Monday, September 26, 2016

RAIS DK.SHEIN ATEMBELEA MRADI UJENZI WA NYUMBA ZA KISASA FUMBA.


 Rais wa Zanzinbar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Azam Group Bw.Said Salim Bakhresa alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za kisasa huko  Fumba wilaya ya Magharibi,Mkoa wa Mjini Magharibi leo alipofanya ziara maalum kuangalia ujenzi wa nyumba hizo zinazojengwa na Kampuni ya Azam Group,(kulia ) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibu Nd,Ayoub Mohamed Mahmoud.
 Rais wa Zanzinbar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (wa pili kushoto) akifuatana na Mwenyekiti wa Kampuni ya Azam Group Bw.Said Salim Bakhresa (kushoto) pamoja na Viongozi mbali mbali wa Serikali wakati alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za kisasa huko  Fumba wilaya ya Magharibi,Mkoa wa Mjini Magharibi leo alipofanya ziara maalum kuangalia ujenzi wa nyumba hizo zinazojengwa na Kampuni ya Azam Group,(wa tatu kushoto) Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) Salum Nassor Khamis,akifuatiwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Khalid Salum Mohamed.
 Rais wa Zanzinbar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akipanda ngazi ya moja ya nyumba zinazojengwa na Kampuni ya Ujenzi ya  Azam Groupakifuatana na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo   Bw.Said Salim Bakhresa  wakati alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za kisasa huko  Fumba wilaya ya Magharibi,Mkoa wa Mjini Magharibi leo alipofanya ziara maalum kuangalia ujenzi wa nyumba hizo.
 Rais wa Zanzinbar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (wa pili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mtaalam wa mashine za kutengenezea lami katika Kampuni ya Ujenzi ya  Azam Group N.P.Singh (wa pili kulia) wakati  alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za kisasa huko  Fumba wilaya ya Magharibi,Mkoa wa Mjini Magharibi leo alipofanya ziara maalum,(katikati) Mwenyekiti wa Kampuni ya Azam Group Bw.Said Salim Bakhresa na (kushoto)Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) Salum Nassor Khamis.
 Rais wa Zanzinbar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Azam Group Bw.Said Salim Bakhresa(kulia) wakati alipotembelea Mtambo wa  kutengenezea lami katika Kampuni ya Ujenzi ya  Azam Group leo wakati  alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za kisasa huko  Fumba wilaya ya Magharibi,Mkoa wa Mjini Magharibi (wa pili kulia) Mtaam wa Mtambo N.P.Singh. Picha na Ikulu.

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imedhamiria kwa makusudi kuitilia mkazo na kuiimarisha sekta ya uwekezaji ambayo matunda yake yatawasaidia wananchi wote wa Zanzibar. 
Dk. Shein aliyasema hayo leo alipofanya mahojiano na waaandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali mara baada ya kumaliza ziara yake ya kuitembelea miradi ya Kampuni ya Bakhresa ikiwemo ujenzi wa nyumba huko Fumba pamoja na ujenzi wa hoteli ya kisasa huko Mtoni mjini Zanzibar. 
Dk. Shein alisema kuwa mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba za kisasa huko Fumba utasaidia kwa kiasi kikubwa kutokana na Serikali kuweza kupata pato sambamba na wananchi wa Fumba na maeneo jirani kuweza kupata ajira. 
“Fumba ilikuwa imefumba lakini hivi sasa itafumbuka kwani kukamilika kwa mradi huu Fumba itakuwa ni sehemu ya pekee katika kukuza uchumi wetu pamoja na kuwasaidia wananchi wote kutokana na pato litakalopatikana katika maradi huo”,alisema Dk. Shein.

