Benny Mwaipaja, WFM, Seoul, Korea
TANZANIA, Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) na Korea ya Kusini zimetiliana saini makubaliano ya pamoja
kutekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya umeme gridi ya Kaskazini Magharibi
inayoanzia mkoani Mbeya, Nyakanazi hadi Kigoma, yenye msongo wa kV 400 mbapo
Serikali ya Korea imeahidi kutoa Dola za Marekani milioni 50 sawa na zaidi ya
shilingi Bilioni 100.18, kwa ajili ya kugharamia mradi huo.
Hali kadhalika, Tanzania na Benki
ya Exim ya Korea, zimesaini Mkataba wa
mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za marekani milioni 90.092 sawa na zaidi ya
shilingi Bilioni 194 za Tanzania, kwa ajili ya mradi wa Upanuzi wa Miundombinu
ya mfumo wa maji taka Jijini Dar es salaam.
Kwa upande wa Tanzania,
Makubaliano pamoja na Mkataba vimesainiwa na Mhe. Dkt. Philip Mpango (MB)
Waziri wa Fedha na Mipango kwa niaba ya Serikali, Oktoba 25, 2016 Jijini Seoul
nchini Korea Kusini huku upande wa AfDB, aliye saini ni Rais wa Benki hiyo
Adesina Akinwumi, na kwa upande wa Benki ya Exim, mkataba huo umesainiwa na
Mwenyekiti ambaye pia ni Rais wa Benki hiyo Lee Duk-Hoon.
Akizungumza mara baada ya kutia
saini makubaliano na mkataba huo, Dkt. Mpango amesema makubaliano na mkataba
vilivyosainiwa vina manufaa makubwa kwa wananchi wa Tanzania.
Pause ( Kwa TV) Waziri
Mpango-akizungumza kuhusu umeme
“Wananchi wa Upande ule waanze
kufurahia kwamba maendeleo yanakuja na hasa tunaposema maendeleo ya viwanda
ambavyo ni lazima vitumie umeme, na kwamba mradi huu unatarajia kupelekwa hadi
Mbeya” Amesisitiza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango, amesema kuwa mradi
huo una umuhimu mkubwa pia kwa kuwa serikali imedhamiria kuufungua ukanda wa
Magharibi mwa Tanzania, kwa upande wa viwanda vya aina mbalimbali.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi
Mtendaji (Uwekezaji) wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini Tanzania-TANESCO,
Decklan Mhaiki, amesema mradi wa umeme wa Nyakanazi hadi Kigoma utakuwa na
urefu wa kilometa 280 na utakapo kamilika utaondoa changamoto ya shirika hilo
kuzalisha umeme unatumika katika ukanda huo wa Magharibi hususan Kigoma, kwa
kutumia majenereta ambayo uendeshaji wake ni ghali na umeme wake si wa uhakika.
“Kuleta laini kama hii, kwanza
itapunguza gharama kubwa, na umeme wa ziada utakao zalishwa tunaweza kuuza nchi
jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, upande wa pili wa Ziwa Tanganyika,
lakini kikubwa ni kuwahakikishia wananchi wa mkoa wa Kigoma kuwa na umeme wa
uhakika” ameongeza Bw. Mhaiki.
Akizungumzia mkataba wa ujenzi wa
miundombinu ya maji taka Jijini Dar es salaam, Dkt. Philip Mpango, amebainisha
kuwa mradi huo unatarajia kuwa na tija kwakuwa utatatua changamoto ya majitaka
kutuama mitaani hasa wakati wa mvua na kusababisha magonjwa ya mlipuko kikiwemo
kipindupindu.
Akifafanua kuhusu mradi huo,
Mchumi ambaye pia ni Afisa anayeshughulika
na utafutaji wa Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Melckzedek
Mbise, amesema kuwa mradi wa maji wa Ruvu unatarajia kuongeza wingi wa maji Jijini Dar
es salaam, utakaosababisha uzalishaji wa maji taka pia kuongezeka, hivyo mradi
huo wa kuondoa maji taka umekuja wakati muafaka.
“Mradi huu umekuja wakati muhimu na
mkopo una masharti nafuu sana” Amesisitiza Bw. Mbise.
Naye Afisa Mkuu wa utafutaji rasilimali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Sabra Issa Machano, amesema kuwa kati ya nchi 54 za Kiafrika zinazohudhuria mkutano wa Tano wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na Afrika, Mjini Seoul Korea, ni nchi nne tu zilizopewa mkopo na ufadhili ambazo ni Kenya, Uganda na Ethiopia, huku Tanzania ikipewa kiasi kikubwa zaidi cha fedha jambo linaloonesha kuwa Tanzania inakubalika Kimataifa.
No comments:
Post a Comment