Wataalamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiwa wamewasili nchini India kwa ajili ya kujengewa uwezo wa kupandikiza figo kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo. Wataalamu hao watakuwapo India kwa muda miezi mitatu na watarejea nchini Desemba 10, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Tiba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Hedwiga Swai akizungumza baada ya wataalamu hao kwenda India kwa ajili ya kujengewa uwezo wa upasuaji na upandikizaji figo.
Mkuu wa Idara ya Urolojia katika hospitali hiyo, Dk Ryuba Nyamsogoro akizungumza na wataalamu wenzake kabla ya kuanza kwa safari ya kuelekea India.
Mkuu wa Idara ya Urolojia katika hospitali hiyo, Dk Ryuba Nyamsogoro akizungumza na wenzake kabla ya kuondoka nchini.
Baadhi ya wataalamu wakimsikiliza Mkuu wa Idara ya Urolojia katika hospitali hiyo, Dk Ryuba Nyamsogoro wakati akitoa maelezo kabla ya kuanza safari ya kuelekea India wiki iliyopita.
Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
Na John Stephen, MNH.
Dar es Salaam, Tanzania. Wataalamu 20 wa fani mbalimbali wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wameondoka nchini kwenda India kwa ajili ya kujengewa uwezo wa upandikizaji figo kwa watu wenye matatizo ya figo.
Wataalamu hao wameondoka wiki iliyopita na wakiwa huko watajengewa uwezo wa kufanya upasuaji na upandikizaji figo kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo.
Mkurugenzi wa Tiba, Dk. Hedwiga Swai amesema leo kwamba wataalamu mbalimbali wakiwamo madaktari bingwa wa upasuaji na upandikizaji figo, madaktari bingwa wa magonjwa ya figo, wataalamu wa maabara, madaktari wa usingizi na madaktari wa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.
Wengine ni wataalamu wa mionzi, wauguzi wa chumba cha upasuaji na chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu na wataalamu wengine ambao wanakwenda kujifunza.
“Suala la mgonjwa kupandikizwa figo ni mchakato na haliwezekani kufanywa na mtaalamu mmoja.Ni kazi inayowahusisha wataalamu wengi,” amesema Dk. Swai.
Pia, Dk. Swai amesema upandikizaji figo utapunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu na kuokoa fedha nyingi za serikali za kuwapeleka nje ya nchi.
Amesema kwamba wataalamu hao watakaa nje ya nchi kwa muda wa miezi mitatu na watarejea nchini Desemba 10, 2016.
“Shughuli za upasuaji na upandikizaji figo zitaanza Januari mwakani,” amesema Dk. Swai.
No comments:
Post a Comment