Serikali
itaendelea kusimamia ubora wa elimu kwa kuhakikisha shule na taasisi zinadahili
wanafunzi wenye sifa stahiki za kujiunga na kozi wanazoomba.Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 24
Novemba, 2016 katika sherehe za mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania
zilizofanyika Bungo, Kibaha Mkoani Pwani.
Kabla ya Rais
Magufuli kutoa kauli hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Prof. Elifas Tozo
Bisanda alieleza kuwa chuo hicho kimeshindwa kudahili idadi kubwa ya wanafunzi
baada ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kuzuia udahili wa wanafunzi wanaotaka
kujiunga na masomo ya elimu ya juu kwa kutumia sifa ya kupatiwa kozi ya awali (Foundation Course) ambayo imekuwa ikitumiwa na wanafunzi wasio na sifa za
kujiunga vyuo vikuu kwa vigezo vya TCU.
"Kwa vile
mnachukuliwa sawa na vyuo vingine ni lazima mzingatie vigezo vya mtu kuitwa
mhitimu wa Chuo Kikuu, kwa hiyo nasema kwa dhati nakubaliana sana tena kwa
asilimia 100 na yale yaliyozungumzwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Ufundi
Prof. Joyce Ndalichako.
"Kwa hiyo ni
lazima hili suala la kuweka viwango vya ubora wa elimu yetu tulizingatie, ni
mara kumi tuwe na wanafunzi hata 10 wanaohitimu elimu ya juu kuliko kuwa na
wanafunzi 20,000 wakati hawana sifa, kwa sababu tutakapokwenda kwenye ajira
hatutauliza kama huyu ametoka Chuo Kikuu Huria, huyu ametoka Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam ama huyu ametoka Chuo Kikuu cha Dodoma, wote tutawaangalia kwa usawa.
"Tusitafute
njia ya mkato, njia ya mkato ni mbaya, kwa hiyo kwa hili kwa kweli Mhe. Prof.
Ndalichako nakubaliana na wewe, nafikiri ndio maana umekuwa Waziri wa Elimu,
tunataka kulinda hadhi ya elimu yetu"
amesema Dkt. Magufuli.
Hata hivyo, Rais
Magufuli amekipongeza Chuo Kikuu Huria kwa kazi nzuri ya kutoa elimu ya juu kwa
Watanzania wengi na kuanzisha matawi katika nchi mbalimbali za Afrika na
ameahidi kuwa Serikali yake itaendelea kuunga mkono juhudi hizo ikiwa ni pamoja
na kukabiliana na changamoto za miundombinu na mahitaji mengine.
Aidha, Rais
Magufuli amewaonya viongozi na watendaji wa taasisi mbalimbali za Serikali ambao
wamekuwa wakitumia vibaya fedha za umma ikiwemo kuweka fedha nyingi za Serikali
katika akaunti za muda maalum (Fixed
Deposit Account) kwenye benki za biashara ambako hujipatia fedha kupitia
faida ya akiba bila kujali kuwa vitendo hivyo husababisha Serikali kukosa fedha
na kulazimika kukopa kutoka benki za biashara ambako hutozwa riba kubwa.
"Sasa
sifahamu kama Chuo Kikuu Huria na nyinyi mmekuwa mkiweka fedha za maendeleo
katika Fixed Deposit Account, lakini huo ndio umekuwa ni mchezo, juzi hapa
tumekuta fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 26 zilizokuwa zimetolewa na Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya matumizi ya TRA, zikapelekwa kwenye benki
tatu kama Fixed Deposit Account na Bodi ya TRA ikapitisha, ndio maana
nilipozipata hizo taarifa, fedha nikachukua na Bodi kwa heri.
"Hata kwa
sasa hivi Waziri upo hapa, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo ilianzishwa
kwa sababu maalum, inachangiwa fedha wakati kuna fedha zao wameziweka kwenye
Fixed Deposit Account, Waziri hiyo ni message sent and Delivered"
amesisitiza Rais Magufuli.
Katika Mahafali
hayo, Mkuu wa Chuo Kikuu Huria na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza
Peter Pinda amewatunuku shahada na vyeti jumla ya wahitimu 4038, wakiwemo
wahitimu 8 wa shahada ya Uzamivu, 217 wa shahada ya Uzamili, 111 wa Stashahada
ya Uzamili, 1,186 wa Shahada ya Kwanza, 484 wa Stashahada na 1,421 wa vyeti
mbalimbali.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
24 Novemba,
2016.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akisalimiana
na baadhi ya wahitimu wa Shahada ya Uzamivu ya Udaktari wa Falsafa
wakati wa mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania yaliyofanyika kwenye kampasi ya chuo hicho huko huko Bungo,
Kibaha, mkoa wa Pwani leo Novemba 24, 2016.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akisalimiana
na baadhi ya wahadhiri wakati wa mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria
cha Tanzania yaliyofanyika kwenye kampasi ya chuo hicho huko huko Bungo,
Kibaha, mkoa wa Pwani leo Novemba 24, 2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akipiga
makofi wakati Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Waziri Mkuu
Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda akimtunuku Shahada ya Uzamivu ya Udaktari wa
Falsafa mhitimu Hebson Opiyo Andala kutoka Rwanda wakati wa mahafali ya
31 ya chuo hicho yaliyofanyika kwenye kampasi ya OUT huko Bungo,
Kibaha, mkoa wa Pwani leo Novemba 24, 2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akihutubia
wakati wa mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika
kwenye kampasi ya chuo hicho huko huko Bungo, Kibaha, mkoa wa Pwani
leo Novemba 24, 2016
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa, Joyce Ndalichako akihutubia
wakati wa mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania yaliyofanyika kwenye kampasi ya chuo hicho huko huko Bungo,
Kibaha, mkoa wa Pwani leo Novemba 24, 2016.
Mkuu
wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe.
Mizengo Pinda akimtunuku Shahada ya Uzamivu ya Udaktari wa Falsafa
mhitimu Philip Filikunjombe wakati wa mahafali ya 31 ya chuo hicho
yaliyofanyika kwenye kampasi ya OUT huko Bungo, Kibaha, mkoa wa Pwani
leo Novemba 24, 2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa
na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi Profesa, Joyce Ndalicha ko, Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania (OUT) na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo
Pinda, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Profesa
Samuel Wangwe Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Elifas Bisanda
wakiondoka jukwaa kuu baada ya kuhitimisha mahafali ya 31 ya chuo hicho
yaliyofanyika kwenye kampasi ya OUT huko Bungo, Kibaha, mkoa wa Pwani
leo Novemba 24, 2016.
PICHA NA IKULU
No comments:
Post a Comment