Tuesday, September 27, 2016

Vijana Wachangia Damu na Kutoa Seti ya Televisheni Leo.

 
 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja, Aminieli Aligaesha (kushoto) kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akipokea msaada wa seti ya televisheni yenye thamani ya Sh 2.4 milioni kwa ajili ya jengo la wazazi (Maternity II). Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Kibosho (UVIKI), Severine Mushi akikabidhi msaada huo LEO na anayefuatia ni Mwenyekiti wa UVIKI, Marcel Mushi (wa tatu kushoto).
 Mlezi wa umoja huo, Dk Methew Kalanga ambaye ni Mkuu wa Idara ya Kinamama Muhimbili akiwapongeza vijana hao kwa kutoa msaada wa seti ya televisheni na kuchagia damu leo. Kulia ni Kaimu Meneja wa Jengo la Wazazi namba mbili, Sister Stella Gerald.
 Vijana wa umoja hao wakimsikiliza Dk Kalanga baada ya hospitali hiyo kupokea msaada wa seti ya televisheni leo.
 Vijana hao wakipewa maelezo na Ofisa Ustawi, Ndekusara Makishe kabla ya kuchangia damu leo.
 Vijana hao wakichangia damu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo.
Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)

Mercy Kaanaeli, MNH.
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imepokea jumla uniti  19 za damu kutoka kikundi cha Umoja wa Vijana wa Kibosho (UVIKI). Kikundi hicho chenye wanachama 40 kimeka katika hospitali hiyo leo na kutoa msaada wa seti ya televisheni na kuchangia damu.

Msaada huo umetolewa leo katika hospitali hiyo una thamani ya Sh 2.4 milioni na seti hiyo itafungwa katika Jengo la wazazi namba mbili. Seti hiyo inahusisha Runinga moja ya nchi 50, Dishi na King’amuzi cha AZAM pamoja na deki.

Akishukuru baada ya kupokea seti hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja, Aminieli Aligaesha amesema seti hiyo ya televisheni itatumika kutoa elimu ya afya kwa kinamama wajawazito.

Kaimu Meneja wa Jengo la Wazazi namba mbili, Stella Gerald amesema seti hiyo ni msaada mkubwa na kwamba  itasaidia kuelimisha kina mama wakati wakisubiri kupata huduma.

“Huwa tunatoa elimu ya maandalizi kwa kinamama ikiwamo vidokezo vya hatari, uandaaji wa chakula lishe pamoja na mambo yanayopaswa kufanywa, hivyo badala ya muuguzi kuongea tutatumia runinga kutoa elimu hiyo,”amesema Stella.

Naye Mkuu wa Idara ya Kinamama, Dk Matthew Kallanga amesema mchango wa damu uliotolewa na kikundi hicho utasaidia kina mama kuwa na uzazi salama.

“Damu iliyochangiwa na kikundi hiki, itasaidia kina mama kuwa na uzazi salama kwani mama mjamzito mmoja huweza kutumia chupa 5 hadi 6,” amesema.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja, Aminieli Aligaesha ametoa wito kwa jamii kuiga mfano wa kikundi cha UVIKI na kutoa damu kwa wingi ili kuokoa maisha ya wagonjwa.

Mwenyekiti wa Kikundi cha UVIKI, Marcel Mushi amesema kuwa watatoa elimu katika jamii wanayoishi ili wanajamii wengi zaidi wajitokeze kuchangia damu.

No comments: