Saturday, October 22, 2016

Prof. Ole Gabriel ahimiza vijana kufanya kazi kuchangia uchumi wa taifa.


Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akifungua kongamano la vijana kutoka shule na vyuo mbalimbali nchini Oktoba 18, 2016 jijini Dar es salaam wakati wa wiki ya maadhimisho ya Umoja wa Mataifa unaofikisha miaka 71 tangu kuasisiwa kwake. Maadhimisho ya hayo yanaongozwa na kaulimbiu kwa upande wa Tanzania inayosema “Jukumu la Vijana wa Tanzania katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii”.

Mwakilishi wa Shirika Umoja wa Mataifa nchini linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) Annamaria Kiaga akimkaribisha Mgeni Rasmi ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel kufungua kongamano la vijana kutoka shule na vyuo mbalimbali nchini Oktoba 18, 2016 jijini Dar es salaam

Baadhi ya washiriki wa kongamano la vijana kutoka shule na vyuo mbalimbali nchini wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel Oktoba 18, 2016 jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa kongamano la vijana lililoandaliwa na Shirika Umoja wa Mataifa linalishughulikia Maendeleo (UNDP).

Baadhi ya washiriki wa kongamano la vijana kutoka shule na vyuo mbalimbali nchini wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel Oktoba 18, 2016 jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi wa kongamano la vijana lililoandaliwa na Shirika Umoja wa Mataifa linalishughulikia Maendeleo (UNDP).

…………………………………………………………………..

Na Eleuteri Mangi, WHUSM

Mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) yanashiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijamii kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 71 ya umoja huo kinachofikia Oktoba 24 mwaka huu baada ya kuasisiwa kwake mwaka 1945.

Tanzania ambayo ni mwanachama hai wa UN imeungana na umoja huo kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kuunganisha nguvu za vijana na kuwajenga kimaadili, kiuchumi ili waweze kujitambua na kujua mustakabali wao katika kujenga uchumi wa nchi.

Kwa kuwa vijana ni nguzo kuu ya kujenga taifa lolote duniani, Tanzania kwa kukushirikiana Umoja wa Mataifa imeona umuhimu wa kuwashirikisha vijana kupitia kongamano la vijana kutoka shule za sekondari na vyuo vikuu nchini lililofanyika Oktoba 18 mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) uliopo jijini Dar es salaam.

Lengo la kongamano hilo ni kuwashirikisha vijana kujadili namna watakavyoshiriki katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na kutafuta namna bora ya kutatua changamoto zinazowakabili vijana nchini.

Vijana hao wamepata fursa ya kukumbushana, kuelimishana na kubadilishana mawazo juu ya namna bora inayowawezesha kutoa mchango wao katika masuala ya kiuchumi na maendeleo ya kijamii nchini.

Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Viana ya mwaka 2007, ujana ni kundi mtambuka ambalo linajumuisha vijana kuanzia miaka 15 hadi 35 ndio maana wanaitwa ni nguvu kazi ya taifa kwa kuwa wengi wao kuanzia miaka 18, umri wa mtu mwenye nguvu na uwezo mzuri wa kufikiri na kuchangia katika maendeleo ya taifa kiuchumi na kijamii.

Akifungua kongamano hilo, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel amewaasa vijana kuwa watakumbukwa kwa mchango wao watakaotoa kwa jamii na si kwa nafasi zao kwa kuchangia uchumi na maendeleo ya nchi, hivyo ni wajibu watambue umuhimu wao kwa taifa.

“Ikiwa kijana huna mchango katika jamii, huna thamani yeyote, ni vema kujijengea uwezo wa kukumbukwa kwa vitu ulivyofanya kwa taifa” alisema Prof. Ole Gabriel.

Akinukuu maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Prof. Ole Gabriel aliwaasa vijana kwa kusisitiza “Baba wa Taifa aliwahi kusema, ni vema tujiulize, tumelifanyia nini taifa na si taifa limenifania nini”

Kaulimbiu iliyoongoza kongamano hilo inawataka vijana watambue nafasi yao katika kujenga uchumu wa nchi “Jukumu la Vijana wa Tanzania katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii”.

Kwa kuthamini nafasi ya kijana katika taifa, Katibu Mkuu Profesa Ole Gabriel amewahimiza vijana nchini kuwa na utamaduni wa kufanya kazi ili kuchangia uchumi wa taifa na maendeleo ya jamii.

Profesa Ole Gabriel amewahimiza vijana kutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa kwa kushiriki kufanya kazi zitakazowaletea maendeleo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) neno “haki za binadamu” limetajwa mara saba katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa ambo ni ndio mwanzilishi na unafanya kazi ya kukuza na kulinda haki za binadamu kwa kuzingatia kuwa huo ndio ufunguo huru wa Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha Serikali zinawawajibika kwa haki za binadamu.

Kwa miaka 15 iliyopita, Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yanaelezwa kufanikiwa katika masuala mengi ambayo yalikuwa yakiathiri maisha ya watoto, vijana na familia zao.

Mafanikio hayo yameonekana katika kupunguza vifo vya mtoto, kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa kiume na wa kike katika shule za awali, msingi na sekondari pamoja na vyuo vikuu, kupunguza umaskini, upatikanaji wa maji salama na chakula bora.

Pamoja na mafanikio hayo, Umoja wa Mataifa na wadau mbalimbali duniani umekuja na malengo mapya ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yaliyowekwa Septemba ya mwaka 2015 na viongozi wa dunia ili kuleta mageuzi ya masuala mbalimbali kwa mustakabali wa maendeleo ya binadamu hadi ifikapo mwaka 2030.

