Wednesday, November 9, 2016

HOTUBA YA MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, KATIKA SEMINA YA WABUNGE KUHUSU UDHIBITI WA UGONJWA WA KIFUA KIKUU NCHINI TANZANIA, UKUMBI WA BUNGE, 8 NOVEMBA, 2016.

·        Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Mhe. Job Ndugai,
·        Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania -
Mhe. Tulia Akson,
·        Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  -
Mhe. Andrew Chenge,
·        Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania -
Dkt. Thomas Kashilila,
·        Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe,
·        Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii Mhe. Peter Serukamba,
·        Wenyeviti wa Kamati mbali mbali za Bunge,
·        Waheshimiwa wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi kukushukuru kwa dhati kwa kutupatia fursa nyingine ya kuongea na Waheshimiwa wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu masuala ya maendeleo katika sekta ya Afya na kwa siku ya leo ajenda yetu ni ‘Janga la ugonjwa wa kifua kikuu’ nchini mwetu.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa kukubali kuhudhuria semina hii muhimu ili kupata fursa ya kuliangalia tatizo la Kifua kikuu kwa kina na kuishauri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto juu ya maboresho muhimu  ili kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya Kifua kikuu. Nawaahidi kwamba, Wizara yangu itazingatia ushauri wa Waheshimiwa wabunge katika kuboresha mapambano dhidi ya ugonjwa huu.

Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi, kwa hotuba nzuri uliyoitoa hivi punde wakati wa ufunguzi wa semina hii. Ni kweli kabisa, kifua kikuu au TB ni ugonjwa hatari, yatupasa kufanya juhudi za kipekee na za ziada ili kuiokoa jamii yetu na janga hili.  Aidha, naomba nimpongeze Mhe. Peter Serukamba, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii kwa salamu zake na maneno yenye hekima kubwa juu ya wajibu wetu katika kukabiliana na tatizo hili la kifua kikuu hapa nchini mwetu. 
Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii pia, kuwashukuru wale wote waliohusika katika kuandaa semina hii ikiwa ni pamoja na wadau wetu wa maendeleo wa shirika la kimataifa la kupambana na Kifua kikuu la KNCV linalosimamia mradi wa Challenge TB unaofahiliwa na USAID. 
Mheshimiwa Spika, kama nilivyobainisha katika hotuba yangu ya bajeti kwa mwaka 2016/17, katika mwaka huu wa fedha wa 2016/17 Wizara inaweka juhudi za kipekee katika kuongeza wigo wa mapambano dhidi ya kifua kikuu na kuboresha mikakati ya uibuaji wa wagonjwa wapya ili kupunguza ukubwa wa tatizo la Kifua kikuu hapa nchini mwetu. Aidha katika tamko langu wakati wa maadhimisho  ya siku ya kifua kikuu Duniani mnamo mwezi Machi, 2016 nilitoa wito wa kumtaka kila mtanzania na taasisi mbali mbali kujiunga pamoja na kuisaidia serikali kutimiza azima yake ya kutokomeza kifua kikuu hapa nchini katika miaka 20 ijayo. 
Mheshimiwa Spika, Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ilikuwa: “Tuungane  Kutokomeza Kifua Kikuu” kwa lugha ya kiingereza: “Unite To End TB” Kauli mbiu hii inaweka msukumo wa kipekee kwa nchi yetu kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya kifua kikuu ili kuibua wagonjwa wengi zaidi, kuwaweka katika matibabu na kuzuia maambukizi mapya. Kauli mbiu hii inatoa pia chagizo kwa nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ikiwemo Tanzania, katika utekelezaji wa mkakati mpya (Global End TB Strategy 2016-2035) wa Dunia wa utokomezaji wa kifua kikuu ifikapo mwaka 2035. 
Mheshimiwa Spika, Mkakati huu unatutaka kuongeza kasi ya juu kabisa katika kuutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu, ili kuwafikia wahitaji na wagonjwa wote, kupunguza kasi ya idadi ya wagonjwa wapya kwa asilimia 90, kuwatibu na kuwaponyesha wote, kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa kifua kikuu kwa asilimia 95 na kukomesha masumbukizo yote yatokanayo na kifua kikuu katika jamii yetu. 
Mheshimiwa Spika, Kifua kikuu kinaleta madhara ya kiafya na huongeza umasikini katika jamii.  Nchini kwetu takriban watu 160,000 huugua kila mwaka na ni wagonjwa 62,180(39%) tu wanagunduliwa na kuwekwa katika matibabu. Miongoni mwa hawa tunaowaweka kwenye matibabu asilimia 90 hupona kabisa. Kwa misingi hiyo, Wizara yangu imeona litakuwa jambo la kheri kukutana na Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge lako Tukufu, kama wadau wakuu na wawakilishi wa wananchi ili kulijadili janga hili angalau kwa muda huu mfupi tulioupata. 
Tunahitaji ushiriki wa kila mtu katika vita hii na kama kauli mbiu inavyoonyesha “TUNAHITAJI KUUNGANISHA NGUVU”. Bunge letu ni chombo nyeti na ushiriki wake unaweza kufanya tofauti kubwa na kuleta tija katika maboresho ya mkakati wa azma ya Taifa letu kuelekea Tanzania isiyo na TB. 
Mheshimiwa Spika, Takwimu zinatuonyesha ya kuwa, takribani asilimia kati ya 30 na 50 ya watanzania wote tayari wameambukizwa Kifua kikuu, yaani watu wapatao million 25. Kwa maneno mengine ni kwamba, pengine hata nusu yetu hapa ukumbini tayari tunayo maambukizi ya TB na endapo kinga yetu itashuka kwa sababu yoyote ile, ugonjwa wa TB utatukumba na kuhitaji kupatiwa matibabu sahihi na kwa wakati. 
Mheshimiwa Spika, Kama tulivyoona, kifua kikuu ndiyo ugonjwa pekee ambao watanzania wengi zaidi wanaishi na vimelea vyake mwilini. Hii ina maanisha na kueleza wazi hatari tuliyo nayo katika jamii yetu. Yatubidi kuchukua hatua za makusudi kuongeza uwekezaji wa rasilimali nyingi zaidi katika mapambano hayo ili kukiokoa kizazi hiki na kijacho. Makundi ya wazee, watoto, watu wanaoishi na maambukizo ya VVU, watu wenye magonjwa hatari ya kudumu kama vile kisukari na kansa, watu walio migodini, wanafunzi katika shule za bweni, wafungwa magerezani, kambi za wakimbizi hawa wote wapo katika hatari kubwa zaidi ya kuugua ugonjwa wa kifua kikuu. 
Mheshimiwa Spika, Ni matarajio yetu ya kuwa mkutano huu, utatoa fursa kwa Waheshimiwa Wabunge kupata uelewa zaidi juu ya hali ilivyo, ukubwa wa tatizo la kifua kikuu hapa nchini na kuwawezesha kuona ni namna gani wanaweza kushiriki katika mapambano dhidi ya janga hili la kifua kikuu. Kuna masuala ya kuhimiza ushiriki kikamilifu wa wananchi, Halmashauri zetu na Taasisi mbali mbali katika vita ya udhibiti wa kifua kikuu. Yapo pia masuala ya bajeti ya kifua kikuu; kwa miaka mingi imekuwa ikitegemea wafadhili kwa zaidi ya asilimia 90 na sasa tunaona wakipunguza misaada yao. Yote haya yanahitaji msukumo wa kisiasa na kisera pia. 
Mheshimiwa Spika, Katika semina hii tutapokea mada mbili kuu, moja itawasilishwa na Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na nyingine ataitoa Mhe. Dkt Faustin Ndungulile, Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Mwenyekiti wa kamati ya UKIMWI, mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na mwanachama mwanzilishi wa Bunge lako Tukufu katika “Global TB Caucus pamoja na Afican TB Caucus”. Mada hizi zitachokoza tu na Waheshimiwa watapata muda wa kutosha kuchangia kwa kutoa ushauri na kuuliza maswali pale ambapo kunahitaji ufafanuzi. Mada hii itafuatiwa na uzinduzi rasmi wa “Tanzania TB Caucus”. 
Mheshimiwa Spika, Naomba nimalizie kwa kushukuru sana tena sana kwa kutupatia fursa hii adimu ya kujadili janga la TB na Waheshiwa Wabunge na napendekeza kikao hiki kiweze kuweka maazimio ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu ushiriki wao na Bunge lako Tukufu katika mapambano dhidi ya TB na kuyapa sura ya utekelezaji katika ngazi zote.
Baada ya kusema hayo narudisha nafasi kwa Mwenyekiti wa Bunge ili kuendelea na taratibu nyingine.


Asanteni kwa kunisikiliza.

No comments: