Saturday, August 27, 2016

Kwanini ni Vigumu Kuwaamini CHADEMA Wanapodai kuwa Magufuli ni Dikteta?

Na. M. M. Mwanakijiji
Kuna msemo wa Kiswahili kwamba Aliyeumwa na nyoka, akiona unyasi anashtuka; msemo huo unafanana maudhui yake na ule wa Kiingereza kuwa Once bitten, twice shy. Misemo yote hii miwili inatukumbusha tu kuwa mtu yeyote aliyefikwa na jambo baya; na hasa jambo ambalo hakulitegemea kabisa basi anakuwa mwoga hasa mazingira yale yale yanapotokea tena kwani anaweza kuhisi jambo lile lile baya linaweza kumtokea tena.

Hili linanikumbusha mojawapo ya michango mikubwa ya Rais Kikwete katika mijadala ya kisiasa na lugha nchini ni pale alipoelezea wakati fulani jambo ambalo lilikuwa kama kichekesho lakini hadi leo limekolea ndani ya hoja za lugha zetu. 
Ni pale alipowahi kuhutubia huko nyuma na kuwaasa Watanzania kuwa wawe waangalifu kama alivyokuwa Mbayuwayu ambaye alipewa ushauri na ndege Gong’ota na ushauri ule kama angeusikiliza ungekuwa mwisho wake. Kwamba, Mbayuwayu alimuuliza huyo ndege jinsi gani anaweza kutoboa miti kwa midomo yake. 
Gong’ota akamwambia kuwa inabidi aruke kwa kasi halafu agonge mdomo wake kwenye jiwe mara mbili ndio utakuwa na uwezo wa kutoboa miti. Mbayuwayu  akakubali na akaenda kuchukua kasi alipokaribia lile jiwe akajiuliza nini kitamkuta akigonga jiwe; akaona ule ulikuwa ushauri mbaya na hivyo akajisemea “akili za kuambiwa changanya na za kwako”.
Swali langu la leo lina lengo la kujenga hoja tu kwamba huku tunakokwenda kuna watu wanaweza kabisa kutuambia kuwa jinsi ya kutoboa miti ni lazima tugonge midomo yetu kwenye mawe; na wapo ambao kati yetu wako tayari kuanza kuruka kasi na wamejipanga kura kasi kwenda kugonga jiwe ili wawe na uwezo wa kutoboa miti. 
Swali ni je watachanganya na za kwao?
Kuna watu ambao wanampinga Magufuli na ambao wanaamini kabisa kuwa Magufuli anaunda utawala wa kidikteta na wengine wanatumia hata neno “ufashisti”. 
Wapo ambao wanasema hivi wakiwa wanaongozwa na misimamo ya ndani kabisa (conviction) na hawafanyi hivi kwa sababu ya siasa. Yawezekana wengi wa hawa ni watu ambao kweli wanasema kwa sababu wanaamini katika wanachokisema. Hawa sina tatizo nao kwani wanaongozwa na imani na misimamo yao.
Hata hivyo kuna kundi jingine – na hili ndio kama yule ndege gong’ota – ambao wanasema tena kwa ukali sana lakini wanapaswa kusikilizwa na mtu ambaye anajua kuchanganya na za kwake. Na naomba kupendekeza kuwa wapo baadhi ya viongozi ndani ya upinzani ambao leo wakisema Magufuli ni “dikteta” au “dikteta uchwara” ni lazima Watanzania wenye kujua kuchanganya na za kwao wanahitaji kufikiria mara mbili kama kweli ndugu zetu hawa wanasema kwa sababu wanaamini kweli kweli (kama hilo kundi la kwanza) au wanasema hivyo kama sehemu ya kuendekeza usiasa hasa kwa vile rekodi yao kwenye haya mambo ya misimamo na kuita watu majina si ya kujivunia hasa.
Kwa muda mrefu baadhi ya viongozi hawa walituaminisha kabisa tatizo la Tanzania ni ufisadi. Na walimaanisha kweli kweli kiasi kwamba alama kuu ya ufisadi uliokubuhu wa Serikali ya CCM ilikuwa ni aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa. Viongozi hawa wa upinzani waliapa, walizungumza 
hata akatokwa  machozi kabisa wakituaminisha kabisa kuwa CCM ikimteua Lowassa kuwa mgombea wao basi itakuwa ndio mwisho. 
Na kwamba, walituaminisha kwa muda mrefu jinsi gani Lowassa alikuwa ameishikilia CCM kiasi kwamba alikuwa amepanga watu wake kweli kweli. Na ukweli huo wengine tuliamini siku ile jina la Lowassa lilivyokatiliwa na Kamati Kuu tulivyoona jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wakiimba kwa uthubutu  kuwa wana Imani na Lowassa! Na tukawaona kina Nchimbi na Sofia Simba walivyojitokeza katika jaribio lililoshinda la kuanzisha uasi dhidi ya kikao cha Kamati Kuu katika jitihada ya kumtetea Lowassa.
lowassambayuwayu
Wengi wetu tulitarajia kuwa baada ya Lowassa kukatwa jina lake, basi upinzani ungefurahi sana kwani sasa CCM ingeweza kumsimamisha yeyote yule na upinzani uliokuwa umejiandaa ukiwa na ajenda kali ya ufisadi utaenda kupeta. 

