Thursday, September 1, 2016

SERIKALI YA RAIS DK JOHN POMBE MAGUFULI IENDELEE NA MIKAKATI YAKE YA KUJENGA NCHI KWA SASA-UVCCM

Pichani kulia ni Kaimu katibu mkuu wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM) Taifa ,Shaka Hamdu Shaka akiongea na waandishi wa habari mjini Dodoma,shoto ni kaimu katibu wa hamasa,sera,utafiti na mawasiliano wa UVCCM Taifa Chief Silvester Yeredi

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema  hakuna mazungumzo, majadiliano wala mijadala inayostahili kufanyika kati ya Serikali ya CCM na Chadema na kuiomba Serikali ya Rais Dk John Magufuli iendelee na mikakati yake ya kisera ili kuimarisha maendeleo ya kiuchumi.

Pia umoja huo  umeeleza kuwa  dunia inajua, ulimwengu unaaelewa na Chadema wanafahamu kuwa Tanzania hakuna mgogoro wa kisasa zaidi ya serikali kupigania mabadiliko, nchi kuwa ya viwanda na kutokomeza  maadui umasikini, ujinga na maradhi.

Msimamo huo umetolewa jana na Kaimu Katibu Mluu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ukumbi wa White House Makao Makuu ya CCM Mkoani hapa.

Shaka alisema UVCCM ilijua, ilielewa na kutambua mapema  Chadema na viongozi wake walikuwa wakifanya maigizo katika  siasa, hawakuwa na ubavu wala jeuri ya kuandamana kwa madai aliyoyaita ni ya  kipuuzi ambayo hayana msingi kwa mustakabali wa nchi na maendeleo yake.

Alisema viongozi na wafuasi wa Chadema  walishindwa kuandamana Septemba Mosi, hawataweza na wala hawatajaribu kufanya hivyo  Oktoba Mosi kwa sababu wanachotaka kukifanya ni utoto wa kisiasa  baada ya kushindwa kubuni mkakati wa kukiendesha chama chao ili kiaminike na kukubalika.

"Tunazo habari  wabunge wa Chadema wamechachamaa na kumbana Mbowe  kwa  hoja wakitaka kurudi bungeni ili kushiriki vikao kwa kuwa hawaeleweki kwa wapiga kura wao majimboni lakini pia wanakabaliwa na 'waya mkali',   hawaoni kwa nini wasishiriki vikao vya Bunge huku baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho wakiwa na utajiri na wengine  wafanyabiashara,"alisema Shaka.

"Cha ajabu hata na wale wazee tuliokuwa tukiwaheshimu bila soni wanashiriki kuudanganya ulimwengu wakitoa madai ati kuna mgogoro wa kisiasa  unaohitaji suluhu, yafanyike mazungumzo na majadiliano,"alisema Shaka.

Alisema UVCCM imeshangazwa na madai ya Chadema na kusema  kwamba chama hicho na viongozi wake wamekuwa wakikutana na viongozi wa madhehebu ya dini na mashirika ya kiraia, kisheria  yaliyowataka ati wasiteshe maandamano kwa muda hadi Oktoba Mosi mwaka huu.

"Tumekuwa tukijiuliza bila kupata majawabu ya kina pale Mbowe na Chadema wanaposema wameshauriwa na viongozi wa madhhebu ya dini na taasisi  zingine. Je hapo awali pia walishirikiana na viongozi hao  kupanga na kuitisha maandamano yenye lengo la kumdhihaki Rais na kumwita dikteta?" alihoji Kiongozi huyo wa Vijana.

Hata hivyo, alisema si jambo linaloingia akilini na mtu alazimike kuyamini maneno ya Chadema kama kweli viongozi wa dini na taasisi zilizotajwa, walihusika na kushiriki mpango wa uitishji maandamano ya vurugu na sasa  wahusike tena kuwakataza Chadema wasifanye  maandamano.

"UVCCM,  wananchi wema, wapenda amani na utulivu, viongozi wa mashirika ya kiraia na madhehebu ya dini, hatuwezi kusimama  hadharani kuitbitishia dunia kama Tanzania kuna mgogoro wa kisiasa  unaohitaji yafanyike mazungumzo, majadiliano hadi kufikia mapatano," alieleza Shaka.

Alisema ulimwengu mzima  unafahamu,  mashirika na jumuia za kimataifa nazo zinaelewa  kwamba katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, wananchi walitekeleza wajibu wao wa kikatiba  na  kupitia demokrasia ya uchaguzi  walimchagua kwa kura Rais Dk. Magufuli kuwa Rais wao na matokeo ya uchaguzi huo yalitangazwa na chombo chenye dhamana ya kisheria na kikatiba ambacho ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Shaka, alisisitiza kuwa wananchi wote, mashrika ya Kimataifa na ulimwengu unaelewa  Dk. Magufuli baada ya kuchaguliwa, serikali yake bila kupoteza wakati imekuwa ikihimiza kwa nguvu zote mpango wa uwajibikaji,  utendaji wenye  ufanisi, nidhamu, huku serikali yake ikipiga vita ufisadi, ubadhirifu wa mali za umma  pia   ikikusanya kodi na kuongeza mapato ya taifa.

"Chadema na UKUTA wao  wanachotaka ni  siasa za mitaani na maandamano haramu. Wanataka kukithiri kwa malumbano na mabishano yasiyo na maana badala ya wakulima, wafanyakazi, wavuvi na wafugaji wafanye kazi kwa bidii, kujituma ili wazalishe mali na kujienga uchumi na kimaendeleo alisema,"alisema Shaka .

Shaka alieleza kuwa haipendezi na  haiwapi hadhi au heshima mbele ya jamii watu  wanaojiita viongozi wa kisiasa wa Chadema kuwa na uhodari wa kutunga uongo, wakauamini, kuueneza na kuutetea kwa misuli ya unafiki na upotoshaji.

"UVCCM tunawaasa viongozi wa Chadema waache mara moja  siasa za utoto na tabia ya kuwatia hofu wananchi, wasiwafanye waishi kwa wasiwasi kwa siasa zao uchwara ambazo zimekosa afya  na wala haiwapi heko au heshima mbele ya dunia,"alisema Shaka.

No comments: