Mgahawa mkubwa unaotoa huduma za
chakula cha Kitanzania unaomilikiwa na mpishi maarufu duniani, Issa
Kapande `Chef Issa', umefunguliwa nchini Sweden na kuvunja rekodi ya
dunia.Mgahawa huo ulizinduliwa na balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mh. Dora Msechu.
Balozi
Msechu alimpongeza Issa Kapande na mkewe kwa kufanikisha kuwapo kwa
mgahawa huo ambao umeweka rekodi kuwa mgahawa mkubwa kuliko yote ya
Kiafrika katika nchi za Ulaya.
Aidha, alimshukuru Torvald Brahm
mwenyeji wa mji huo kwa kumuunga mkono Issa hadi kufanikisha ndoto yake
ya kuwa na mgahawa wa kwanza wa Kiafrika katika mji wa Trollhattan
utakatoa huduma ya chakula cha kitanzania.
Katika uzinduzi huo
ambapo wenyeji wa manispaa hiyo akiwemo Meya na mwenyekiti wa
Trollhattan, Paul Akerlund na msaidizi wake Peter Eriksson walikuwepo,
balozi ambaye ndio kwanza ameanza kazi alielezea kufurahishwa na juhudi
za Kapande.
Alisema Issa ameonesha njia kwamba inawezekana kwa
watu waliopo Ughaibuni sio tu kuajiriwa, bali kujiajiri katika nyanja
mbalimbali.Alisema hilo linawezekana kutokana na kufuatilia kwa karibu
taratibu za wenyeji na kisha kutumia mafunzo yaliyopo kukamilisha
ndoto."Ni dhahiri kuwa, Chef Issa kwa kupitia taaluma yake ya
upishi amewezeshwa kumiliki mgahawa huu hapa Trollhattan,S weden kwa
hilo, napenda tuishangilie na kuipigia makofi Sweden na
Trollhattan."Alisema akimpongeza kijana huyo ambaye pia amewekeza mkoani
Mtwara.
Katika mahojiano, Mpishi Mkuu Issa Kapande alisema
mafanikio yake yanatokana na juhudi kubwa na nia aliyoiweka katika
kujifunza na kufundisha wengine katika mitandao ya wapishi wakuu.
Alisema
akiwa amefanyakazi katika nchi 17 na tayari akiwa na vitega uchumi
nchini alianzia nia ya kuwekeza Sweden mwaka 2009 wakati alipohamia
nchini humo akitokea Uswisi. Alisema alianza kwa kuomba vibali, lakini
mchakato kamili ulianza mwaka 2013."Tulilazimika kufanya utafiti kidogo"
alisema na kuongeza kuwa katika utafiti huo walihoji watu 300 na kujua
mwelekeo hasa wa shughuli yao unastahili kuwaje.
Kapande ambaye
ni mhitimu wa chuo kikuu cha Manchester Metropolitan na Chuo kikuu cha
kimataifa cha menejimenti ya hoteli cha Uswis amesema amepambana vikali
na mkewe hadi kufikia hatua ya kuanzisha mgahawa huo ambao upo katika
eneo la ukubwa wa skwea mita 810.Kapande ambaye mwaka jana alitwaa tuzo
ya dhahabu katika upishi akiwa na timu ya Sweden magharibi alisema kuna
umuhimu mkubwa kwa wapishi wa nyumbani kukubali kubadilika na kufanya
kazi kwa pamoja kwa lengo la kujifunza na kufunza ili kuwa na aina
nyingine ya mapishi katika kuendeleza sekta.Ndani ya mgahawa huo pia watu mbalimbali watapatiwa taarifa za utalii Tanzania.
Katika
kazi yake ya upishi, amebahatika kuwapikia watu mashuhuri duniani,
baadhi wakiwa Andrew Young, Mchungaji Jesse Jackson, Robert Mugabe (Rais
wa Zimbabwe), Paul Kagame (Rais wa Rwanda), Benjamini Mkapa (Rais
mstaafu wa Tanzania), Raila Odinga (Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya),
Daniel Arap Moi (Rais Mstaafu wa Kenya), Waziri wa Mambo ya Nje wa
Marekani Bi. Hillary Clinton na mumewe Bill Clinton, Mke wa Rais wa
zamani wa Marekani Laura Bush.
Wengine ni Rais wa Zanzibar Dk. Ali
Mohamed Shein, mwigizaji Chris Tucker, Rais wa zamani wa Afrika Kusini
hayati Mzee Nelson Mandela, Koffie Olomide, Youssour ndour, Arsene
Wenger (Kocha wa Arsenal ya England), Gianluca Vialli (nyota wa zamani
wa Italia aliyewahi kuichezea na kuinoa Chelsea ya England), Rais wa
Congo DRC, Joseph Kabila, Billy Gates na wengine wengi.
No comments:
Post a Comment