Lakini katika maajabu yote ambayo yamewahi kutokea katika siasa za Tanzania hakuna kubwa kama wale wale, waliopinga ufisadi, waliomuita Lowassa fisadi mkubwa na wakawabeza watu waliotaka kumpa uongozi na kumvumilia ndani ya CCM kuwa ni washirika wake wakaamua kumchukua kwa kupiga magoti mbele yake kuwa mgombea wao!

Yaani, yote waliyoyasema kuhusu ufisadi wa Lowassa, yote waliyoyasema juu ya uongozi wa Lowassa yakafutwa. 

Na tena wakageuza mpira na kusema “kama Lowassa alikuwa fisadi mahakama gani ilimuonesha?” tena na wengine wakauliza “kama serikali inaamini Lowassa fisadi basi wangemkamata” na kwa vile hajakamatwa na hakuna mahakama yoyote iliyomuona fisadi – bila ya kujali yale yote waliyoyaita kama ushahidi wa Lowassa (ikiwemo ile orodha ya mafisadi) – basi alikuwa ni mtu safi kabisa ambaye angeweza kubeba ajenda ya dhidi ya ufisadi kwa tiketi na kuwa Rais wa Watanzania.
Bahati mbaya kwao, siye mbayuwayu tukashtuka na kuchanganya za kwetu. Na mamilioni ya Watanzania nao wakashtuka wakachanganya na za kwao wakakwepa jiwe!
Sasa leo, kama vile wamesahau au wanadhania Taifa zima limesahau, watu wale wale, wakitumia mbinu ile ile, na lugha zile zile wamegeuza kibao na sasa wameamua kuja na hoja ya Magufuli Dikteta! Tena wana ushahidi mkubwa wa sheria kuvunjwa, na Katiba kuvunjwa  – kama walivyokuwa na ushahidi wa sheria na mifano mbalimbali ya ufisadi wa Lowassa.
Wale wale walioandamana kutaka Lowassa akamatwe na nakumbuka mmoja alisimama hadharani na kumuita Lowassa, mwizi, fisadi, na mnafiki lakini mwaka jana mtu huyo huyo alisimama na kumnadi mbele ya Watanzania! Watu wale wale walioshangilia Lowassa alipoitwa mwizi, fisadi na mnafiki kwenye mji ule ule walirudi na wakawa wazungusha mikono na kusema ati “Lowasaaaaa – Mabadiliko” Ndugu zetu hawa waligoma kuchanganya na kwao!
Sasa itakuwaje kwamba, watu wakaamini (na tayari inaonekana wapo walioamini hili) kuwa kweli Magufuli ni dikteta, halafu wakaanza kumuita kila aina ya majina – kama watu walivyofanya kwa Lowassa. Halafu Magufuli akawa na hali ndumu ndani ya chama chake na mwisho kweli akawa –kama wengine wanavyoombea – kuwa Rais wa awamu moja? Chama chake ikifika Juni 2020 baada ya mtifuano mkubwa zaidi kuliko wa 2015 ukalikata jina la Magufuli na kumnyima kugombea kwa tiketi ya CCM?
magufulimbayuwayu
Vipi Magufuli akaamua kuvamia meli ile ile ya CHADEMA? Na CHADEMA wakaamua kumchukua tena na kuanza kuimba “MAGUFULI- MABADILIKO” (Baada ya kumtupilia mbali mgombea wao wenyewe wa leo Lowassa)?

