Tuesday, October 11, 2016

MAMLAKA YA USAFIRI BAHARINI YAKANUSHA TUHUMA ZA KUSAJILI MELI ZA KOREA KASKAZINI

 Mkurugenzi Mkuu wa  Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibari  (ZMA) Abdallah Hussein Kombo akizungumza na  waandishi wa Habari  kukanusha tuhuma za kusajili Meli za Korea ya Kaskazini kinyume na Azimio la Baraza  la Usalama la Umoja wa Mataifa.
 Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini  Abdallah Hussein Kombo wakati alipokutana nao Ofisini kwake Malindi .
 Mwandishi wa Idara ya  Habari  Maelezo  Zanzibar Ramadhan Ali akimuliza suala Mkurugenzi Mkuu  (ZMA) hayupo pichani.
Katibu Mkuu wa  Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji  Zanzibar Mustafa Aboud Jumbe  akitowa ufafanuzi  wa masuala yaliyoulizwa na Waandishi wa Habari katika Mkutano huo. (Picha na Miza Othman Habari Maelezo Zanzibar).


Na Ramadhan Ali/Maelezo Zanzibar          11.10.2016

Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA) imekanusha tuhuma zinazotolewa kuwa imesajili meli za Korea Kaskazini kinyume na Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa mwezi Machi mwaka huu za kuzikatalia usajili Kampuni za meli za nchi hiyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mkurgenzi Mkuu wa ZMA Abdalla Hussein Kombo amesema tuhuma hizo zilizotolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uchambuzi wa Taasisi ya NK News kupitia Jarida la NK Pro la Mjini Seoul, Korea Kusini sio za kweli.

Amesema ZMA baada ya kupata taarifa ya Azimio hilo iliunda Kamati ya wataalamu kulifanyia uchambuzi na kutoa mapendekezo kwa Mamlaka juu ya hatua za kuchukuliwa."Azimio hilo limetaja majina ya meli 31 za Korea Kaskazini ambazo nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa, ikiwemo Tanzania, inazitaka kuzifutia usajili au kutozisajili," alisema Mkurugenzi Mkuu ZMA.

Aliongeza kuwa ZMA ilifanya uhakiki wa meli zote zilizosajiliwa na Mamlaka hiyo na orodha ya meli zilizoainishwa kupitia Azimio hilo na kubaini kuwa meli moja yenye jina la First Cleam ilikuwa imesajiliwa kabla ya vikwazo vya usajili wa meli za Korea Kaskazini lakini ikaamua kuifutia usajili.

Amesema kuanzia wakati huo, Mamlaka haijawahi kusajili meli yeyote ambayo ilikuwemo katika orodha iliyotolewa na Umoja wa Mataifa na imekuwa ikichukua tahadhari kubwa katika usajili wa meli.

Mkurugenzi Mkuu wa ZMA alisisitiza kuwa ili kuhakikisha hawatoi usajili kwa meli zenye uhusiano na Korea Kaskazini imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Taasisi za Kimataifa ikiwemo IMO.

Hata hivyo amekiri kuwa Kampuni ya Filtex ambayo ilikuwa wakala wa ZMA nchini Dubai na kuvunja naye mkataba bado inaendelea kusajili meli kwa jina la Zanzibar  kinyume na sheria.

Amesema  tayari wameshawasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kuifuatilia Kampuni hiyo na kuifungulia mashtaka kwenye mahakama za Kimataifa.Amesema katika kukabiliana na uharamia unaofanywa na Kampuni ya Filtex, miezi michache ijayo, ZMA itafungua Ofisi yake nchi Dubai kwa ajili ya usajili wake wa meli wa Kimataifa.



Kufuatia majaribio ya Korea Kaskazini kutengeneza silaha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kikao chake cha 7638 kilichofanyika tarehe 2 Machi, 2016 ilipitisha Azimio la kuiongezea vikwazo Korea Kaskazini ikiwemo kuzinyima usajili meli zote za nchi hiyo ama zenye uhusiano nazo.

No comments: