi ya barabara ya Mkoa wa Singida.

 Wajumbe na wadau mbalimbali wa bodi ya barabara wakichangia hoja katika kikao cha 38 cha bodi ya barabara ya Mkoa wa Singida.

No comments: