Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
Wizara ya Fedha na Mipango imekamilisha ujenzi wa mfumo wa malipo moja kwa moja kupitia akaunti za walipwaji katika mtandao wa malipo wa Benki Kuu ya Tanzania (Tanzania Interbank Settlement System – TISS), katika mkoa wa Morogoro, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa miamala mbalimbali inayofanywa na serikali
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James amezitaja Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Halmashauri za Wilaya ya Kilombero, Morogoro, Mvomero, Kilosa na Ulanga, kwamba zitaanza kufanya malipo hayo kwa mfumo huo wa TISS kuanzia mwezi Desemba mwaka huu.
“Nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwezi Desemba, 2016 Halmashauri zote zilizopo katika Mkoa wa Morogoro ziweze kufanya malipo kwa kutumia mfumo wa malipo wa TISS” alisema Dotto James.
Amesema kuwa malipo hayo yatafanyika kwa kutumia mfumo wa malipo wa TISS uliojengwa katika mikoa yote Tanzania Bara ikiwemo Ofisi za Hazina Ndogo na Sekretariati za Mikoa, Wizara, Idara za Serikali zinazofanya malipo yake kupitia Ofisi Kuu ya Malipo (CPO) iliyopo Hazina, malipo ya Pensheni kwa wastaafu, Kitengo cha Kupambana na Fedha Haramu, Mfuko wa Bunge, Mfuko wa Mahakama na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
“Hivi karibuni mfumo huu wa malipo umeunganishwa katika Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Kinondoni na Temeke. Katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, mfumo huu umeunganishwa katika Halmashauri za Wilaya ya Ukerewe, Magu, Sengerema, Kwimba, na Misungwi” alifafanua Katibu Mkuu huyo.
Ameongeza kuwa katika mkoa wa Mbeya, mfumo huo umefungwa katika Halmashauri ya jijini la Mbeya, Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Kyela, Mbarali, Chunya, Mbeya, Mbozi na Ileje wakati mkoani Arusha maeneo yanayohusika ni Halmashauri ya Jiji la Arusha, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Longido, Meru, Monduli, Karatu, Ngorongoro.
Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma mfumo huu umeunganishwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Kongwa, Mpwapwa, Chamwino, na Kondoa wakati mkoani Tanga, Halmashauri ya Jiji la Tanga, Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Pangani, Muheza, Handeni, Kilindi, Korogwe, Lushoto na Mji wa Korogwe zimeunganishwa katika mfumo huo.
Kuanzia Julai, 2010 hadi katikati ya Mwezi Novemba, 2016 mfumo huu ulikuwa tayari umeunganishwa katika Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizopo katika Mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya, Songwe, Arusha, Dodoma na Tanga ambapo umeonesha mafanikio makubwa” Alisema Bw. Dotto James.
Katibu Mkuu huyo amewataka wadau wote wanaofanya biashara na maeneo yaliyofungwa mfumo huo mkoani Morogoro, kuwasilisha taarifa muhimu ili ziweze kuingizwa katika Mtandao wa malipo wa Serikali [Intergrated Financial Management System (IFMS)] ili uanze kutumika kuanzia Mwezi Desemba mwaka huu kufanya malipo.
Taarifa hizo zinahitajika kwa kuwa ni muhimu ili kuwezesha malipo kufanyika kwa mlipwaji, ikiwa ni pamoja na Namba ya akaunti ya benki, Namba ya tawi la benki, Jina la akaunti, Aina ya akaunti, Namba ya kuandikishwa biashara, Namba ya kuandikishwa Kampuni, Namba ya Mlipakodi, Jina la benki na Jina la Tawi la benki.
“Hivyo Makampuni na watu wanaofanya biashara na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Halmashauri za Wilaya ya Kilombero, Morogoro, Mvomero, Kilosa, na Ulanga wanashauriwa kuwasiliana na Halmashauri husika ili waweze kupatiwa fomu maalum za kujaza taarifa hizo muhimu” Alisisitiza Dotto James.
Amesema kuwa zoezi hilo ni endelevu ambapo Serikali itaendelea kufunga mfumo huo kwenye mikoa na Wilaya zote zilizobaki upande wa Tanzania Bara.
No comments:
Post a Comment