Friday, October 14, 2016

TEMESA SHINYANGA YAZIDAI MILLIONI 163 HALMASHAURI, MASHIRIKA NA TAASISI ZA SERIKALI.

Mtendaji Mkuu wa TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu(kushoto) akisikiliza taarifa kuhusu kituo cha TEMESA Mkoa wa Shinyanga kutoka kwa Meneja wa TEMESA Shinyanga Mhandisi Riziki Lukali, alipotembelea kituoni hapo katika ziara yake katika vituo vya TEMESA Kanda ya Ziwa.
Mtendaji Mkuu TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu akikagua chumba cha kuhifadhia vipuri vya matengenezo ya magari TEMESA Mkoa wa Shinyanga, alipotembelea kituoni hapo katika ziara yake katika vituo vya TEMESA Kanda ya Ziwa.
Mtendaji Mkuu TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu (wa pili kulia) akitoa maelekezo kwa watendaji wa kituo cha Shinyanga alipotembelea kituoni hapo katika ziara yake katika vituo vya TEMESA Kanda ya Ziwa.
Mtendaji Mkuu TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu (menye shati la rangi ya bluu)akiangalia gari la TANESCO Shinyanga, linaloshikiliwa na TEMESA Shinyanga kwa sababu ya deni la Sh Millioni 96 kushoto ni Meneja wa TEMESA Shinyanga Mhandisi Riziki Lukali.Picha zote na Theresia Mwami TEMESA Shinyanga.

………………

Na Theresia Mwami TEMESA Shinyanga

Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Mkoa wa Shinyanga inazidai Halamashauri, Mashirika na Taasisi za Serikali mkoani humo jumla ya shillingi 163,269,269.82 kutokana na kupata huduma ya matengenezo ya magari.

Katika taarifa yake kwa Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Meneja wa TEMESA Shinyanga Mhandisi Riziki Lukali amesema madeni hayo ni ya mwaka wa fedha 2016/2017 na wamesha wasilisha madai yao kwa wahusika na wanasubiri kulipwa.

Mhandisi Riziki Lukali aliwataja wadaiwa hao kuwa ni TANROADS Shinyanga Sh 24,193,733.21, TANESCO Shinyanga Sh Milioni 96,267,987.63, DED Kishapu Sh 6,753,735.03, RAS Shinyanga Sh 2,742,097.36, KUWASA Kahama Sh 9,855,714, KASHUWASA Shinyanga Sh 1,992,430, TBA Shinyanga Sh 5,103,062.56, Mahakama Kuu Shinyanga Sh 5,470,628.91, Uhamiaji Shinyanga Sh 896,333.63, DAS Kishapu Sh 1,071,573.57, NSSF Shinyanga Sh3,798,184 pamoja na RMO Shinyanga shilingi 5,123, 789.92 milioni na jumla ya madeni hayo yote ni Sh 163,269,269.82.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu amefurahishwa na utaratibu wa TEMESA Shinyanga wa kuzuia magari ya taasisi, halmashauri na mashirika yanayodaiwa na kituo hadi hapo yatakapolipiwa gharama za matengenezo.

Na pia amemuagiza Meneja wa TEMESA Shinyanga kutoa taarifa kwake kama kuna Taasisi za Serikali ambazo hukiuka Sheria kwa kutopeleka magari yake kwenye karakana za TEMESA na kupeleka magari hayo kwenye karakana binafsi zilizomo mkoani humo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Dkt Mgwatu amesisitiza watumishi kuendelea kujituma kufanya kazi kwa weledi na kwa ubora zaidi ili karakana iweze kuvuta wateja wengi na kuongeza pato la kituo.

Aidha TEMESA Shinyanga kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 kituo kimepanga kukusanya jumla ya Sh 458,160,000 kutokana na madeni na huduma zinazoendelea kutolewa kituoni hapo.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu yupo katika ziara ya kutembelea vituo vya TEMESA vilivyopo Kanda ya Ziwa ili kubaini changamoto mbali mbali zilizomo na kuzitafutia ufumbuzi.

No comments: