Na Adili Mhina, Kigoma
Wizara ya Fedha na Mipango -Tume ya Mipango kwa kushirikiana na Serikali ya Ubelgiji inaendesha mafunzo ya maandalizi ya miradi ya maendeleo kwa ajili ya ufadhili wa washirika wa maendeleo kwa Mkoa wa kigoma.
Akifungua mafunzo hayo yanayoendelea mjini kigoma na kuwashirikisha Makatibu Tawala, Wakurugenzi na wataalam wa sera na mipango kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa kigoma, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri alieleza kuwa Serikali ya Ubelgiji ambayo ndio iliyofadhili mafunzo hayo kuwa imefanya jitihada kubwa katika kufadhili miradi mbalimbali katika Mkoa wa Kigoma.
“Tunaishukuru sana Serikali ya Ubelgiji kwani kwa kipindi kirefu imekuwa ikifanya kazi kubwa katika kufadhili miradi ya maendeleo hususan kwenye sekta za kilimo na maji ambapo kwa kiwango kikubwa imesaidia kuboresha maisha ya wananchi wa mkoa huu,” alieleza Bibi Mwanri.
Alisisitiza kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana kupitia miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Ubelgiji katika Mkoa wa Kigoma zipo changamoto kadhaa ambazo zimeonekana kupunguza ufanisi wa miradi husika.
Miongoni mwa changamoto hizo ni; rushwa, kiwango kisichoridhisha cha uratibu wa utekelezaji wa miradi, uwakilishi duni katika kamati za utekelezaji wa miradi na ugumu wa kupata taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Changamoto nyingine ni pamoja na miundombinu mibovu hususan barabara na umeme ambayo inachangia kutokuvutia wataalam kuishi katika mkoa wa Kigoma, na uhaba wa utaalam katika maandalizi, kutekeleza na kusimamia kwa ufanisi fedha zinazotumika kugharamia miradi ya maendeleo.
Mwanri aliongeza kuwa baada ya kubaini changamoto hizo, Tume ya Mipango kwa kushirikiana na Serikali ya Ubelgiji iliona umuhimu wa kutoa mafunzo ili kuongeza uelewa wa wataalam katika kuainisha, kuchagua, kuchambua, kutafuta njia sahihi za ugharamiaji, kusimamia utekelezaji, na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo.
Nae Mratibu wa mafunzo hayo Bw. Paul Sangawe alifafanua kuwa katika kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21) uwekezaji wa Umma umeongezeka ambapo kwa sasa Serikali inatumia Shilingi za kitanzania trilioni 11.8 kila mwaka, na katika kipindi cha miaka mitano ijayo shilingi Trilioni 59 zinatazamiwa kutumika kugharamia miradi ya maendeleo.
“Ni muhimu kuelewa kuwa ugunduzi wa gesi, madini, nk kunaendana na ongezeko la mapato kwa Serikali huku matumizi katika eneo la miradi ya maendeleo nayo yakiongezeka. Hivyo, ni vyema kijiandaa mapema ili kuhakikisha kuwa fedha zitakazopatikana zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo tarajiwa,” alieleza Sangawe.
Kwa mujibu wa Sangawe, matarajio katika mafunzo hayo ni pamoja na; kupata maoni kutoka kwa washiriki kwa ajili ya maandalizi ya programu ya ushirikiano wa maendeleo baina ya Serikali ya Tanzania na Ubelgiji (2017- 2021), kuongezeka kwa ufanisi wa utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo na kuhakikisha kuwa maandiko yote ya miradi ya maendeleo yanazingatia Mwongozo wa Usimamizi na Uwekezaji wa Umma.
Sangawe ambaye pia anasimamia Klasta ya Biashara za Kimataifa na Mahusiano ya Uchumi Tume ya Mipango amewahakikishia washiriki wa mafunzo hayo kuwa washirika wa maendeleo wanaunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha uchumi na hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri akitoa hotuba ya Ufunguzi wa mafunzo ya miradi ya maendeleo kwa ajili ya ufadhili wa washirika wa maendeleo kwa Mkoa wa kigoma. Kulia ni mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa kigoma Bw. Samwel Tenga, wa kwanza kushoto ni Kaimu Naibu Katibu Mtendaji Klasta ya Uchumi Jumla kutoka Tume ya Mipango, Dkt. Lorah Madete na pembeni yake (mwenye tai) ni Mratibu wa mafunzo hayo Bw. Paul Sangawe.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ambao ni Makatibu Tawala, Wakurugenzi na wataalam wa sera na mipango kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Kigoma wakiendelea wakifuatilia mafunzo.
Mratibu wa Mafunzo Bw. Paul Sangawe akitoa maelezo juu ya utayari wa washirika wa maendeleo katika kufadhili miradi ya maendeleo nchini. Kulia ni Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri na Kushoto ni Dkt. Lorah Madete kutoka Tume ya Mipango.
Mkufunzi wa Mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. John Mduma akitoa mafunzo juu ya maandalizi ya miradi ya maendeleo kwa ajili ya ufadhili wa washirika wa maendeleo.
Baadhi ya wadau wa mafunzo wakimsikiliza mkufunzi (hayupo picha ni) wakati wa mafunzo mjini Kigoma.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri (Wapili kutoka kulia kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wakufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Matibu Tawala wa Wilaya za Kigoma, Kasulu, Kibondo, Uvinza na Kakonko. Wa kwanza kulia (waliokaa) ni mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Bw. Samwel Tenga, wengine ni viongozi kutoka Tume ya Mipango.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri (Wapili kutoka kulia kwa waliokaa) akiwa na wakurugenzi wa Mipango kutoka Halmashauri za Mkoa wa Kigoma.
Picha ya pamoja kati ya Kaimu katibu Mtendaji, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wa pili kutoka kulia (waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na maafisa Mipango, Wachumi, na Watakwimu kutoka Halmashauri za mkoa wa Kigoma. Wa kwanza kulia (waliokaa) ni mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Bw. Samwel Tenga wengine ni viongozi kutoka Tume ya Mipango.
No comments:
Post a Comment