Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilikagua eneo liliopo Mtofaani kwenye Makutano ya Bara bara za Hawaii na Masingi ambalo liliombwa na Wananchi kwa shughuli za Kijamii lakini kwa sasa kuna tetezi ya kumilikiwa na Mtu mwengine.
Balozi Seif akipata ufafanuzi kutoka kwa Mwenyekiti wa Tawi la Mofaani Bwana Iddi Sultan kuhusiana na utata wa eneo hilo linalomilikiwa na mtu binafsi hivi sasa.
Balozi Seif kushoto akiwa nyuma ya Ukuta wa Matofali uliojengwa kati kati ya eneo hilo akijaribu kuangalia upande wa Pili wa eneo hilo lenye utata wa umiliki. Aliyepo upande wa Kulia ni Mwakilishi wa Jimbo la Welezo Mheshimiwa Hassan Khamis Hafid.
Eneo la wazi liliopo Makutano ya Bara bara ya kuelekea Msingini na Hawaii liliopo Mashariki mwa Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Sehemu hilo.
Ukuta wa matofali uliojengwa kati kati ya Eneo la wazi liliopo Makutano ya Bara bara ya kuelekea Msingini na Hawaii lenye kuleta utata wa umiliki wake.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Wananchi wa Shehia ya Mtofaani Masingini ndani ya Jimbo la Welezo wameiomba Serikali Kuu kufikiria maombi yao ya kutaka kupewa eneo lililokuwa likimilikiwa na Kikosi cha Kuzuia Magendo { KMKM } kwa ajili ya kulitumia kwa shughuli zao za Kijamii.
Wamesema eneo hilo ni sehemu pekee iliyowazi kwa shughuli za Kijamii katika shehia ya Mtofaani ambalo linaweza kuwasaidia kwa ujenzi wa Soko,huduma za Afya, Skuli na Michezo ili kuwaondoshea usumbufu Watoto na Wananchi kufuata huduma hizo katika Masafa marefu.
Wananchi hao walipaza sauti zao mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika kukagua eneo hilo baada ya kupokea kilio chao wanacholalamikia eneo hilo kumilikiwa na Mtu aliyetambulika kwa jina Moja tu la Zahor ambae kwa sasa ameshaamua kulizunguushia Ukuta eneo lote.
Walieleza kwamba muda mrefu uliopita Kamati ya Maendeleo ya Eneo hilo kupitia Sheha wa Shehia hiyo iliwahi kupeleka maombi yao ili kupatia eneo hilo lakini jitihada hizo hazikufanikiwa na badala yake kushuhudia ugawaji wa Viwanja uliopelekea kuwavunja moyo.
Walifahamisha kupigwa kwao na mshangao na butwaa pale Vijana wa eneo hilo walipozuiwa na Mtu huyo liyejitambulisha kulimiliki eneo hilo kutofanya shughuli yoyote ya Michezo na Burdani katika Vipindi vya Siku Kuu za Iddi.
Akijibu hoja na kutoa ufafanuzi wa Kilio cha Wananchi hao wa Shehia ya Mtofaani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwaahidi kwamba atamuagiza Waziri anayehusika na masuala ya Ardhi pamoja na Maofisa wake kwa kushirikiana na Uongozi wa Kikosi cha KMKM kufanya uchunguzi wa kina kutambua uhalali halisi wa Mmiliki wa Eneo hilo.
Balozi Seif ameamua kuchukuwa hatua hizo ili kupata Taarifa na Ripoti sahihi itakayobainisha Mmiliki halali wa sehemu hiyo ili Serikali Kuu itakapokuja chukuwa maamuzi isije ikaonea upande wowote.
Eneo hilo la ardhi zamani likitumiwa kwa shughuli za ufyatuaji Matofali lililojengwa ukuta wa matofali kati kati yake likiwa mashariki mwa Msikiti Mkuu wa Ijumaa uliopo Mtofaani makutano ya Bara bara za Masingini na Hawaii linakadiriwa kuwa na ukubwa wa eka Nne.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
24/11/2016.
No comments:
Post a Comment