Sitoshangaa kabisa – kwani tayari kuna precendent – kwamba wapo watu ndani ya CHADEMA na Watanzania ambao leo wanamuita kabisa Magufuli Dikteta ambao wataamua kuanza kuzungusha vichwa (sijui kama watarudia kuzungusha mikono) na kuanza kusema Magufuli ndio Mabadiliko yao!  Sitoshangaa kabisa, wale wale ambao leo tunawaona kwenye TV na wengine wanatishiana hadi mahakamani na ambao watawafanya watu kuandamana kupinga udikteta – kama walivyowafanya kwenye ufisadi lakini baadaye wakagundua kuwa yule “dikteta” siyo dikteta kweli!
Kwamba, hakuna mahakama yoyote iliyomkuta na hatia ya vitendo vya kidikteta kama ambavyo Lowassa hakukutwa na hatia hiyo na kuwa hakuna mahali popote ambapo Serikali au chombo chochote kilimuona kuwa ni dikteta na hivyo akawa mgombea wao tena!
Hapa ndipo nasema kuwa Watanzania hasa waliyoyaona ya huko nyuma wamejifunza vizuri zaidi sasa; wanaelewa kabisa kuwa kuzungumza kwa ukali, kwa hisia n ahata kunukuu vifungu vingapi vya sheria havifanyi kuwa hoja za watu kuwa ni za kwali kwani tulishapitia hapa. 
Kwamba, wanachosema siyo tu wanamaanisha lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa ni siasa tu za kutafuta nafasi ya kubakia kwenye ulingo wa kisiasa.
Niliandika wakati ule (walipomchukua Lowassa) kuwa kuna watu waliokufa kwenye maandamano wakiamini wanapinga ufisadi ambao kama wangepewa nafasi ya kugundua kuwa vifo vyao havikumaanisha kweli chama kinapinga ufisadi kwani kilienda kumchukua yule yule ambao waliaminishwa kuwa ni fisadi nina uhakika vijana wale wasingethubutu ati kuandamana tena kumpinga Rais ati ni “dikteta” kwa vile tu anafanya mambo ambayo hawakubaliani nayo au yanayoonekana kuwa anatumia nguvu kubwa sana ya madaraka yake ya Kikatiba na Kisheria.
Na kwa vile hadi leo hii hakuna mahakama yoyote, au chombo chochote cha ndani au cha nje ambayo kina jalada au hata kesi moja ya udikteta wa Magufuli basi ni wajibu wa kila mtu kuanza kuchanganya na za kwake. Je, yuko tayari kwenda kupiga jiwe kwa kichwa ili awe kama gong’ota kwa vile ndio ameambiwa?
Lakini kwa wale ambao wanaamini kabisa wanapinga udikteta na kuwa hawajali sana maneno ya viongozi wa kisiasa na wako tayari kweli kufa kusimamia na kupigania kile wanachoamini hawa binafsi nawapongeza na nawatakia kila la kheri katika kusimamia kanuni zao. Binafsi naamini hawa ndio watu pekee ambao wanapaswa na wanaweza kuungwa mkono kusimama kuandamana kwa sababu wanafanya hivyo wakiamini kweli kweli.
Lakini wale ambao wanafanya hivyo kwa sababu wameambiwa na wale wale waliowaambie lile jingine basi hawa hatuna namna ya kuwasaidia bali tusubiri tuone tu kama baada ya kutoka kwa mwendo kasi kuliekea lile jiwe kama wataweza kubadili fikra zao baada ya ‘kusikiliza akili za kuambiwa, halafu wakachanganya na za kwao”.
Waswahili wanasema “Aliyeumwa na nyoka akiona unyasi anashtuka”. Wenzetu wazungumzao Kiingereza wanasema “Once beaten, twice shy“. Nani anabisha? Who would argue with that?

Nisome zaidi: zamampya.com 

No comments: