Friday, September 9, 2016

WAZIRI MKUU KUFUNGA AIRTEL RISING STARS.


 Mchezaji wa Kinondoni Hassan Kipera (nyekundu) akimiliki mpira mbele ya mchezaji wa Mbeya Ernest Kamange wakati wa fainali za taifa za mashindano ya Airtel Rising Stars yanaoendelea kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Kinondoni ilishinda 2-1.
 Mchezaji wa Kinondoni SalumYohana  (nyekundu) akijiandaa kuifungia timu yake bao la pili  wakati wa fainali za taifa za mashindano ya Airtel Rising Stars yanaoendelea kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Kinondoni ilishinda 2-1.
 Mchezaji wa Kinondoni Salum Yohana  (nyekundu) akimpiga chenga mlinda mlango wa Mbeya ma kuifungia timu yake bao la pili  wakati wa fainali za taifa za mashindano ya Airtel Rising Stars yanaoendelea kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Kinondoni ilishinda 2-1. 
 Beki wa Kinondoni Haji Mohammed Haji  (nyekundu) akipinga mpira kichwa kuondoa hatari golini kwake huku akisongwa na washambuliaji wa Mbeya wakati wa fainali za taifa za Airtel Rising Stars yanaoendelea kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Kinondoni ilishinda 2-1.
Mshambuliaji wa timu ya Mbeya (nyeupe) akichuana vikali na beki wa timu Kinondoni wakati wa fainali za taifa za Airtel Rising Stars yanaoendelea kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Kinondoni ilishinda 2-1.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa atakuwa mngeni rasmi wakati wa kufunga fainali za taifa za michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars Jumapili 11 Septemba mwaka huu kwenye uwanja wa Karume Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) Salum Madadi amesema hiyo ni heshima kubwa kwa vijana, viongozi na wadhamini wa mashindano hayo. “Ujio wa Waziri Mkuu utaamusha ari ya wachezaji”, alisema Madadi. 

Fainali za mashindano hayo zilifunguliwa Jumanne 6 Septemba na Mkuu wa wilaya ya Ilala Sophia Mjema kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda. Jumla ya timu 12 zinashiriki mashindano hayo huku sita zikiwa za wavulana na sita wasichana. Mikoa inayoshiriki niTemeke, Ilala, Kinondoni, Mbeya, Morogoro na Mwanza kwa wavulana na Temeke, Ilala, Kinondoni, Arusha, Lindi na Zanzibar kwa wasichana.

Katika hatua nyingine, timu za mkoa wakisoka wa Kinondoni za wavulana na wasichana zimekuwa za kwanza kujikatia tiketi ya kucheza nusu fainali ya Airtel Rising Stars baada ya mechi zilizochezwa asubuhi, Alhamsi Septemba 8 kwenye uwanja wa Karume. Timu ya wasichana Kinondoni waliwafunga Lindi 10-0 huku wavulana wakishinda 2-1 dhidi ya Mbeya.

Wasichana Kinondoni walianza vyema mashindano hayo baada ya kuwafunga Arusha 4-0, kwa hivyo waliingia uwanjani wakiwa wakitaka sare ya aina yeyote kutinga hatua ya nusu fainali. Iliwachukua dakika tano kupata goli la kwanza likifungwa na Aisha Juma. Mchezaji nyota wa mechi hiyo Prisca Bahela aliifungia timu yake mabao matano peke yake kati ya dakika ya 16, 20, 25 kipindi cha kwanza na 30 na 31 kwenye kipindi cha pili. 

Magoli mengine yalifungwa na Isabela John dakika ya 7 na 19 kipindi cha kwanza huku Mwantum Ramadhani na Veronica Mapunda wakifunga dakika ya 23 na 29 kipindi cha pili.

Kwenye mechi kati ya wavulana Kinondoni na Mbeya, timu hizo ziliingia uwanjani kila moja ikiitaji ushindi ili kusonga mbele. Hali hiyo ilisababisha mechi kuwa kali na ya kuvutia huku timu zote zikishambuliana kwa zamu. 

Timu ya Kinondoni ndio iliyokuwa ya kwanza kupata goli kwenye dakika ya 14, goli likifungwa na Shaban Maguli  aliyewashinda nguvu mabeki wa Mbeya na kuruka juu kufunga akiunganisha krosi nzuri kutoka kwa mshambualiaji mwenzake Marco Muhiru. Baada ya kupata bao, kasi ya mchezo iliongezeka huku Mbeya wakitafuta goli la kuzawazisha na Kinondoni wakitaka kuongeza bao kujihakikishia ushindi. Mpaka kipindi kwa kwanza kinamalizika Kinondoni 1 Mbeya 0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ileile lakini walikuwa ni Kinondoni waliowafurahisha mashabiki wake kwenye dakika ya 57 baada ya kiungo Salum Yohana kupokea pasi nzuri kutoka kwa Hassan Kipera na kufanya kazi nzuri ya kuwachambua  mabeki watatu pamoja na mlinda mlango na kuiandikia timu yake bao ya pili. 

Baada ya bao hilo, Mbeya waliongeza kasi iliyosababisha kupata bao dakika ya 77 likifungwa na Pius Crinton akiunganisha mpira wa kona uliopingwa na Ernest Kamange. Matokeo yalibakia hivyo mpaka mwisho wa mechi na kufanya Kinondoni wavulana na wasichana kusonga mbele. 
Robo fainali za michuano hiyo zitachezwa Jumamosi Septemba 10 huku zikihitimishwa na kilele cha fainali Jumapili 11 Septemba.

No comments: