Tuesday, November 15, 2016

DC CHATO – USHIRIKIANO WA PLAN INTERNATIONAL UMEFANIKISHA KUDHIBITI AJIRA ZA WATOTO MSASA

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Mkuu wa Wilaya ya Chato iliyopo mkoani Geita, Shaban Ntarambe amekiri kuwa ushirikiano wa shirika la Plan International katika kudhibiti ajira hatarishi za watoto umefanikiwa kumaliza tatizo hilo katika Kijiji cha Msasa.

Hayo yamesemwa leo mkoani Geita na Mkuu huyo alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hii juu ya mchango wa Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na Vitendo vya Ukatili kwa Watoto unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na kuratibiwa na shirika la plan International jinsi ulivyowasaidia wananchi wa Kijiji hicho.

Ntarambe amesema kuwa ushirikiano wa Shirika hilo, jamii pamoja na uongozi wa migodi iliyopo kwenye Kijiji hicho umesaidia katika kuhakikisha elimu ya ajira, afya na usalama kwa watoto inatolewa, hivyo kupitia elimu hizo wananchi wamepata uelewa juu ya athari za ajira za watoto na kujumuika katika uzuiaji wa ajira hizo.

“Tumefanikiwa kwa asilimia zote kuzuia ajira za watoto katika eneo hilo ambalo lina mkusanyiko mkubwa wa wachimbaji wa madini, kimsingi ni kwa sababu ya ushirikiano unaotolewa na shirika la Plan International kwani wanatoa rasilimali nyingi zinazowezesha kufanikisha kuondoa tatizo hilo”, alisema Ntarambe.

Akiongea kuhusu suala la athari wanazopata watoto wadogo wanaobebwa na mama zao wanaofanya kazi migodini amesema kuwa wanasaidiana na shirika hilo katika kuwapatia elimu pamoja na mitaji ili waachane na kazi za migodi na badala yake watafute kazi mbadala za kujitafutia vipato ili kuwakinga watoto wadogo wasiathiriwe na kazi zinazofanyika katika maeneo hayo.

Kwa upande wake Mratibu wa Mawasiliano wa Shirika hilo, Raymond Kanyambo amemshukuru Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kutambua umuhimu wa shirika hilo na kuahidi kuendelea kushirikiana nae katika kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wa wilaya hiyo haswa katika masuala ya unyanyasaji wa watoto na ukatili unaofanywa kwa wanawake.

“Shirika letu linahusika na kutetea haki za watoto, hivyo tuliona ni vyema kupeleka nguvu zetu katika maeneo yenye migodi kwa kuwa ni maeneo yanayoongoza katika utoaji wa ajira za watoto walio na umri chini ya miaka 18, mradi huu ulitekelezwa katika wilaya za Nyan’ghwale na Geita lakini baada ya kuona mafanikio tumeamua kuiongeza wilaya ya Chato ili kukomesha kabisa tatizo hili”, alisema Kanyambo.

Mradi huu wa miaka mitatu una lengo la kuondoa ajira hatarishi na vitendo vya ukatili kwa watoto wanaoishi karibu na maeneo ya migodi, umeanzishwa Novemba 2015 na utagaharimu jumla ya Euro 1,500,000 hadi kuisha kwake.
Mkuu wa Wilaya ya Chato iliyopo mkoani Geita, Shaban Ntarambe akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya umuhimu wa Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na Vitendo vya Ukatili kwa Watoto unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na kuratibiwa na shirika la plan International.
Mratibu wa Mawasiliano wa Shirika la Plan International, Raymond Kanyambo akitoa shukrani kwa Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaban Ntarambe kwa kutambua umuhimu wa Mradi wa Uondoaji Ajira Hatarishi na Vitendo vya Ukatili kwa Watoto unaoratibiwa na shirika hilo.

No comments: