Friday, November 11, 2016

MAFUNZO YA UFUNGASHAJI BORA,KUWEKA NEMBO,RAJAMU NA MASOKO YAFANYIKA MASASI NA RUANGWA

Mhe Joseph Mkirikiti akikabidhi lebo za vifungashio kwa Bi Safina Selemani mzalishaji wa mafuta ya alizeti kutoka kata ya Nandagala B kikundi cha CHIUKUTE, lebo hizo zimetengenezwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya Tanzania (TanTrade)
Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mhe Joseph Mkirikiti akipokea lebo za vifungashio kwa wazalishaji wa mafuta ya alizeti katika mkoa wa Ruangwa kata ya Nandagala B kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya Tanzania (TanTrade) Bw Edwin Rutageruka

MAFUNZO YA UFUNGASHAJI BORA, KUWEKA NEMBO, RAJAMU NA MASOKO (MASASI & RUANGWA) NA KUTOA LEBO KWA WAZALISHAJI WA MAFUTA YA ALIZETI

Mhe Joseph Mkirikiti Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa ahimiza uzalishaji wa mafuta ya Alizeti, Ufuta na Nazi kwa wingi katika wilaya ya Ruangwa sababu ni kioo na msingi imara ya kuwawezesha ajira iwe ya kudumu na tena ajira bora kwa wananchi. 

Hayo aliyasema akiwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo kwa vitendo kwa wakulima ambao ni wazalishaji wa bidhaa za mbegu za mafuta ya ufuta, nazi na alizeti wa Ruangwa na akipokea lebo za vifungashio vya mafuta ya alizeti kwa wazalishaji wa bidhaa za mafuta ya alizeti zaidi ya 1000 zilizotengezwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade). 

Mafunzo hayo yameanza tarehe 7 hadi 10 Novemba, 2016 juu ya namna ya ufungashaji bora wa bidhaa za mbegu za mafuta ya ufuta, alizeti na nazi, kuwa na lebo bora kwenye kila bidhaa inayozalishwa, rajamu (branding) kwenye bidhaa hizo, namna ya kuboresha ubora wa bidhaa na mbinu ya kuuza bidhaa hizo kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi kwa wazalishaji wapatao 50 wa Ruangwa na 50 wa Masasi.

“Elimu mtakayopata hapa itawachukueni kwenye hatua nyingine ya kufanya maboresho makubwa ya ajira yenu, hapa nchini mahitaji ya mafuta ya kula kwa mwaka ni lita 350,000 wakati uzalishaji kwa sasa ni asilimia 40 pekee na asilimia 60 huagizwa kutoka nje ya nchi hivyo basi, tuna fursa kubwa ya kunufaika na sekta hii.” 

Akasisitiza kuwa ni vyema kusikiliza na kutumiamafunzo hayo kwa makini na kwenda kuambukiza elimu hiyo kwa wengine waliokosa kuhudhuria mafunzo haya ili kwa pamoja kama Taifa tufanye biashara yenye faida na kufikia malengo ya Taifa na mtu mmojammoja. 

Mhe Mkirikiti aliendelea kusema kuwa Ruangwa iwe mstari wa mbele sasa katika kuzalisha bidhaa zenye ubora na kupitia msaada wa lebo kutoka TanTrade na vifungashio bora ili bidhaa zionekane kwenye macho ya mlaji kabla ya kutumia na kuleta ufahari kwa nchi ya Tanzania pindi bidhaa zetu zitakavyoweza kuvuka nje ya nchi hivyo watumie mafunzo hayo kutangaza bidhaa zetu bora zaidi. 

Alieleza kuwa anaimani kupitia mafunzo haya yataboresha pia maeneo ya kazi ili ubora usipungue na pia wakiendelezwa wajasiliamali wadogo kutapelekea kuanzishwa viwanda vidogo vingi zaidi na kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mafuta na maendeleo kuja kwa haraka sana na kupunguza kwa kiwango kikubwa kuagiza mafuta kutoka nje.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendelo ya Tanzania (TanTrade) alisema moja ya kazi ya taasisi ni kuwajengea uwezo na kuwaendeleza wazalishaji wadogo, hivyo imeandaa mafunzo haya kwa ushirikiano wa wadau wa kimkakati ambao ni SIDO na TBS ilikuimarisha fursa kwa wakulima kuzalisha kitu cha thamani ili kuweza kuleta ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.

“Mwezi Agosti kwenye maadhimisho ya siku ya wakulima (88), TanTrade ilifanya ziara fupi kwenye wilaya za Ruangwa, Masasi na Kilwa na pia kupita kwenye mabanda ya washiriki kubaini fursa zilizopo kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara kupitia vikundi mbalimbali vilivyoshiriki maadhimisho hayo ili kuendeleza fursa hizo kwenye masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi.”

Akaongeza kwa kusema kuwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya Tanzania (TanTrade) ilipobaini changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye kilimo biashara (Agribusiness) hivyo ikaona ni vyema kutatua changamoto hizo kwa kuanza kuwajengea uwezo wazalishaji wa bidhaa hizo kwa kutoa mafunzo kwa vitendoyatakayojikita kwenye mbinu za kutafuta masoko na mikakati ya kuingia sokoni, uzalishaji wa viwango vyenye ubora wa mbegu za mafuta (Alizeti, Ufuta na Nazi) na vifungashio vya mafuta hayo, Nembo ya utambulisho wa bidhaa zao (lebo) na elimu juu ya mfumo wa matumizi ya simbomilia (barcode) na nembo ya ubora katika wilaya ya Ruangwa na Masasi na kuwatengeneza lebo ili bidhaa zao ziweze kutambulika kwenye masoko yao. 

Akishukuru kwa niaba ya kikundi cha CHIUKUTU kilichopo kata ya Nandagala B wilaya ya Ruangwa Bibi Safina Selemani baada ya kupokea lebo kwaajili ya bidhaa zao kutoka kwa Mkuu wa Wilaya alisema changamoto kubwa ilikuwa ni ukosefu wa elimu ya namna ya uboreshaji wa uzalishaji bora wa bidhaa za mafuta, hivyo ni fursa ya pekee kwao kupatiwa mafunzo na lebo hizo ili kujiendeleza kwenye uzalishaji. 
























No comments: