Friday, August 19, 2016

VIJIJI 63 ITILIMA KUPATA UMEME WA REA AWAMU III

Na Stella Kalinga, Simiyu

Zaidi ya Vijiji 63 vya wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu vinatarajia kupata umeme kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya III inayoanza mwishoni mwa Mwezi Septemba, 2016.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Merdard Kalemani alipozungumza na wananchi wa maeneo tofauti ya wilaya ya Itilima wakati wa Ziara yake ya kukagua miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya II Mkoani Simiyu.

Pamoja na kupeleka huduma ya umeme kwa wananchi kutoka katika vijiji hivyo 63 Dkt. Kalemani amesema Serikali imedhamiria kupeleka huduma ya umeme katika Taasisi za Serikali zikiwemo shule za Msingi na Sekondari Ofisi za Serikali, Vituo Vya Afya na Zahanati na katika maeneo ya miradi ya maji.

Dkt. Kalemani ameelekeza Serikali za vijiji kwa kushirikana na Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) kuainisha wananchi wanaohitaji huduma ya umeme ili mradi utakapoanza kutekelezwa waanze kupata huduma hiyo mara moja.

Wakati Serikali ikiweka mikakati ya kujenga Ofisi za TANESCO Wilaya, Naibu Waziri Nishati na Madini amemuagiza Meneja wa TANESCO Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Rehema Mashinji kuteua maafisa watatu kutoka katika Ofisi yake watakaowafuata wananchi vijijini badala ya wananchi kuifuata huduma maofisini.

Aidha, Dkt Kalemani amelitaka Shirika la Umeme TANESCO kuainisha wataalam wake wanaohusika na REA, kupeleka Orodha yao katika Ofisi za Vijiji na kutoa elimu juu ya gharama na taratibu za kuunganisha umeme ili wananchi wasidanganywe.

“Ili kudhibiti ulaghai wa kuongeza gharama ambazo hazipo kila mtaalam awe na muhuri na majina yote ya wataalam wa TANESCO yapelekwe katika Ofisi za Vijiji tuweze kuwatambua vishoka. Kuna watu wanaweza kuwaongezea wanachi gharama wakati gharama halisi ni shilingi 27,000/= kwa yule ambaye ameshasuka nyaya kwenye nyumba yake, na fomu anachukua bure.” Alisema Kalemani.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu Silanga amesema anaishukuru Serikali kwa kuwaweka katika mpango wa kupata umeme wananchi wa Wilaya ya Itilima na akawataka Wenyeviti wa Serikali za Vijiji kupita katika kaya zote na kusaidia kubaini kaya zisizona umeme katika maeneo yao.

Wakati huo huo Mhe. Dkt. Kalemani amekitambulisha kifaa cha kuweka umeme bila kusuka nyaya ndani ya nyumba kiitwacho UMETA kinachotumika kuunganisha umeme kwa gharama isiyozidi 36,000/=,ambapo amesema kifaa hicho kinaweza kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kusuka nyaya katika nyumba zao

Akizungumza mara baada ya hotuba ya Naibu Waziri, Bibi.Milembe Katani mkazi wa Kijiji cha Nanga Kata ya Chinamili amesema anaishukuru Serikali kwa kuweka mikakati ya kuwapelekea umeme kwa kuwa utasaidia vijana wao kujiajri katika saluni, kuchomelea vyuma, na kuwekeza katika Mashine za kukamua alizeti na kukoboa mpunga.

Naibu Waziri Dkt. Kalemani yuko Mkoani Simiyu kwa ajili ya ziara ya Siku tatu ambapo amekagua miradi mbalimbali ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) katika Wilaya za Busega, Bariadi na Itilima.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani akizungumza na wananchi wa kata ya Sawida wilayani Itilima (hawapo pichani) , wakati wa Ziara yake ya kukagua miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya II Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani (wa pili kushoto) na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji (wa nne kulia mbele) walipokutana katika ukaguzi wa Mradi wa Kisima kilichochimwa kwa ushirikiano wa Misri na Tanzania, wakati wa Ziara zao wilayani Itilima; Mhe.Kalemani alikuwa akikagua miundombinu ya umeme katika mradi na Mhe. Kamwelwe kukagua miradi ya Maji.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani (kushoto) na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwelwe (kulia) wakishauriana jambo walipokutana katika ukaguzi wa Mradi wa Kisima kilichochimbwa kwa ushirikiano wa Misri na Tanzania, wakati wa Ziara zao wilayani Itilima; Mhe.Kalemani alikuwa akikagua miundombinu ya umeme katika mradi huo na Mhe. Kamwelwe kukagua mradi huo wa maji, (katikati) Mbunge wa Jimbo la Itilima, Njalu Silanga.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Sawida wakionesha mabango yao wa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani(hayupo pichani) wakati wa Ziara yake ya kukagua miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya II Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani (kulia) akimkabidhi Milembe Katani, Mkazi wa Kijiji cha Nanga Wilayani Itilima kifaa cha UMETA , wakati wa Ziara yake ya kukagua miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya II Mkoani Simiyu.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Chinamili wilayani Itilima wakimshangilia Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani(hayupo pichani) wakati wa Ziara yake ya kukagua miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya II Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt Merdard Kalemani akizungumza na wananchi wa kata ya Chinamili wilayani Itilima(hawapo pichani) , wakati wa Ziara yake ya kukagua miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya II Mkoani Simiyu

No comments: