Saturday, September 17, 2016

MWENGE WA UHURU WAWASILI MKOANI SINGIDA NA ISHARA YA UHURU WA TANGANYIKA

MWENGE wa Uhuru baada ya kuwasili mkoani Singida Mwenge huu ni ni kitu mfano wa kikombe chenye mpini mrefu na utambi ambacho aghalabu huwasha na kukimbizwa katika kusheherekea au kutukuza tukio fulani.
Askari wa Jeshi la Polisi wakiulinda Mwenge ishara ya kuwasili muda mfupi kabla ya kukabidhi kwa uongozi wa Mkoa wa Singida

Kushoto ni Katibu tawala wa Mkoa wa Singida Dkt Angelina M. Lutambi akimkabidhi Mwenge Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mhe Geofrey Mwambe tayari kwa ajili ya kumulika Miradi 18 katika Wilaya hiyo

Baadhi ya viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma walipowasili kukabidhi Mwenge katika Kijiji cha Lusilile Kata ya Kintinku Wilaya ya Manyoni
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akiwa ameushikia Mwenge ishara ya Makabidhiano mara baada ya kuwasili
Katibu tawala wa Mkoa wa Singida Dkt Angelina M. Lutambi akikabidhiwa Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bi Rehema S. Madenge
 Wananchi wakishuhudia kwa karibu zoezi la makabidhiano ya Mwenge
Wakuu wa Wilaya za mkoa wa Singida wakishuhudia zoezi la makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru
 Wengi wamefika kushuhudia Mwenge ukiwasili mkoani Singida
 Viongozi wa Mkoa wa Singida wakifanya mazoezi ya maandalizi ya kuupokea Mwenge
 Timiza wajibu wako kata Mnyoro wa Rushwa
Katibu tawala wa Mkoa wa Singida Dkt Angelina M. Lutambi akisoma salamu za shukrani mara baada ya kupokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma katika Kijiji cha Lusilile

Na Mathias Canal, Singida
KATIBU tawala wa Mkoa wa Singida Dkt Angelina M. Lutambi leo ameupokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bi Rehema S. Madenge ambao utakimbizwa Mkoani Singida kwa siku saba katika Halmashauri saba ambapo utaanzia Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.

Dkt Lutambi amekabidhiwa Mwenge huo pamoja na wakimbiza Mwenge Kitaifa katika eneo la Kijiji cha Lusilile Kata ya Kintinku Wilaya ya Manyoni ukiwa umewaka na kuahidi kuukabidhi kwa katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora pasina mashaka utakapomaliza muda wake Mkoani Singida.

Lutambi alisema kuwa mwenge wa Uhuru ukiwa Mkoani humo utalitia jumla ya miradi 61 inayohusu sekta ya ufugaji, Mazingira, Maji, Afya, Elimu, Barabara, Utawala Bora, Kilimo, Ushirika, Biashara, Ardhi na Programu za mapambano dhidi ya Dawa za kulevya, Malaria Rushwa na Ukimwi.

Alisema kuwa jumla ya Miradi 33 itazinduliwa, 13 itawekwa jiwe la msingi minne itawekwa jiwe la msingi na mingine mitano itatembelewa ambapo miradi yote hiyo itakayopitiwa itakuwa na thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 14.

Mbio za Mwenge wa uhuru kwa Mwaka 2016 zimebeba kauli mbiu ya "Vijana ni nguvu kazi ya Taifa, Washirikishwe na kuwezeshwa" ambapo hata hivyo kila Halamashauri nchini zimeelekezwa kutenga asilimia 5% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vijana na asilimia 5% nyingine kwa ajili ya kina mama.

Katika kumaliza mizizi wa Rushwa, Dawa za kulevya, ukimwi na Malaria Mwenge wa Uhuru umejikita zaidi katika kauli mbiu ya "Timiza wajibu wako kata Mnyororo wa Rushwa" kwenye mapambano dhidi ya Rushwa, Kauli mbiu ya "Tujenge jamii, Maisha na Utu wetu bila dawa za kulevya" kwenye Mapambano dhidi ya Dawa za kulevya, Kauli mbiu ya "Tanzania bila maambukizi mapya, Unyanyapaa na Vifo vitokanavyo na UKIMWI inawezekana" kwenye Mapambano dhidi ya Ukimwi na Mapambano dhidi ya Malaria, chini ya kauli mbiu ya " Wekeza katika maisha ya baadae, Tokomeza Malaria".

Kwa upande wake katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bi Rehema S. Madenge wakati akikabidhi Mwenge wa Uhuru Mkoani Singida alisema kuwa Mwenge wa Uhuru umekimbizwa katika Wilaya zote saba za Mkoa huo ambapo jumla ya Miradi 47 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 12.

Bi Madenge amewapongeza wananchi wote kwa ushirikiano na juhudi kubwa walizofanya katika kuianzisha, kuiendeleza na kuikamilisha Miradi yote.

Pia alisema kuwa katika Wilaya zote walizozuru wakimbiza Mwenge wamepata taarifa za utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Mwaka 2015 na kuelezea namna inavyoendelea kutekelezwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mhe Geofrey Mwambe wakati akikabidhiwa Mwenge wa uhuru na katibu Tawala wa Mkoa wa Singida amesema kuwa Mwenge huo unataraji Kutembelea Miradi 18 ambapo hii leo utatembelea miradi 7 na hapo kesho utatembelea Miradi 11.

Miongoni mwa Mirafi itakayofunguliwa ni pamoja na uzinduzi wa Programu ya Ufuatiliaji na kuteketeza mbu, Kufungua Mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu nane ya vyoo na ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa, Ufunguzi wa daraja la Makutupora, Kuzindua Klabu ya wapinga Rushwa, Kuzindua Mradi wa Ujenzi wa kituo cha Maarifa ya kupambana na UKIMWI, Kuzindua Mradi wa Vijana wa kufyatua matofali, na Kuzindua Klabu ya Kupambana na Dawa za Kulevya.

Kwa mujibu wa ratiba za mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu, unakimbizwa katika Halmashauri na Manispaa zipatazo 179 na kilele cha mbio hizo ni Octoba 14 mwaka huu katika Mkoa wa Simiyu.

Mwenge wa Uhuru unaashiria Nuru na Mwanga, Uliwashwa rasmi kwa mara ya awali juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro Disemba 9, 1961

No comments: