’Wito watolewa kwa kila mwananchi kuwajibika kwa malengo ya Dunia’
OKTOBA 24 kila mwaka Umoja wa Mataifa hufanya maadhimisho ya kuzaliwa kwake.
Mwaka
huu mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kwa kushirikiana na
serikali, wadau wa maendeleo na vijana wataadhimisha miaka 71 ya uwapo
wa Umoja wa Mataifa kwa staili ya aina yake.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa katika mkutano wa waandishi wa habari na
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikishirikiana
na Umoja wa Mataifa , maadhimisho hayo mwaka huu yamelenga kuelezea kwa
undani shughuli zinazofanywa kwa pamoja kati ya pande hizo mbili ili
kuwezesha maendeleo endelevu.
Katika
mkutano huo wa pamoja, waandishi wa habari walielezwa kwa ufupi Mpango
Mpya wa Maendeleo Chini ya Ufadhili wa Umoja wa Mataifa ( UNDAP ll -2016
hadi 2021) kwa serikali ya Tanzania; na mpango wa maendeleo wa miaka
mitano wa Tanzania ambamo malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) kama
yalivyosanifiwa na kukubalika na jumuiya ya kimataifa, yameshirikishwa.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt.
Augustine Mahiga akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani)
katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es
Salaam. Mhe. Balozi Dkt. Mahiga, amezungumzia umuhimu wa maadhimisho wa
Siku ya Umoja wa Mataifa na faida za Jukwaa la umoja huo kwa maendeleo
ya Taifa. Maadhimisho hayo yatafikia kilele tarehe 24 Oktoba,
2016.(Picha zote na Reginald Kisaka wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki).
Katika
mkutano huo na waandishi wa habari pia kulikuwepo na majadiliano ya
mafanikio ya shughuli za Umoja wa Mataifa hadi sasa duniani na pia
nchini Tanzania .Pia mazungumzo hayo yalijikita katika malengo ya
Maendeleo Endelevu (SDGs) na umuhimu wa malengo hayo kumilikishwa kwa
wananchi na wajibu wao katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na utekelezaji
wenye mafanikio.
Pia
ilielezwa katika mkutano huo kwamba maadhimisho ya miaka 71 ya Umoja wa
Mataifa, Siku ya Umoja wa Mataifa, yatafanyika katika viwanja vya
Karimjee jijini Dar es Salaam Oktoba 24.Maadhimisho hayo ambayo mwaka
huu yamebeba ujumbe wa :“Uwezeshaji wa vijana Tanzania kufikia malengo
ya dunia” yanafanyika huku kukiwa na malengo mapya ya dunia ya maendeleo
endelevu.Malengo hayo ya SDGs yamelenga kuondoa umaskini kwa kuwa na
maendeleo endelevu.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt.
Augustine Mahiga katika mkutano na waandishi wa habari.
Aidha
ujumbe huo unaenda sanjari na mpango wa maendeleo wa awamu ya pili wa
Umoja wa Mataifa kwa Tanzania (UNDAP II) ambao unaendeleza ule wa awali
wa kuanzia 2011-16 ukiwa umejikita katika masuala ambayo ni muhimu
kwenye kukabili umaskini kwa kuwa na maendeleo endelevu.
Maadhimisho
ya mwaka huu yalitanguliwa na kongamano la vijana wapatao 200, ambao
walijadili masuala yanayogusa fursa za uchumi na maendeleo ya jamii na
mchango ambao unaoweza kutolewa na vijana kufanikisha utekelezaji wa
malengo hayo.
Maadhimisho
hayo yatafikia kilele chake nchini kwa tukio litakalofanyika Visiwani
Unguja Oktoba 26 mwaka huu.Imeelezwa kuwa maadhimisho ya mwaka huu
yanaonesha uwapo wa ushirikiano mkubwa na wenye tija kati ya Tanzania,
wananchi wake na Umoja wa Mataifa.
Kaimu
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika
la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bi.Chansa Kapaya
akizungumza na waandishi wa habari.
Aidha
maadhimisho hayo yanaonesha ni kwa namna gani pande zote zipo tayari
kutekeleza mipango ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania
yenye lengo la kusaidia utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.
Akizungumza
umuhimu wa ushirikiano huo katika kutekeleza mpango wa maendeleo wa
miaka mitano, ukiwa ni mpango wa wananchi wenyewe, Waziri wa Mambo ya
nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw Augustine Mahiga, alielezea
Tanzania kuunga mkono Umoja wa Mataifa ukifanyakazi kama taasisi moja na
kuwataka watengeneza sera kuhakikisha kwamba wananchi wote wananufaika
na ushirikiano huu wa Tanzania na Umoja wa Mataifa.
Waziri
Mahiga alisisitiza wakati Tanzania inajikita katika kutekeleza mpango
wake mpya wa taifa wa maendeleo, kuna haja ya kuhakikisha kwamba
wananchi wanaelewa na kumiliki mpango huo ambao umejumuisha malengo ya
maendeleo endelevu.
Mkurugenzi
Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kushoto)
akifuatilia mkutano. Kulia ni Kaimu Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja
wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP) nchini Bi.Chansa Kapaya.
Alisema:
“Tanzania imeshirikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) katika
sera za taifa na pia katika mipango ya maendeleo inayotekelezwa katika
maeneo ya msingi yanayohitaji uangalizi kufanikisha maendeleo
endelevu”.
Hata
hivyo aliongeza kusema kwamba: “ Hiyo inajulikana wazi kwamba serikali
pekee haiwezi kufanikisha utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu
bila msaada wa sekta binafsi na wadau wetu wa maendeleo, na hivyo iko
haja ya kushirikishana. Tunaitaka sekta binafsi na wadau wetu wa
maendeleo kujiunga nasi katika juhudi hizi kwa kutuwezesha kifedha ili
tuweze kutekeleza mipango yetu ya maendeleo. Tunachohitaji sisi
tunaofanyakazi katika ushirikiano wa kimataifa kuhakikisha kwamba
hatutamwacha yeyote nyuma katika harakati zetu za kuleta maendeleo”.
Naye
Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Bw. Alvaro Rodriguez
akizungumzia maadhimisho ya miaka 71 ya Umoja wa Mataifa na uhusiano
wake alisema: “Tanzania na Umoja wa Mataifa zimekuwa na ushirikiano wa
maendeleo kwa miongo mingi. Wakati Tanzania sasa inabadilika, msaada
unaotolewa na Umoja wa Mataifa unatakiwa kukidhi haja mpya, hasa taifa
linapoelekea katika uchumi wa kati”.
Pia
katika hotuba yake aliongeza kwamba: “Malengo ya maendeleo endelevu ni
muhimu katika ushirikiano wetu kwani unaweka umuhimu wa shughuli za
Umoja wa Mataifa nchini Tanzania za kusaidia kupatikana kwa mafanikio
katika nyanja za uchumi, ustawi wa jamii na utunzaji wa mazingira.”
No comments:
Post a Comment