Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akionesha aina tofauti za
maboksi yatakayotumika kufungashia chaki nyeupe na za rangi ambazo zinatarajiwa
kuanza kuzalishwa na Vijana wa Wilaya ya Maswa, Mkoani humo wakati
alipohitimisha Mafunzo ya Teknolojia ya Utengenezaji wa Chaki kwa vijana hao,
(katikati) Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Seif Shekalaghe (kulia) Mwenyekiti wa
CCM wilaya ya Maswa, Mhe. Peter Bunyongoli.
Mkuu wa Wilaya
ya Maswa, Mhe. Seif Shekalaghe akizungumza na vijana na wadau wengine wakati wa
kuhitimisha mafunzo Teknolojia ya
utengenezaji chaki yaliyotolewa na Shirika la Viwanda Vidogo vidogo SIDO kwa
Vijana wajasiriamali wa Wilaya ya Maswa, katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya
Wilaya hiyo.
Meneja
wa Shirika la Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) Mkoa wa Shinyanga, Athanas Moshi
(aliyesimama) akizungumza na vijana
na wadau wengine wakati wa kuhitimisha mafunzo ya Teknolojia ya
utengenezaji chaki yaliyotolewa na Shirika hilo kwa Vijana wajasiriamali wa Wilaya ya Maswa.
Baadhi ya Vijana
wajasiriamali wa Wilaya ya Maswa wakiangalia sampuli za maboksi
yaliyopendekezwa kutumika kufungashia chaki pindi uzalishaji utakapoanza wakati
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) akihitimisha mafunzo
ya Teknolojia ya utengenezaji chaki yaliyotolewa na SIDO kwa vijana hao,
wilayani humo
Vijana
wajasiriamali wa Wilaya ya Maswa wakiweka chaki walizotengeneza wakati wa
mafunzo ya Teknolojia ya utengenezaji chaki yaliyotolewa na SIDO katika maboksi
mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (hayupo pichani) kabla ya Mkuu huyo wa mkoa kuhitimisha mafunzo hayo.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Serikali Mkoani Simiyu imetangaza azma yake ya kuanza kutengeneza Chaki ambazo zitauzwa
katika Wilaya za Mkoa huo na nchi nzima kabla ya Oktoba 14 mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony
John Mtaka wakati alipohitimisha mafunzo ya Teknolojia ya utengenezaji wa Chaki
kwa vikundi vya vijana Wajasiriamali wilayani Maswa, yaliyotolewa na Shirika la
Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) Mkoa wa Shinyanga.
Mtaka amesema shule zote za Msingi na Sekondari za
Serikali Mkoani humo zinatumia jumla ya
katoni 1200 za chaki ambazo zinagharimu shilingi 25,000,000 kwa kila mwezi,
hivyo kama Vijana wa Wilaya ya Maswa wakizalisha Chaki na kusambaza katika mkoa
mzima watajipatia kipato na kuondokana na umaskini.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema katika kutekeleza azma ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa na
Tanzania ya Viwanda, Mkoa huo umejipanga kuimarisha uwekezaji katika
viwanda vidogo vidogo ambavyo vitazalisha mahitaji ya kila siku ya wananchi,
hivyo wamedhamiria kuwa na uzalishaji wa bidhaa moja kwa kila wilaya ( one
district one product), ambapo Wilaya ya
Maswa itakuwa ikizalisha chaki.
“ Wilaya ya Maswa imepokea shilingi 38,000,000 Meatu 31,000,000 kwa ajili ya vijana kutoka
Wizara yenye dhamana na Vijana, sasa hivi tumepeleka maombi ya wilaya zilizobaki. Tumedhamiria
kuutambulisha Mkoa kwa kuzalisha bidhaa zetu wenyewe, tumeanza na Chaki wilaya
ya Maswa, Wilaya ya Meatu wao watazalisha maziwa, tutaendelea kutengeza utambulisho(brand) wa wilaya
nyingine kwa kuzalisha bidhaa zinazoendana na malighafi zilizopo” alisema
Mtaka.
Akizungumza katika hitimisho la Mafunzo hayo kwa
Vijana, Meneja wa Shirika la Viwanda vidogo (SIDO) Mkoa wa Shinyanga, Athanas
Moshi ametoa wito kwa vikundi vya vijana kuwa na mipango itakayowasaidia kutangaza
bidhaa zao na kupata soko la bidhaa hizo ndani na nje ya Mkoa ili kujiongezea
kipato.
“Mtakapoanza kuzalisha chaki, kulingana na tathmini
iliyofanyika kama mtauza kwa Mkoa wa Simiyu tu mtakuwa na uwezo wa kutengeneza
faida ya shilingi 8,000,000 kila mwezi, hiyo si fedha ndogo mkiwa na mipango
thabiti mkazalisha chaki bora mtaweza kuuza chaki zenu nchi nzima na hata nje
ya nchi” alisema Moshi.
Naye mmoja wa vijana waliopata mafunzo ya
utengenezaji wa chaki, Kelvin Steven ametoa wito kwa Wananchi wa Simiyu na Watanzania kwa ujumla, kuunga mkono juhudi za Vijana Wajasiriamali na
kuthamini bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili kuinua uchumi wa Vijana hao na
Taifa kwa jumla.
Aidha, Bi. Specioza Fundikira ambaye pia amepata
mafunzo hayo amesema matarajio ya Vijana waliopata mafunzo ni kuwa uzalishaji
wa chaki utakapoanza kutakuwa na soko la uhakika kwa Shule zote za Msingi na
Sekondari za Serikali mkoani humo na mikoa ya jirani, vijana watapata ajira na
kuachana na shughuli zisizo halali kama wizi na ulevi.
Kwa Mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Seif
Shekalaghe vijana kutoka vikundi 8 vya Wajasiriamali ambao wameunda kikundi
kimoja cha ‘Maswa Youth Enteprises’ wamepatiwa mafunzo ya Teknolojia ya
utengenezaji wa chaki na Shirika la Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) Mkoa wa
Shinyanga kuanzia tarehe 29/08/2016 hadi tarehe 03/09/2016.
No comments:
Post a Comment