Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akifafanua jambo
katika eneo la Lwenge, Nyamikoma ambalo ni moja ya maeneo yaliyotengwa kwa
ajili ya kuhifadhi magwangala.
Na Greyson Mwase, Geita
Mgogoro uliodumu kwa muda mrefu katika mkoa wa Geita kuhusu upatikanaji wa
magwangala na eneo la kuhifadhi magwangala hayo, umepatiwa ufumbuzi baada ya
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kukutana na mkuu wa
mkoa wa Geita, uongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), watendaji wa
halmashauri ya mkoa huo na wawakilishi kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Profesa Muhongo alifanya ziara katika mkoa huo ikiwa ni utekelezaji wa agizo
lililotolewa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania John Magufuli lililotolewa
Julai 31 mwaka huu la wachimbaji wadogo kupatiwa magwangala pamoja na
maeneo ya kuhifadhi magwangala hayo ili kuchenjua na kupata dhahabu.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita. Kulia ni mkuu wa mkoa huo, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga.
Akizungumza katika kikao kilichokutanisha watendaji kutoka Mkoa wa Geita, Wizara
ya Nishati na Madini, Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na Baraza la Taifa la
Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Profesa Muhongo alisema maeneo ya
awali yaliyopatikana kwa ajilli ya kuhifadhi magwangala hayo ni pamoja na Lwenge-
Nyamikoma, Kasota B na Samina B yaliyopo mkoani Geita.
Aliagiza Ofisi ya Madini Mkoani Geita kutoa leseni za uchenjuaji madini mara moja
kwa vikundi vyote vya wachimbaji madini ili waanze kazi mara moja ya uchenjuaji
madini kwa kutumia magwangala hayo.
“Ninaagiza Ofisi ya Madini Mkoani Geita kutoa leseni za uchenjuaji madini kwa
vikundi vilivyoundwa kupitia halmashauri mara moja bila vikwanzo vyovyote ili
waanze na shughuli za uchenjuaji madini mara moja,’ alisema Profesa Muhongo.
Akizungumzia suala la usafirishaji wa magwangala katika maeneo hayo Profesa
Muhongo alisema ni jukumu la vikundi vilivyopewa magwangala hayo kusafirisha
kutoka kwenye mgodi hadi kwenye maeneo yaliyoainishwa.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga (mbele) akisoma taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kubaini maeneo kwa ajili ya kuhifadhia magwangala mbele ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Halmashauri ya Geita.
Aliongeza kuwa iwapo vikundi vitakosa uwezo wa kusafirisha magwangala hayo,
halmashauri inaweza kufanya mazungumzo na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM)
kwa ajili ya gharama ya kusafirisha magwangala hayo.
Aidha katika kikao hicho Waziri Muhongo alikubaliana na uongozi wa Mgodi wa
Dhahabu (GGM) kwa ajili ya kusafirisha tani 10 kwa kila eneo kwa kuanzia kama
njia ya kuonesha nia ya kuwasaidia wachimbaji wadogo.
Profesa Muhongo alisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa wachimbaji
wadogo wa madini wananufaika na sekta ya madini kupitia shughuli za uchenjuaji
madini na kuwataka kuomba ruzuku pindi zinapotangazwa.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga (hayupo pichani) Katikati ni Kamishna Msaidizi wa Madini-Uchimbaji Mdogo, Julius Sarota.
Awali akiwasilisha taarifa ya mkoa wa Geita kuhusu utekelezaji wa mpango wa
uainishaji wa maeneo ya kuhifadhia magwangala, mkuu wa mkoa huo Meja Jenerali
Mstaafu Ezekiel Kyunga alisema kuwa suala la magwangala limekuwa la muda
mrefu ambapo wananchi wa Geita wamekuwa wakihitaji magwangala hayo ili
wafanye shughuli za uchenjuaji kwa lengo la kujipatia kipato.
Kyunga alisema kuwa ili kutekeleza azma hiyo ya kuwapatia wananchi magwangala,
jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu
kwa kushirikisha viongozi wa serikali, taasisi za kimazingira pamoja na wadau
mbalimbali.
Alisema katika utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Joseph Pombe Magufuli alilolitoa Julai 31 mwaka huu la kuwapatia wananchi
magwangala tayari mkoa umefanya hatua za awali kwa kutafuta maeneo tisa
yatakayofaa kwa ajili ya uhifadhi wa magwangala.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisisitiza jambo katika kikao hicho.
Aliainisha maeneo yaliyopatikana ni pamoja na Magogo, Lwenge-Nyamikoma,
Kasota A, Kasota B, Bugulula A, Bugulula B, Manga- Saragulwa, Mgusu, Samina A
na Samina B.
Aliongeza kuwa maeneo yaliyopewa kipaumbele cha kwanza ni pamoja na Lwenge-
Nyamikoma, Samina A, Manga-Saragulwa, Kasota B na Mgusu.
Aliongeza maeneo yaliyopewa kipaumbele cha pili ni pamoja na Samina A, Samina
B (Mpomvu), Bugulula A na Bugulula B.
“Kipaumbele cha tatu ni Magogo, pamoja na mapendekezo hayo bado tuliona
maeneo mawili ya Manga- Saragulwa na Mgusu ambayo yanaweza kutumika kwa
kuanzia kwa kuzingatia suala la usalama, idadi ya askari waliopo kulingana na
changamoto ya uhalifu unaoweza kujitokeza na kufanya tathmini ya uendeshaji wa
shughuli hiyo,” alisisitiza Kyunga.
Akielezea matokeo ya uwepo wa shughuli za magwangala mkoani Geita Kyunga
alieleza kuwa ni pamoja na ongezeko la watu katika maeneo hayo na kuhitaji
uimarishwaji wa ulinzi.
Sehemu ya watendaji kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani).
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akizungumza na watendaji kutoka Mkoa wa Geita, Wizara ya Nishati na Madini, Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) (hawapo pichani) Kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Selestine Gesimba na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga
Sehemu ya watendaji kutoka Mkoa wa Geita, Wizara ya Nishati na Madini, Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani).
No comments:
Post a Comment