NA DAUDI MANONGI, MAELEaZO.
Novemba 5 mwaka 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli ametimiza mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani akiwa na dhamira mpya ya serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mara kadhaa Rais Magufuli amekuwa akisisitiza umuhimu wa viwanda ambapo anasema vinaweza kutengeneza ajira kwa watanzania waliojiajiri wakiwemo vijana wanaohitimu vyuo mbalimbali nchini.Katika kutimiza azma iyo aliagiza mifuko ya Hifadhi ya Jamii ijikite zaidi kwenye uwekezaji wa viwanda ili kuunga mkono lengo la Serikali.
Katika kutekeleza agizo la Rais Magufuli tayari mfuko wa Pensheni wa PPF umeanza kutekeleza agizo hilo kwa kuingia ubia na jeshi la Magereza na kuanzisha kiwanda cha kuzalisha viatu na bidhaa za ngozi.Makubaliano haya yalisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa PPF Bw.William Erio na Kamishna Jenerali wa Magereza Bw.John Minja Octoba 4, 2016 katika ukumbi wa mikutano wa makao Makuu ya Jeshi la Magereza uliopo Jijini Dar es Salaam.
Aidha katika makubaliano hayo PPF itakarabati na kuboresha miundombinu ya kiwanda cha viatu cha karanga ambacho uzalishaji ulianza mwaka 1977 na kufunguliwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Pamoja na kiwanda cha sasa PPF itajenga kiwanda kipya cha kisasa ambacho kitakuwa kikisindika ngozi na kuzalisha bidhaa zitokanazo na ngozi kwa kutumia mashine za kisasa na teknolojia ya hali ya juu na hivyo kuongeza uzalishaji na kupanua masoko ya viatu nchini na kuongeza pato la Taifa.
Akizungumza wakati wa kutiwa saini mkataba wa makubaliano Mkurugenzi Mkuu wa PPF Bw. William Erio alisema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ni utekelezaji wa lengo la Serikali la kuwa na uchumi wa viwanda na faida kubwa kwa nchi kwa kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini kwa ajili ya soko la ndani na hivyo kuokoa matumizi ya fedha za kigeni ambazo zingetumika kununua malighafi mbalimbali kutoka nje ya nchi.
Vile vile kiwanda hicho kipya kitatoa ajira kwa watanzania lakini pia PPF itanufaika kwa faida itokanayo na uwekezaji pamoja na kupata wananchama wapya watakaojiunga na mfuko huo.
Aidha Mkurugenzi Mkuu wa PPF Bw.William Erio alisema uzalishaji katika kiwanda kipya cha uchakataji ngozi unatarajiwa kuanza mwaka 2018 na kwamba katika kipindi ambacho ujenzi wa kiwanda kipya utakuwa unaendelea kile cha zamani kitaboreshwa ili kuongeza zaidi ufanisi wa uzalishaji.
Katika hatua nyingine mfuko wa PPF umeanza hatua za awali za kuwekeza katika kiwanda cha Sukari eneo la Mkulazi lililopo kilometa 195 kutoka Manispaa ya Morogoro na km 75 kutoka Ubena-Zomozi barabara kuu ya Dar es Salaam na Morogoro ambapo uwekezaji huo utafanyika kwa ubia kati ya PPF na NSSF kwenye eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 63000 ambapo tayari kampuni ya pamoja imeshaanzishwa azma hiyo.
Kiuchumi eneo la Mkulazi liko karibu na Reli ya kati kwenye kituo cha Ngerengere na lipo karibu na Reli ya TAZARA kupitia kituo cha kidunda hivyo uwekezaji katika eneo hilo utafanya usafirishaji wa malighai na bidhaa kuwa rahisi.
Kiwanda hicho kitazalisha zaidi ya tani 200,000 za Sukari kwa mwaka lakini pia kitatoa ajira za moja kwa moja na ajira shirikishi kwa watanzania zaidi ya 100000 na hivyo kutimiza lengo la Rais na Serikali yake katika kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira pamoja na kuongeza pato la Taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa PPF Bw.William Erio alisema uwekezaji huu utafanyika katika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itahusisha uzalishaji wa Miwa na ujenzi wa kiwanda cha Sukari na awamu ya pili utahusisha kilimo cha nafaka kama vile Mahindi,Mpunga na Mtama.
PPF itaendelea kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika kufanikisha azma yake ya Tanzania ya viwanda kwa kuwekeza katika maeneo yenye tija kwa mfuko ili kukuza uwekezaji na tija kwa wanachama na jamii kwa ujumla.
Katika kuzidi kuunga mkono Serikali ya awamu ya tano na falsafa yake ya “Hapa kazi tu” PPF itafanya uwekezaji wa ujenzi wa jengo la kiwanda kwenye kiwanda cha nguo cha Touku kilichopo eneo la Mabibo katika ukanda maalumu wa kiuchumi wa Benjamin Mkapa ambapo kiwanda hiki huzalisha nguo zenye ubora kwa ajiri ya soko la Marekani kupitia mpango wa ukuzaji fursa za kiuchumi Afrika AGOA(African Growth and Opportunity Act uku uwekezaji wa Jengo la kiwanda utapanua wigo wa ajira kwa watanzania kutoka 1600 waliopo sasa mpaka kufikia ajira 7000.
Mfuko wa PPF unaendelea kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kuwafikia watanzania wajasiriamali ili kuboresha biashara na maisha yao.
Sanjari na hilo tayari PPF imeanzisha mfumo wa uchangiaji wa hiari ujulikanao kama Wote Scheme ambao unawalenga wanachama waliojiajiri wenyewe katika sekta isiyo rasmi ambao kwa mujibu wa takwimu za kitaifa sekta hiyo inachukua zaidi ya asilimia 90 ya nguvu kazi ya Taifa.
Mfuko huu unawalenga watu waliojiajiri katika makundi ama mtu mmoja wakiwemo wakulima, wavuvi, wafugaji, madereva wa daladala, bodaboda ,mabasi,Teksi,Mama lishe,Wajasiriamali mbalimbali wenye maduka na biashara nyingine pamoja na vikundi vya Vikoba.
Kwa kupitia mfumo wa wote Scheme watanzania watakuwa na uhakika wa kupata bima ya afya,mkopo wa elimu na maendeleo ya biashara pamoja na pensheni ya uzeeni endapo mwanachama atafikia kiwango cha kustaafu.
Kupitia mfumo wa wote scheme watanzania watakuwa na uhakika wa kupata bima ya afya,mkopo wa elimu na maendeleo ya biashara pamoja na pensheni ya uzeeni endapo mwanachama atafikia kiwango cha kustaafu.
Kupitia mfumo wa wote scheme mwanachama anaweza kuchangia kiwango kisichopungua elfu ishirini kwa mwezi au zaidi na mfumo huu ni rahisi sana ambapo wanachama wanaweza kulipa michango yao kwa simu ya mkononi kupitia mifumo kama vile M-pesa,Airtel Money,Tigo Pesa popote pale walipo eneo lao la kazi bila hata kufika ofisi za PPF.
Pamoja na hayo tunayaomba makundi mbalimbali ya wajasiriamali walioko katika sekta isiyo rasmi kujiunga na mfumo huu kwa faida ya maisha yao ili waweze kufaidika na huduma mbalimbali zinazotolewa katika mfumo huu.
Pamoja na Mfuko wa PPF kusajili wanachama kukusanya michango kuwekeza na kulipa mafao imekuwa mstari wa mbele kuchangia katika shughuli za kijamii kama vile afya,elimu na kuchangia kwenye maendeleo ya jamii katika kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano kwenye sekta ya elimu mfuko wa PPF umekuwa mstari wa mbele kuchangia changamoto ya upungufu wa madawati kwa shule za msingi na sekondari kitaifa.
PPF imeendelea kuunga mkono mpango wa serikali katika kutatua changamoto ya madawati kwenye shule mbalimbali ambapo mfuko umechangia shilingi milioni 200 katika kufanikisha mpango huo uku lengo kuu la mfuko wa PPF likiwa ni kuhakikisha wanafunzi hawasomi wakiwa wamekaa chini kwani ndio nguvu kazi ya Taifa la Kesho na ni wanachama watarajiwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo PPF.
No comments:
Post a Comment