MKUU wa wilaya ya Arusha, Mhe. Gabriel Fabian Daqarro, amemugiza afisa Usitawi wa Jamii wa halmashauri ya jiji la Arusha kuhakikisha wazee wote wa jiji hilo wanapatiwa vitambulisho kabla ya mwisho wa mwaka huu ili waweze kupata huduma mbalimbali ikiwemo matibabu mahospitalini.
Mhe. Daqaro ametoa agizo hilo kwenye mkutano na wazee wa jiji la Arusha uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ya kimataifa (AICC), ulikuwa una lengo la kusikiliza kero zao ili zipatiwe ufumbuzi na pia kufahamiana.
Mkuu huyo wa wilaya ameiagiza Idara hiyo kuhakikisha vitambulisho vinapatikana kabla ya mwisho wa mwezi ujao, sanjari na kuwataka watendaji wa serikali, mashirika ya umma na taasisi mbali mbali za serikali katika jiji la Arusha kuhakikisha kuwa zinatoa kipaumbele kwa wazee ambao wamekuwa hawapati huduma zao kwa wakati.
Aidha amewataka wenyeviti wa mitaa,kata na tarafa kushirikiana na jeshi la polisi kuhakikisha wanaimarisha usalama kwenye maeneo yao ili kuwezesha wazee kuishi kwa usalama bila kubughudhiwa na kuhakikisha wanasimamia maadili.
‘’Mumepewa madaraka ya kuimarisha ulinzi. Yatumieni ili wazee wasibughudhiwe...Tambueni kuwa wazee ni watu muhimu na ndio waliotufikisha hapa. Sasa sitaki kusikia kuwa wanasumbuliwa... sitaki kusikia malalamiko ya kuporomoka kwa maadili ””alisema Daqarrro.
Wakichangia kwenye mkutano huo wazee wamedai kuwa taasisi za fedha pamoja na halmashauri ya jiji haziko tayari kuwakopesha wazee kwa hofu ya kuwa watakufa karibuni na kutaka dhana hiyo iondoke kwa kuwa kuzeeka sio kufa .
Wamesema nao wana mahitaji mbalimbali ya kuendesha sghuhuli zao za kiuchumi hivyo wanayo haki ya kupewa mikopo kama yalivyo makundi mengine ya jamii.
Wazee hao pia ameomba kushirikishwa kuanzia ngazi ya mtaa hadi halmashauri ili wawe na wawakilishi wao ambao watawasilisha kero zao kwenye vikao vya maamuzi vya serikali na baraza la madiwani. Pia wameomba wapate uwakilishi bungeni kama yalivyo makundi mengine ya walemavu, vijana na wanawake.
Wamelalamikia kukosa Vitambulisho ambavyo vingeliwawezesha kupata huduma za haraka kwenye taasisi mbalimbali za serikali,ikiwemo dawa kwenye hospital za serikali, pia wamelalamikia lugha za kuwadharirisha zinazotolewa na baadhi ya wahudumu wa hospital za serikali na vituo vya afya.Wamelalamikia hatua ya Zahanati kutokutoa huduma siku za mwisho wa wiki hali ambayo inawasababisha kukosa huduma za matibabu.Aidha wamelalamikia TASAF kutoa fedha kwa ajili ya watu wasiokuwa na uwezo kwa upendeleo ambapo walengwa wamekuwa hawanufaiki na mpango huo wa TASAF.
|
No comments:
Post a Comment