Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza jambo alipofika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera ili kujadiliana kuhusiana na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani humo. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu Salim Kijuu.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akielezea jambo wakati wa kikao na wataalamu wanaofanya utafiti wa tetemeko Mkoani Kagera (hawapo pichani).
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Profesa Abdulkarim Mruma ambaye ni kiongozi wa timu ya wataalamu wanaofanya utafiti wa tetemeko mkoani Kagera akionesha kitovu cha tetemeko hilo katika kijiji cha Kigazi, Kata ya Minziro kilomita 88 kutoka Bukoba mjini kupitia barabara ya Bukoba-Kyaka-Minziro.
Baadhi ya nyumba katika kijiji cha Kampanji kilichopo Mpakani mwa Tanzania na Uganda ambazo zilibomoka kutokana na tetemeko la ardhi.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akikagua eneo lililokumbwa na Tetemeko na kusababisha mpasuko kwenye ardhi katika kijiji cha Kigazi, Kata ya Minziro ndani ya Kitongoji cha Bilongo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kulia) akizungumza wakati wa ziara ya kukagua shughuli za utafiti wa tetemeko zinazofanywa na timu wataalamu kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Mtendaji Mkuu wa GST, Profesa Abdulkarim Mruma ambaye ni kiongozi wa timu ya wataalamu hao.
Wataalam kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanaofanya utafiti wa tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 10 Septemba, mwaka huu mkoani Kagera, wametakiwa kuhakikisha kuwa wanafanya utafiti wa kina ili kubaini namna ambavyo miamba ya maeneo husika ilivyo na vilevile kuandaa ramani mpya ya miamba katika maeneo yatakayotafitiwa.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipofanya ziara mkoani humo kwa lengo la kukagua shughuli za utafiti wa tetemeko zinazoendelea maeneo mbalimbali mkoani humo.
Alisema kuwa, utafiti huo utachukua muda mrefu kwani hautafanyika mkoani Kagera pekee bali utafanyika pia katika Mikoa ya Geita, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Dodoma na baadaye nchi nzima.
Katika ziara hiyo, Waziri Muhongo aliwaagiza wataalam hao kuhakikisha wanatoa mafunzo ya awali kwa umma hususan kwenye maeneo yaliyoathiriwa zaidi na tetemeko ili waelewe nini wanapaswa kufanya endapo tetemeko litatokea.
Aliagiza elimu hiyo ianze kutolewa siku ya Jumamosi, tarehe 24/9/2016 Saa 4 Asubuhi, huku wakiandaa ratiba ya mafunzo hayo kwa maeneo mengine na kuandaa vipeperushi vyenye maelezo ya kutosha kuhusu Tetemeko la Ardhi kwa ajili ya kuwasambazia wananchi.
Aidha, Profesa Muhongo aliwaagiza wataalam hao, kuepuka kutoa kauli zinazokinzana ili kuepusha kuwachanganya na kuwaletea hofu wananchi waliokumbwa na kadhia hiyo na kueleza kuwa Msemaji Mkuu wa wataalam hao wanaofanya utafiti husika ni Mtendaji Mkuu wa GST, ambaye yupo mkoani humo akishirikiana na wataalam kufanya utafiti.
Mbali na hilo, Profesa Muhongo aliagiza kuwa, ujengwe mnara maalum katika eneo ambalo tetemeko hilo lilianzia huko katika kijiji cha Kigazi, Kata ya Minziro, kilomita 88 kutoka Bukoba mjini ili iwe kumbukumbu ya baadaye.
"Eneo hili mliwekee alama, muandike siku na muda ambao tetemeko lilitokea," aliagiza Profesa Muhongo.
Katika ziara hiyo, Waziri Muhongo pia amekagua miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambayo iliathiriwa na tetemeko la ardhi, ili kubaini hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa lengo la kuiboresha na baadaye leo hii atakutana na Kamati ya Maafa ili kuweka mikakati ya kusimamia Shughuli za maafa na namna bora ya kuwaelimisha wananchi jinsi ya kujihami kabla na baada ya Tetemeko.
No comments:
Post a Comment