Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa pamoja na watendaji wa Serikali na Wizara wakikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Kivuko cha Mv. Tanga kulia ni Mkuu wa wilaya ya Pamgani Mhe. Zainabu Abdallah Issa .
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa pamoja na watendaji wa Serikali na Wizara wakizindua Gati la Bandari ya Tanga.Ukamilifu wa Gati hiyo utasaidia Meli mbalimbali kuweza kutia nanga wilayani Pangani.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia) akisafiri na wakazi katika Kivuko cha Mv.Tanga kutoka Pangani kwenda Bweni mara baada ya uzinduzi. Wanne kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga.
Mbunge wa Jimbo la Pangani Mhe. Jumaa Awesu akizungumza na wananchi wa Jimbo hilo katika uzinduzi wa Kivuko cha Mv. Tanga na Gati ya bandari ya Pangani uliofanyika Mkoani Tanga.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Eng.Karim Mattaka akisoma taarifa ya ujenzi wa Gati ya bandari ya Pangani kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani) katika uzinduzi wa Kivuko cha Mv. Tanga na Gati hiyo uliofanyika Mkoani Tanga.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Ndg. Martin Shigela akielezea taarifa ya utekelezaji wa Miradi ya Miundombinu katika Mkoa wa Tanga kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani) katika uzinduzi wa Kivuko cha Mv. Tanga na Gati hiyo uliofanyika Mkoani Tanga.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa wananchi wa Pangani katika uzinduzi wa Kivuko cha Mv. Tanga na Gati hiyo uliofanyika Mkoani Tanga.
Wananchi wa Pangani wakishangilia ujio wa Kivuko kipya cha Mv. Tanga Wilayani hapo kinachotoa huduma ya usafirishaji kati ya Pangani na Bweni.
…………………………………………………………………
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amezindua kivuko kipya na cha kisasa cha Mv. Tanga kinachotoa huduma ya usafirishaji kati ya Pangani na Bweni na kuzindua Gati ya Bandari ya Pangani wilayani pangani mkoani Tanga.
Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri Mbarawa amesema kuwa ujio wa kivuko hicho utafungua fursa za kibiashara na kuchochea maendeleo ya kiuchumi wilayani hapo.
“Naamini ujio wa kivuko hiki utarahisisha huduma za kijamii na maendeleo ya kiuchumi wilayani hapa, hivyo naomba mkitunze vizuri kivuko hiki ili kiweze kudumu kwa muda mrefu”, amesema Prof.Mbarawa.50 242
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha huduma za kivuko zinakuwepo muda wote wilayani hapo, Serikali kupitia Wizara hiyo imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa boti ambayo itatumika kama mbadala wa usafiri wakati wa usiku katika maeneo hayo ambapo kivuko cha Mv.Tanga hakifanyi kazi.
Kuhusu ujenzi wa Gati ya bandari ya Pangani Waziri Mbarawa ameseama kuwa ujenzi wa gati hiyo utapelekea Meli kubwa kuweza kutia nanga na kurahisisha usafiri wa moja kwa moja kutoka Pangani kwenda visiwa vya Unguja na Pemba.
Amefafanua kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wataanzisha huduma ya boti za haraka kutoka Pangani kwenda Mkokotoni Zanzibar hivyo kufungua fursa za kibiashara na kitalii baina ya Tanga na Zanzibar.
Kwa upande wa huduma za mawasiliano ya simu wilayani hapo, Prof.Mbarawa amesema kuwa huduma hiyo itaanza mwezi Desemba mwaka huu kwa mkandarasi kufika na kuanza ujenzi wa miundombinu ya simu na hivyo kuondoa tatizo la mawasiliano wilayani hapo.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amehahidi kuanza ujenzi wa Barabara ya Tanga-Pangani-Saadani hadi Bagamoyo (KM 242) kwa kiwango cha lami ifikapo mwakani.
Amefafanua kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakuwa wa awamu ili kuweza kuharakisha kukamilika kwake ambapo awamu ya kwanza itahusisha kipande cha barabara ya Tanga- Pangani (KM 50) na kuongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utafungua fursa za kiuchumi kati ya Tanga na Pangani.
“Naahidi kujenga barabara hii ambayo ni kiungo kati ya Tanga na Pangani, naamini ukamilifu wake utalete maendeleo mkoani hapa”. Amesisitiza Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eng.Joseph Nyamhanga amezipongeza kampuni za Songoro Marine na Alpha Logistic kwa kumaliza kwa wakati ujenzi wa kivuko na Gati ya bandari hiyo.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Eng.Manase Ole-kujan amesema kuwa kivuko cha Mv.Tanga kimejengwa kwa sh.bilioni nne ambapo kina uwezo wa kubeba tani 50 abiria 100 na magari madogo 6 kwa wakati mmoja.
Ujenzi wa Kivuko cha Mv. Tanga ni moja ya utekelezaji wa ahadi ya Mhe.Rais Dkt.John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wilayani Pangani Mkoani Tanga.
No comments:
Post a Comment