Katika kupanga malengo hayo, zaidi ya mamilioni ya watu walishiriki katika kuandaa ajenda mpya ya maendeleo endelevu.

Washiriki hao ni pamoja na Serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi, wasomi, mfumo wa Umoja wa Mataifa na watu binafsi. 

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) Annamaria Kiaga anasema kuwa kila Oktoba 24, UN husherehekea kuanzishwa kwake ambapo huandamana na shughuli mbalimbali kwa nchi wanachama pamoja na kukaa na wadau ili kupata maoni yao yaweze kusaidia katika kuleta maendeleo.

Katika Malengo Endelevu 17 yaliyoainishwa na Umoja wa Mataifa, malengo matatu yanampa nafasi kijana kuweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Lengo la 3 la SDGs linalenga kuhakikisha vijana wanapata maisha yenye afya na kukuza ustawi wao kifamilia kwa kuzingatia mazingira ya asili kwa ajili ya ukuaji na ustawi ya wanafamilia wake wote hasa watoto, kwa kuwapa ulinzi na msaada ili waweze kupata mahitaji yao kikamilifu ndani jamii yao.

Mshiriki wa kongamano hilo, mwananfunzi Matilda Mashauri kutoka shule ya sekondari ya Gerezani jijini Dar es Salaam anaiomba Serikali iungane na jamii kuwaelimishe wazazi na walezi katika kusimamia ipasavyo haki na huduma kwa watoto ili vijana waweze kufikia malengo yao na taifa kwa ujumla.

Mawazo hayo ya Matilda yanaendana na lengo la nne (4) SDGs ambalo linalenga kuhakikisha umoja na usawa katika utoaji wa elimu bora pamoja na kukuza fursa sawa ya kujifunza kwa watoto wote ambapo inatarajiwa ifikapo 2030 wasichana na wavulana wote wapate elimu ya msingi bure, kwa usawa na ubora wenye kuleta ufanisi katika kujifunza.

Zaidi hayo, malengo ya maendeleo endelevu yanahakikisha wanafunzi wote wanapata maarifa na stadi zinazohitajika kukuza maendeleo endelevu, ikiwa ni pamoja na haki za binadamu, usawa wa kijinsia, kukuza utamaduni wa amani, kuthamini utamaduni na mchango wa utamaduni.

Ili kujipambanua na mataifa mengine Prof. Ole Gabriel anasema kuwa changamoto inayowakabili vijana wengi nchini Tanzania ni fikra ya namna ya kujiletea maendeleo kwa kutumia utamaduni chanya wa kufikiri kwa kutumia rasilimali zilizopo na anawatahadharisha juu ya uvamizi wa teknolojia ambayo isipotumika vizuri itabomoa vijana ambao ni tegemeo la taifa.

“Nchi yoyote duniani isiyokuwa na maadili imeparanganyika, tusipokuwa na utamaduni mzuri taifa letu halitakuwa salama” alisema Prof. Ole Gabriel.

Katika kuhakikisha utamaduni wa Mtanzania unadumishwa Prof. Ole Gabriel anasema kuwa ni vema teknolojia itumike vizuri ili kuwaletea vijana na taifa maendeleo endelevu ili kuendana na Sera ya Taifa ya Tanzania ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Naye Mjasiriamali kijana Abdul Faraji mzaliwa wa mkoani Tanga amemweleza Mgeni Rasmi Prof. Ole Gabriel kuwa licha ya yeye kuwa na makazi yake jijini Dar es salaam, ameamua kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana wa ukanda wa bahari waishio mkoani Tanga kwa kuanzisha kituo kijulikanancho kama Vijana House ili kurasimisha kazi zao za kiuchumi ziwe zenye tija kwa maendeleo yao.

Mawazo ya kijana Abdul Faraji yamekuwa ni njia ya kulelekea kutekeleza lengo la tano (5) la SDGs katika kufikia usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana kutambua asili, hadhi na haki sawa ya wanafamilia wote kwa msingi wa uhuru, haki na amani duniani ambapo taasisi yake itafanya kazi na vijana wote bila kujali jinsia zao.

Akizindua Malengo ya 17 ya Maendeleo Endelevu (SDGs) Septemba 29, mwaka 2015 jijini Dar es Salaam, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania ambaye pia ni Mwakilishi Mkazi wa UNDP Bw. Alvaro Rodriguez alisema kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya dunia, serikali zimekutana na kukubaliana kupeana malengo kwa ajili ya kila mtu.

“Malengo haya yatasaidia mataifa yote kushirikiana katika kuwezesha ustawi, kupunguza matumizi na kuilinda dunia dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi. Katika hilo watashughulikia viashiria vinavyohusu maendeleo endelevu; ukuaji wa uchumi, ustawi wa jamii na kulinda mazingira.” Amesistiza Bw. Alvaro.

Malengo hayo 17 ya SDGs ni pamoja na kuondoa umasikini, kumaliza tatizo la njaa duniani, afya njema na ustawi miongoni mwa jamii, utoaji elimu bora, kuwepo na usawa wa kijinsia, upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira pamoja na uhakika wa kuwa na nishati nafuu na salama.Mengine ni watu wapate kazi nzuri yenye kukuza uchumi, kukuza viwanda, kuwepo ubunifu katika sekta mbalimbali, na kuboresha miundombinu, kupunguza ukosefu wa usawa, kuendeleza miji na jamii, kuimarika uwajibikaji, utumiaji na uzalishaji, utunzaji wa hali ya hewa, utunzaji wa maisha ya viumbe hai chini maji na maisha juu ya ardhi, kuwepo amani na kuwa taasisi imara za kusimamia haki pamoja na uwepo wa ushirikiano kwenye malengo thabiti miongoni mwa mataifa.

No comments: