Tuesday, September 13, 2016

SERIKALI PAMOJA NA TAASISI ZA KIRAIA WAKUTANA MOROGORO KUTENGENEZA MFUMO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI NCHINI

Dr. Stephen Nindi Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi Tanzania akizungumza jambo juu ya Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa pamoja kuhakikisha maeneo yanapimwa na kuweka mpango mzuri wa Matumizi Bora ya Ardhi.
Aliyekuwa muwezeshaji katika Mkutano huo Profesa Aldo Lupala Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Ardhi ambaye ni Mkuu wa Kitivo cha Usanifu Majengo akitoa mwongozo wakati wa mkutano huo
 Wadau wa mkutano huo wakiendelea kufuatiliamkutano huo
Mratibu wa Mradi wa Ardhi yetu kutoka CARE International Tanzania Mary Ndaro akifafanua jambo wakati wa mkutano huo wa kikosi kazi
Mwakilishi kutoka Wizara ya Kilimo akielezea mikakati mbalimbali waliyonayo kuhusu mpango wa matumizi bora ya ardhi
Bw. Amos Mfuga kutoka Tume ya Taifa Mipango na Matumizi ya Ardhi akichangia jambo ikiwa ni pamoja na Tume kuweka vipaumbele kama kuangalia na kumaliza migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini 
 Wadau wa mkutano huo wa kikosi kazi kutoka Sehemu  mbalimbali wakiendelea na mkutano huo
Bw. Mdubi kutoka CARE International Tanzania akichangia jambo wakati wa Mkutano huo wa kikosi kazi
Naomi Shadrack kutoka Shirika la Kimataifa la OXFAM Tanzania akielezea namna shirika hilo likifanya kazi hapa Nchini na jinsi wanavyoshiriki katika mpango huo wa matumizi bora ya Ardhi
Bw. Jamboi kutoka Ujamaa Community akielezea ushiriki wao katika mpango wa matumizi bora ya ardhi
Bw.Emanuel Msofe kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii akichangia jambo juu ya ushiriki wao katika kikosi kazi hicho.
John Lugaso mmoja wa viongozi kutoka Chama cha wafugaji Tanzania , akieleza malengo ya chama hicho ikiwa ni pamoja na mipango ya baadae ya uanzishaji wa viwanda mbalimbali kwa ajili ya bidhaa zinazotokana na mifugo.
Mkutano ukiendelea
Picha zote na Fredy Njeje/Blogs za Mikoa

Katika kupanga matumizi bora ya ardhi nchini Tanzania ikiwa na lengo la jamii kutumia rasilimali hiyo vizuri kwa matumizi ya kawaida, Serikali imesema kuwa hadi sasa imefikia takribani vijiji 1645 na Wilaya 40 nchi nzima. Kutokana na ufinyu wa bajeti na kasi ndogo ya upimaji bado kuna vijiji 11,393 ambavyo havijafikiwa.

Akizungumza Mkoani Morogoro ,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Ardhi,Dkt Stephen Nindi wakati wa Mkutano wa  Kikosi kazi cha kuanda mpango kazi wa upangaji,utekelezaji na usimamizi wa maendeleo ya Ardhi nchini.
Pia Mkutano huo ulijadili kuhusu migogoro ya ardhi inayoendelea nchini na mipango ya matumizi ya ardhi kama inaweza kusaidia kupunguza migogoro hiyo,uliowakutanisha  wadau mbalimbali kutoka Serikalini ,taasisi na Mashirika mbalimbali yanayosimamia masuala ya ardhi.

Alisema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanashirikiana kwa pamoja kuhakikisha maeneo yanapimwa na kuweka mpango mzuri wa matumizi ya ardhi kwa matumizi yaliyokusudiwa katika kujadiliana ni namna gani wataona njia zinazofaa kutumika kukamilisha zoezi hilo la upimaji kwa vijiji vingine ikiwemo kuwepo kwa teknolojia mpya ya upimaji na kuwepo kwa bajeti ya kutosha.

Aliongeza kuwa lengo la  kupima,kumilikisha na Kupanga kila kipande cha ardhi ni pamoja na kuhakikisha ardhi inakuwa na matumizi mazuri katika nchi.

 Dkt.Nindi alisema tayari serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wametoa elimu katika timu za wilaya 100 kuwawezesha kujua  kupima,kupanga,kumilikisha ,kutekeleza na kusimamia mipango ya matumizi ya ardhi .

Kwa upande wake Mratibu wa Programu ya Mradi ya Ardhi yetu kutoka Shirika la Kimataifa la CARE nchini Tanzania ,Mary Ndaro alisema mpaka sasa ni miaka mingi tangu nchi ipate uhuru kasi ya upimaji wa maeneo imekua ndogo .

Alisema kama nchi inajiandaa kuwa na wawekezaji wengi zaidi inatakiwa kuhakikisha inakuwa na mipango bora ya  matumizi ya ardhi ambayo baadae haitaweza kuleta mgogoro wowote kati ya wanakijiji na muwekezaji.Aliongeza kuwa kwa sasa kati ya vijiji 12,545 nchi nzima ni vijiji 1645 ndiyo tayari vina mipango ya matumizi ya ardhi mpaka sasa. 

Vijiji vingi bado havina mipango kutokana na ufinyu wa bajeti na kuwepo kwa kasi ndogo ya upangaji.Ndaro alisema lengo la mkutano huo wa wadau ni kuona ni namna gani  vijiji   vilivyobaki kati ya vijiji 12,545  vinapangiwa matumizi ya ardhi, kunakuwa na ushirikiano wa karibu wa wadau na namna vipi wanashirikiana kutatua migogoro ya ardhi ambayo inazidi kuongezeka.

“Pamoja na kuwepo kwa kasi ndogo ya upangaji matumizi  ya ardhi, bado kuna changamoto ya kutoheshimu mipango ya matumizi ya ardhi iliyokwishaandaliwa ambapo  utakuta kijiji tayari kimepangwa lakini kinakuja kukatwa katikati na kuwa vijiji viwili au zaidi,”alisema

Alisema serikali inapaswa kuweka mipango ya matumizi ya ardhi ipasavyo ili kuweza kudhibiti hali ya migogoro ya ardhi kati ya watumiaji mbalimbali, mfano baina ya wawekezaji na wanavijiji kwa kupanga matumizi ya ardhi.“Serikali inapoita wawekezaji nchini inapaswa pia kuhakikisha mpango ya matumizi bora ya ardhi inayoeleweka kwa lengo la manufaa ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,”alisema

No comments: