Naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akitoa maelekezo kwa Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), mkoa wa Mbeya Bw. Issa Hamadi alipokagua uwanja wa ndege wa Songwe Mkoani Mbeya.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (wa pili kushoto), akikagua na kupata maelezo ya njia ya kuruka na kutua ndege katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe Mkoani Mbeya, kulia kwa waziri ni Kaimu Meneja wa uwanja huo Bw. Amir Hamis.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (mwenye miwani) akikagua kifaa cha kupima kiasi cha jua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe Mkoani Mbeya.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akitoa maelekezo kwa mkandarasi DB Shapriya anayejenga jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe Mkoani Mbeya.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akikagua daraja katika reli ya TAZARA mkoani Mbeya na kusisitiza uboreshwaji wa haraka wa mazingira katika nguzo za daraja hilo ili kutoathiri daraja hilo na reli kwa ujumla.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akikagua mashine aina ya (traction motor), inayotumika kuendeshea injini ya gari moshi alipokagua karakana ya utengenezaji wa vichwa vya treni ya TAZARA Mkoani Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Amosi Makalla akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani walipokutana kutathimini ziara ya Naibu Waziri huyo mkoani Mbeya.
…………………………………………………………………..
Viongozi na wafanyakazi wa taasisi za Serikali wametakiwa kubadilika kimtazamo ili kwenda sambamba na malengo na matarajio ya Serikali ya awamu ya tano katika kukuza uchumi wa viwanda na kuongeza ajira.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amesema Serikali imedhamiria kufufua na kuyawezesha mashirika yake yote kufanya biashara na kuzalisha faida ili kujitegemea na kuachana na utegemezi wa ruzuku toka Serikalini.
Akizungumza katika majumuisho ya ziara yake ya siku tatu mkoani Mbeya Eng. Ngonyani amezitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA), na Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) kubuni vyanzo vya mapato.
“Fanyeni kazi kwa ubunifu ili mzalishe faida na kuwa na uwezo wa kujiongezea mishahara na stahili mbalimbali, acheni kulalamika na kutegemea ruzuku ya Serikali katika kila jambo”. Amesisitiza Eng. Ngonyani.
Amewataka TAA kuhakikisha ndege nyingi zinautumia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe kwani ukitumika vizuri unaweza kuwa kitovu cha uchumi kwa ukanda wa kusini na nchi jirani kutokana na ubora wake.
Naibu Waziri huyo amezungumzia umuhimu wa TAZARA kutafuta soko la ndani badala ya kutegemea soko la nje pekee kwani kufanya hivyo kutapunguza mizigo mingi inayosafirishwa kwa njia ya barabara na kuhamia kwenye reli hali itakayopunguza msongamano na uharibifu wa barabara.
Ameziagiza taasisi zilizo chini ya Wizara ya ujenzi kuiamini TEMESA, kufanya kazi na taasisi hiyo na kulipa madeni zinazodaiwa ili kuiwezesha kukua na kuaminika kwa taasisi nyingine na sekta binafsi.
Akizungumza kwa niaba ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mwenyekiti wa taasisi hizo Eng. Paul Lyakurwa amesema taasisi hizo zimejipanga kuboresha miundombinu ya reli, barabara na mawasiliano ya simu na anga ili kufungua mikoa ya nyanda za juu kusini na sehemu nyinginze za nchi na hivyo kuwezesha usafirishaji wa mazao na bidhaa zilinazozalishwa katika mikoa hiyo kufika sokoni kwa wakati.
Naibu waziria Ngonyani amekuwa katika ziara ya siku tatu Mkoani Mbeya ambapo pamoja na mambo mengine amekagua meli mbili za mizigo zinazojengwa katika Ziwa Nyasa, miradi ya barabara katika Wilaya ya Kyela, Busokelo na Rungwe na kukagua uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe na Karakana ya kutengeneza vichwa vya treni ya TAZARA.
No comments:
Post a Comment