Thursday, August 25, 2016

RC SIMIYU ATOA UFAFANUZI SAHIHI WA TAARIFA KUHUSU WALIMU WAKUU KUVULIWA MADARAKA

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthon Mtaka akizungumza na Maafisa Elimu na Viongozi wa CWT wa Mkoa huo katika kikao maalum cha kutoa ufafanuzi wa agizo lililotolewwa na Serikali Mkoani humo la kufanya mabadiliko ya Walimu wakuu na Waratibu Elimu kata, ambalo liliripotiwa tofauti katika vyombo ya habari na mitandao ya kijamii. kuwa Serikali imetangaza kuwavua madaraka.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ametoa ufafanuzi wa agizo la kufanya mabadiliko ya Walimu wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata mkoani humo, ambalo Serikali ya Mkoa ililitoa tarehe 17 Agosti ,2016 katika kikao ambacho alipokea Vishikwambi (tablets) 637 kutoka EQUIP Tanzania (Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Nchini) kwa ajili ya Walimu wakuu na Waratibu wa Elimu Kata

Mkuu huyo wa Mkoa ametoa ufafanuzi huo kufuatia kuwepo kwa taarifa za upotoshaji wa agizo hilo kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii., kuwa Mkuu wa Mkoa ametangaza kuwavua madaraka Walimu wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata wote wa Mkoa huo; hali iliyopelekea baadhi ya Walimu wakuu na Waratibu kukosa ari ya kufanya kazi, kwa kigezo cha kusubiri kuvuliwa madaraka.
Baadhi ya Wajumbe wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (hayupo pichani) katika kikao maalum cha kutoa ufafanuzi wa agizo lililotolewa na Serikali Mkoani humo la kufanya mabadiliko ya Walimu wakuu na Waratibu Elimu kata, ambalo liliripotiwa tofauti katika vyombo ya habari na mitandao ya kijamii. kuwa Serikali imetangaza kuwavua madaraka, 

Mtaka amesema Mkoa ulipokea taarifa za takwimu za wanafunzi hewa, vyumba vya madarasa, idadi ya walimu na idadi ya madawati, baada ya kupokea taarifa hizo ulionekana utofauti mkubwa wa takwimu hizo ndipo Serikali mkoani humo, ikaahidi kupitia mapungufu ya udanganyifu wa takwimu hizo kwa kila shule na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha Walimu wakuu na Wakuu wa Shule waliodanganya idadi ya wanafunzi.

Aidha, Mtaka amesema Mkoa wa Simiyu umepata bahati ya kuwa na Mradi wa EQUIP Tanzania ambao umewawezesha waratibu kupata pikipiki na posho, walimu wakuu wamepewa vishikwambi kwaa jili ya utunzaji wa takwimu, hivyo Serikali inao wajibu wa kuangalia mahitaji ya Mkoa katika elimu ambapo alielekeza yafanyike mabadiliko ya Walimu wakuu Msingi, Sekondari na Waratibu wa mkoa mzima.
Katibu wa CWT Mkoa wa Simiyu, Said Mselema(kulia) akizungumza na Maafisa Elimu na Viongozi wa CWT wa Mkoa huo (hawapo pichani) katika kikao maalum cha kutoa ufafanuzi wa agizo lililotolewa na Serikali Mkoani humo la kufanya mabadiliko ya Walimu wakuu na Waratibu Elimu kata, ambalo liliripotiwa tofauti katika vyombo ya habari na mitandao ya kijamii, kuwa Serikali imetangaza kuwavua madaraka. 

“Nililisema mwanzo na leo nalirudia tutafanya mabadiliko makubwa kwa Wakuu wa Shule za Msingi, Sekondari na Waratibu Elimu kata kwa kujiridhisha na maendeleo ya shule zetu, idadi ya walimu waliopo,idadi ya wanafunzi, kiwango cha ufaulu wa wanafunzi na mazingira ya shule ; lakini tutatoa upendeleo kwa shule 10 bora katika kila wilaya kwa Mitihani ya Kitaifa ya Darasa la IV, VII Kidato cha II na IV , hiki ni kipimo kimojawapo cha walimu wa kuendelea nao. Nasisitiza hakuna mtu atakayeonewa wala kufedheheshwa”, alisema Mtaka.

Mtaka amesema azma ya Serikali ni kuibua vipaji vipya vya viongozi wa Elimu katika ngazi ya Wilaya ambapo alisema ameshaagiza Maafisa Elimu wa Wilaya kuwasilisha taarifa ya walimu waliojiendeleza katika ngazi shahada ya kwanza na shahada ya uzamili ili watakaokuwa na sifa waweze kuteuliwa katika nafasi za Walimu wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata ambao watafanyiwa upekuzi (vetting) na Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Baadhi ya Wajumbe wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (hayupo pichani) wa kikao maalum cha kutoa ufafanuzi wa agizo lililotolewwa na Serikali Mkoani humo la kufanya mabadiliko ya Walimu wakuu na Waratibu Elimu kata, ambalo liliripotiwa tofauti katika vyombo ya habari na mitandao ya kijamii. kuwa Serikali imetangaza kuwavua madaraka. 

Sanjari na hilo , Mkuu huyo wa Mkoa amesema Walimu wakuu na Wakuu wa shule wa zamani ni tofauti na wale wa sasa, kwa kuwa sasa hivi wamekuwa maafisa masuuli wa shule zao ambapo wanapokea fedha za Elimu bila malipo kupitia akaunti za shule zao, hivyo ni lazima wapatikane watu waadilifu, wenye sifa na uwezo wa kuongoza shule na kusimamia fedha za Serikali.

Akichangia katika kikao hicho Afisa Elimu (Msingi) Wilaya ya Meatu, George Lowasa ameshauri Uchambuzi wa watu watakaoteuliwa ufanyike katika umakini mkubwa ili wapatikane watendaji wazuri na kuhusu utoaji wa takwimu sahihi alishauri kuwe na utaratibu wa kuziboresha kila (robo) baada ya miezi mitatu ili kuwa na takwimu sahihi pale zinapohitajika.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini amesema Uteuzi huo utazingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya uteuzi ambapo hakuna mtu atakayeonewa au atakayependelewa.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa amesema atawachukulia hatua Maafisa wale wanaolalamikiwa na walimu kwa kuwatolea lugha mbaya kila wanapotoa huduma kwa walimu hao katika Halmashauri za Mkoa huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini akizungumza na Maafisa Elimu na Viongozi wa CWT wa Mkoa huo (hawapo pichani) katika kikao maalum cha kutoa ufafanuzi wa agizo lililotolewa na Serikali Mkoani humo la kufanya mabadiliko ya Walimu wakuu na Waratibu Elimu kata, ambalo liliripotiwa tofauti katika vyombo ya habari na mitandao ya kijamii, kuwa Serikali imetangaza kuwavua madaraka.

Naye Katibu wa CWT Mkoa wa Simiyu, Said Mselema ameshauri baada ya mabadiliko ya wakuu wa shule na Waratibu wa Elimu Kata kufanyika wale ambao wataonekana hawana sifa za kuendelea kushika nafasi hizo waondolewe kwa staha, ambapo aliomba Serikali ngazi ya Wilaya na Mkoa ikishirikishe chama hicho katika masuala yote muhimu ya kuendeleza sekta ya Elimu, kwa kuwa wanamsaidia mwajiri katika usimamizi wa utendaji kwa walimu.

Kikao hicho cha wadau kilichofanyika mjini Bariadi na kimewahusisha Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Maafisa Elimu kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu pamoja na Wenyeviti na Makatibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ngazi ya Mkoa na Wilaya.

No comments: