Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaharu Yoshida (kulia) na Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Flora Rajabu Yongolo, wakisaini
hati za makubaliano ya msaada wa shilingi za Tanzania milioni 170
uliotolewa na Serikali ya Japan kusaidia Mradi wa upanuzi wa Kituo cha
Afya cha Murangi kilichopo wilayani Musoma, mkoani Mara.
Wanaoshuhudia (waliosimama) ni Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge
wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) na Kaimu Mkuu
wa Mkoa wa Mara ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose
Nyamubi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Flora Rajab Yongolo,
akitoa neno la shukrani kwa Serikali ya Japan kwa msaada uliotolewa.
Waziri wa Nishati na Madini ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Vijijini,
Profesa Sospeter Muhongo (aliyeshika kipaza sauti), akimshukuru na
kumuaga Balozi wa Japani nchini Tanzania, mara baada ya kuhitimisha
hafla ya kutia saini makubaliano ya msaada utakaosaidia upanuzi wa kituo
cha afya cha Murangi kilichopo wilayani Musoma, Mkoa wa Mara.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya
Butiama, Annarose Nyamubi, akizungumza katika hafla hiyo.
Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaharu Yoshida, akiwa ameongozana
na mwenyeji wake, Waziri wa Nishati na Madini na Mbunge wa Musoma
Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo; akisalimiana na viongozi mbalimbali
ngazi ya Mkoa, Wilaya, Vyama vya siasa na viongozi wa Kituo cha Afya
cha Murangi, alipowasili katika Kituo hicho hivi karibuni kwa ajili ya hafla ya
kutia saini makubaliano ya msaada utakaosaidia upanuzi wa Kituo husika
kilichopo wilayani Musoma, Mkoa wa Mara.
Na Veronica Simba - Musoma
Serikali ya Japan kupitia kwa Balozi wake nchini, Masaharu Yoshida,
imetia saini makubaliano ya shilingi za Tanzania milioni 170 kwa ajili ya
kusaidia mradi wa upanuzi wa Kituo cha Afya cha Murangi kilichopo
wilayani Musoma, Mkoa wa Mara.
Makubaliano hayo yaliyosainiwa baina ya Balozi huyo na Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Flora Rajabu Yongolo, kituoni hapo
hivi karibuni, yameshuhudiwa na Waziri wa Nishati na Madini ambaye pia
ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo.
Wengine walioshiriki hafla hiyo na kushuhudia tukio hilo la utiaji saini, ni
viongozi mbalimbali ngazi ya Mkoa, Wilaya na Halmashauri pamoja na
wananchi wa Jimbo husika.
Akizungumza mara baada ya kutia saini, Balozi Yoshida alisema kuwa,
Serikali ya Japan imeamua kutoa msaada huo kutokana na uhaba wa vifaa
tiba na zana katika Kituo hicho cha Afya, ambavyo havitoshelezi ongezeko
la idadi na mahitaji ya wagonjwa.
Akifafanua zaidi, Balozi Yoshida alisema kuwa, msaada huo utatumika
kujenga nyumba za wafanyakazi, choo cha wagonjwa, shimo la kutupia
kondo la nyuma na kurekebisha tanuru la kuchomea taka za hospitalini
kwa lengo la kuwapatia wagonjwa huduma safi na salama pamoja na
kuboresha mandhari ya kazi kwa wauguzi.
Aidha, Balozi Yoshida alisema kuwa, Serikali ya Japan inaihakikishia
Serikali ya Tanzania kuwa, itaendelea kutoa michango yake katika
kuisaidia Tanzania kupitia mpango huo.
Kwa upande wake, Prof Muhongo amewataka wananchi wa Jimbo hilo
kuendelea kuchapa kazi kwa bidii zaidi na ubunifu na kuwahakikishia kuwa
maendeleo zaidi yanakuja jimboni humo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Flora Rajabu
Yongolo, alimshukuru Balozi wa Japan kwa msaada ambao Serikali yake
imeutoa na kumhakikishia kuwa rasilimali zote za mradi husika zitatunzwa
na kutumika ipasavyo.
Kituo cha cha Murangi kilijengwa mwaka 1972. Ni Kituo kikubwa cha Afya
wilayani Musoma na hupokea wagonjwa wengi wa rufaa kutoka Zahanati
Nane (8) wilayani humo.
Mkataba uliosainiwa ni kupitia mfuko wa mpango wa Miradi midogomidogo
kwa ajili ya usalama wa binadamu yaani Grant Assistance for Grassroots
Human Security Projects (GGHSP).
No comments:
Post a Comment