Alisema kuwa matarajio ya ujenzi huo ambao kwa maelezo ya uongozi wa Kampuni hiyo, eneo hilo litakuwa ni Dubai ya Zanzibar linatoa matumaini makubwa katika kuuimarisha uchumi wa Zanzibar, ambapo mradi huo utajulikana kwa jina la ‘Uptown Living’. 
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa nchi nyingi duniani ziliazia na miradi kama hiyo ambazo zilikuwa ni masikini kuliko Zanzibar lakini hivi sasa zimeweza kupiga hatua kubwa na kuwa nchi tajiri kutokana na kuwepo miradi kama hiyo na kueleza kuwa kinachofanywa na serikali katika suala zima la uwekezaji ni tija kwa wananchi wote, 
Kutokana na juhudi hizo Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kuheshimu na kufuata taratibu zote zilizowekwa na Serikali juu ya suala zima la matumizi ya ardhi.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisikitishwa na tabia ya baadhi ya wananchi kuvunja sheria na taratibu zilizowekwa juu ya umili wa ardhi huku wakitambua kuwa ardhi ni mali ya serikali hivyo kila mmoja ana jukumu la kuilinda na kuitunza ardhi iliopo. 
Kwa upande changamoto ya ajira kwa vijana wa Zanzibar hasa katika sekta ya utalii, Dk. Shein alieleza kuwa jambo muhimu ambalo litawapa vijana wa Zanzibar kuajiriwa kwa haraka katika sekta hiyo ni kuwa na elimu ya fani hiyo. 
Alisema kuwa suala la elimu ni muhimu sana na kutoa wito kwa vijana wa Zanzibar kujikita zaidi katika kujitafuatia elimu na ndio maana Serikali anayoiongoza imeweza kutilia mkazo suala hilo kwa kukiimarisha Chuo chake cha Huduma za Watalii kiliopo Maruhubi kwa kutoa mafunzo ya Cheti, Diploma huku kukiwa na mchakato wa kukiingiza kuwa ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). 
Dk. Shein alisisitiza kuwa iwapo vijana watakuwa na elimu ya kutosha suala la upendeleo halitochukua nafasi huku akitoa inzari umuhimu wa elimu kwa hi sasa kwa vijana hao hasa katika ushindani wa ajira katika soko la Afrika Mashariki. 
Mapema Dk. Shein alipata nafasi kutembelea mradi ya nyumba za kisasa zinazojengwa na Kampuni ya Bakhresa huko Fumba akiwa na mwenyeji wake Said Salim Bakhresa na kupata maelezo juu ya uendelezaji wa mradi huo utakaojenwga nyumba 600 ambapo awamu ya kwanza ni wa nyumba 92 za kisasa zinazoendelea kujengwa ambazo zitakuwa kwa ajili ya wananchi wenye kipato cha  juu na kipato cha kati. 
Mradi huo ambao mbali ya nyumba utakuwa na eneo maalum la bustani kwa ajili ya wananchi, bandari ambayo itawasafirisha wakaazi wa eneo hilo kutoka eneo hilo hadi Dar-es-Salaa kwa boti maalum zitakazokuwepo eneo hilo huku uongozi huo ukieleza hatua zitakazochukuliwa katika kuhakikisha suala ziama la ulinzi na usalama linaimarishwa. 
Pia, Dk. Shein alipata fursa ya kuangalia mtambo wa kisasa wa kupikia lami unaomilikiwa na Kampuni hiyo ya Bakhresa na baadae kukagua barabara itakayotoka eneo hilo hadi uwanja wa ndege. 
Ziara ya Dk. Shein ilimalizia huko Mtoni nje kidogo ya mji wa Zanzibar ambapo alijionea ujenzi wa hoteli hiyo itakayokuwa na sifa ya kimazingira ‘Eco Friend’ ambayo inajengwa kwa umiliki wa Kampuni hiyo ambayo inatarajiwa itakuwa ni ya pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki. 
Kwa mujibu wa maelezo ya Mkuu wa ujenzi wa mradi huo Salim Aziz, alisema kuwa hoteli hiyo itajitosheleza kwa huduma za maji na  umeme na kupunguza gharama katika matumizi hayo. 
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitembela eneo la bahari kuona shughuli za ufukiaji bahari ‘Land Reclamation’ lenye ukubwa wa heka 4 ambalo ni eneo la hoteli hiyo linalotarajiwa kuwa na maegesho ya meli ndogo na meli kubwa, huduma za bustani ya maji ambayo inajumuisha michezo ya kila aina itakayochezwa na wananchi pamoja na watalii.

Akimalizia Ziara yake, Dk. Shein alitembelea Gofu la Mtoni ‘Mtoni Palace Ruins’ na kupata maelezo ya kihistoria na hatimae alipata mapumziko yalioambatana na burudani mwanana kutoka kikundi cha Rahatul-zaman na kutumbuizwa kwa nyimbo zilizoibwa na Kitukuu cha Siti Bint Saada pamoja na mpiga Ganon  maarufu Zanzibar Nasor Mohamed hapo katika mkahawa wa hoteli hiyo. 
Katika ziara yake hiyo, Dk. Shein alifuatana na viongozi mbali mbali wa vyama na Serikali.




No comments: