Thursday, November 17, 2016

MAKAMU WA PILI RAIS ZANZIBAR BALOZI SEIF ALI IDDI AZINDUA JENGO LA MAABARA YA SKULI YA KITOPE

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikata utepe kuashiria kuzindua pamoja na kukabidhi Jengo la Maabara la Skuli ya Sekondari ya Kitope aliloligharamia yeye pamoja na ufadhili wa Ubalozi China Nchini Tanzania na Kampuni ya simu za mkononi yaTigo.
Mwalimu wa Masomo ya Sayansi wa skuli ya Sekondari Kitope Mwalimu Ali Mohamed aliyeshika kifaa cha Maabara akimuelezea Balozi Seif  urahisi wa kazi yao ya ufundishaji kwa sasa baada ya kupata  Maabara yenye kukidhi kiwango kinachokubalika kwa skuli za Sekondari.
Mwalimu Ali Mohamed akiendelea kutoa maelezo kwa Balozi Seif  jinsi wanafunzi wa masomo ya sayansi katika skuli yao walivyofarajika kutokana na kujengewa maabara iliyokamilika kwa kazi zao za vitendo.
 Mwalimu Wanu Ndende Juma akiwasilisha Risala ya walimu na wanafunzi wa skuli ya Sekondari ya Kistope kwenye hafla ya uzinduzi na kukabidhiwa rasmi jengo la Maabara ya skuli hiyo lililomalizika kujengwa pamoja na kuwekwa vifaa vyake.
Baadhi ya Wanafunzi wa skuli ya sekondari ya Kitope wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyojiri kwenye uzinduzi wa maabara ya skuli yao.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Ndugu Issa Juma akitoa salamu katika hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la maabara ya skuli ya sekondari ya kitope.
 Waziri wa Elimu Mh. Riziki Pemba Juma akimshukuru Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif  kwa uzalendo wake wa kuunga mkono sekta ya Elimu wakati wa hafla ya uzinduzi wa Maabara ya skuli ya Kitope.

Picha na – OMPR – ZNZ.
                             
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliitahadharisha Jamii  kuelewa kwamba maendeleo kwa wana Taaluma wa Fani ya Sayansi iwe Maskulini au vyuoni  yataendelea kuwa ndoto iwapo  hakutakuwa na mipango imara ya  kuimarisha miundombinu kwenye Majengo ya Maabara katika maeneo husika.

Alisema Wazazi kwa kushirikiana na Kamati za Maskuli na vyuo kupitia usimamizi wa Wizara inayosimamia masuala ya Elimu bado wana jukumu la kuhakikisha vilio vya Wanafunzi kutokana na kukabiliwa na ukosefu wa Maabara kwenye Taasisi zao vinamalizika.

Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda alitoa tahadhari hiyo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi pamoja na kulizindua rasmi Jengo la Maabara ya Skuli ya Sekondari ya Kitope iliyomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “B”.

Jengo hilo aliloligharamia yeye pamoja na kupata msaada wa nguvu za ufadhili wa baadhi ya vifaa kutoka Ubalozi wa Jamuhuri ya Watu wa China na Kampuni ya mitandao ya simu za mkononi ya Tigo limegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni 38,780,000/-.

Balozi Seif  alisema wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Kitope kwa sasa hawana sababu ya kufanya vibaya katika mitihani yao ya Kitaifa kutokana na kumalizika kwa Jengo hilo la Maabara ambalo lilikuwa kilio kwao na walimu wao kwa karibu miaka Kumi sasa.

Aliwaasa Wanafunzi hao kuhakikisha kwamba Vifaa walivyopatiwa kwenye Maabara ya Skuli yao wataendelea kuvitunza kwa tahadhari  ili viweze kudumu kwa kipindi kirefu na kutumiwa pia na wanafunzi wenzao watakaofuatia baada ya wao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliupongeza na kuushukuru Uongozi wa Ubalozi wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Nchini pamoja na ule wa Kampuni ya Mitandao ya Simu za mkononi wa Tigo kwa upendo wao wa kuunga mkono Sekta ya Elimu hapa Zanzibar.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/11/2016.

No comments: