Wednesday, November 2, 2016

Usalama, Faragha na Imani katika matumizi Changamoto kwenye TEHAMA Changamoto kubwa katika TEHAMA


Mkurugenzi Mkuu, Mh. James Kilaba
Na Mwandishi Maalum, Hammamet, Tunisia.

PAMOJA na maendeleo na faida mbalimbali za Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), masuala ya Usalama, faragha na imani katika matumizi bado yameendelea kuwa masuala ya kuwekwa maanani katika ngazi za kitaifa na kimataifa.

Akihutubia kikao cha Mkutano wa Dunia wa Masuala ya Viwango Katika Mawasiliano (World Telecommunication Standardization Assembly – WTSA-16) mjini Jasmine Hammamet, nchini Tunisia hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Eng. James Kilaba amesema tekinolojia mpya ndani ya TEHAMA zina mchango mkubwa katika usalama (wa mitandao,mifumo, vifaa, data na wa watumiaji); faragha ( katika data na watumiaji) na Imani (kwenye mitandao,mifumo, vifaa, data na kwa watumiaji). 

“Katika vikao kama hivi vya majadiliano kuhusu TEHAMA, wakati mwingi hatusahau kuzungumzia masuala ya huduma, vifaa na ukuaji wa watumiaji, mtandao na hata mapato. Leo tunazungumzia mchango wa teknolojia mpya katika usalama, faragha na Imani katika matumizi ya TEHAMA”, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA aliuambia mkutano huo.

Eng. Kilaba ailisema kumekuwepo na mabadiliko ya teknolojia kutoka zilizotawaliwa kwa kiasi kikubwa na kuendeshwa kwenye mfumo wa intaneti kwa kutumia kompyuta binafsi zilizounganishwa kwa mfumo wa waya hadi tekinolojia zinazotumia vifaa ya mkononi vilivyounganishwa bila kutumia waya. Amesema hii imewezesha na kufanikisha mawasiliano zaidi na kwa kupitia mfumo wa intaneti kuifikia dunia iliyounganishwa na mfumo wa kompyuta.

Eng Kilaba aliongeza kwamba mada kuu ya majadioiano katika mkutano huo ilikuwa ni huduma, vifaa, kukua na kuongezeka kwa watumiaji na kupanuka na kwa mifumo ya mawasiliano ambayo inawafika mbali zaidi na kuwafikia watu wengi zaidi.

“Wasimamizi wa mawasiliano duniano kote wanayo changamoto ya kukabiliana na mahitaji ya watumiaji na kubadilika kwa vifaa, bila kujali kuwa vimefungwa wapi au kutumiwa vipi ili mradi vinaimarisha usalama, faragha na Imani ya watumiaji. Kwa hiyo kimsingi ni watu ambao wanaishi kwenye utamaduni tofauti na katika maeneo tofauti ya kijiografia”, amesema Mkurugenzi Mku wa TCRA.

Ameeleza kwamba Tanzania, kama nchi inayoendelea imefanya mengi katika sekta ya usalama wa mitandao ya kompyuta zinazotumika kwa mawasiliano. Aliongeza kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inao mfumo wa Usalama wa Matumizi ya Usalama Mtandaoni ambao umewekwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali.

Amesema Tanzania imeanzisha mfumo wa kitaifa wa kushughilikia dharua zinazohusiana na matumizi ya kompyuta za mawasiliano (TZ- CERT) ambao unatumika kutoa elimu kuhusu masuala ya usalama wa mitandao, taarifa na ujuzi kwa wadau na watumiaji ili kuwawezesha kuwa na kiwango cha kuridhisha cha utaalamu unaohitajika katika kushughulikia masuala makubwa yanayohusiana na matumiai ya mitandao ya inayotumia mifumo ya kompyuta kwa mawasiliano.

Hali kadhalika, aliongeza kuwa Tanzania ina kituo cha kitaifa kinachohifadhi data. Vilevile aliuambia mkutanio huo kwamba Tanzania imeanzisha utaratibu wa kuzuia matumizi mabaya ya data au taarifa kutoka kwenye simu za mkononi zilizoibwa nchini Tanzania.Eng. Kilaba alisema kwamba vitengo vya kushughulikia dharua za mifumo ya mawasiliano inayotumia kompyuta imeanzishwa katika nchi nne na kwa kiasi kikubwa nchi hizo zinabadilishana na kulinganisha taarifa kuhusu masuala ya usalama wa mitandao.

Kupitia umoja wa taasisi za Mawasiliano Afrika Mashariki ambao unajulikana kama EACO, nchi wanachama zinakutana na kujadili masuala mbalimbali kuhusu usalama wa mitandao. Aliongeza kwamba changamoto zilizojitokeza kuhusiana na usalama, faragha na Imani katika matumizi ya TEHAMA zinaweza kuainishwa katika maeneo matano ambao ni viwango hafifu, sera, sheria na mikakati.

“Viwango, Sheria na Mikakati vinahitajika ili kuinua kiwango cha ulinzi wa nchi katika masuala ya ulinzi wa mitandao. Kwa kuwa masuala ya usalama wa mitandao hayaishii ndani ya mipaka ya ncchi moja, viwango vilivyowekwa, sheria zilizowekwa na Kanuni zilizopo znahitajika kuhuishwa ili zitumike katika maeneo ya nchi zaidi ya moja na pia ulimwenguni pote. Inaaminika kwamba kuna wataalamu wachache wa masuala ya usalama wa mitandao wenye hadhi ya kimataifa wanaoweza kushughulikia kikamilifu ulinzi na makosa yanayohusiana na mitandao” alileza Mhandisi Kilaba.

Alisisitiza kwamba kuna umuhimu wa kuwa na mikakati ya kitaifa kuhusu masuala ya usalama wa mitandaoo ambayo itawezesha kueneza elimu, ufahamu na ujuzi wa watumiaji na wadau wengine na watumiaji wengine ili kuwawezesha kushughulikia kikamilifu matukio ya usalama wa mitandao. Alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na mfumo wa kuthibiti usalama wa mitandao ndani na nje ya mipaka ya nchi husika.

“Baadhi ya nchi zinazoendelea hazina mifumo ya kuthibiti usalama wa mitandao ya kompyuta za mawasiliano. Mifumo hii ikiwekwa na kutumika inawezesha uratibu, uchambuzi na uchukuaji wa hatua za kuimarisha mifumo na kubadilishana taarifa kuhusu usalama na tishio kwa mifumo ya kompyuta za mawasiliano’, Eng. Kilaba aliuambia mkutano huo.Mkutano wa WTSA unafanyika kila baada ya miaka minne. Mkutano wa wa mwaka huu ulianza 25 Oktoba hadi Novemba 3. Ulitanguliwa na Mkutano wa Dunia wa masuala ya viwango uliofanyika 25 Oktoba 2016.

No comments: