Monday, August 22, 2016

Kongamano la tano la kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kuanzia tarehe 23 hadi 25 Agost, 2016.

TUME YA TAIFA YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA
ISO 9001: 2008 CERTIFIED


 
Ndugu waandishi wa habari, tumewaiteni kuwaeleza kuwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), imeandaa Kongamano la tano la kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.

Kongamano hili ni fursa kwa wataalam wakiwemo watafiti, wabunifu, watunga sera pamoja na wajasiriamali kukutana na kujadili na kuelezea mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu katika kufikia taifa la viwanda. Kongamano la mwaka huu litafanyika kwa muda wa siku tatu, ukumbi wa Kisenga jengo la LAPF Kijitonyama, jijini Dar es salaam, kuanzia tarehe 23 hadi 25 Agost, 2016.
Kupitia kongamano hilo ambalo siku ya ufunguzi mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, wadau watatoa mchango wao wa namna sayansi, teknolojia na ubunifu vitakavyochangia kufikia uchumi wa viwanda katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ambayo ni mshauri mkuu wa serikali kwa mambo yote ya sayansi na teknolojia, imeratibu na kuhamasisha tafiti kulingana
na vipaumbele vya taifa hasa; kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili, viwanda, mazingira, nishati, TEHAMA na sayansi ya jamii.
Tafiti katika vipaumbele hivyo, yametoa matokeo chanya yanayodhihirisha uthubutu wa kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Watafiti watapata fursa ya kuwasilisha matokeo ya miradi kumi na mitano iliyofadhiliwa kwa pamoja kati ya serikali za Afrika ya Kusini na Tanzania  tangu mwaka 2013ambapo kila nchi ilichangia zaidi ya shilingi milioni mia tano. Matokeo ya tafiti hizi yanatupatia fursa ya kuwashirikisha watanzania ili wafahamu kinachoendelea katika Nyanja ya utafiti.
Baadhi ya matokeo ya tafiti yatakayowasilishwa kwenye kongamano hilo, ni pamoja na teknolojia ya kuongeza thamani na usindikaji wa ngozi. Teknolojia hiyo iliyogunduliwa chini ya COSTECH, mpaka sasa imewezesha kujengwa kiwanda kidogo cha ngozi Morogoro kwa ajili ya mafunzo. Mafunzo yatatolewa kwa wakurugenzi wa wilaya zote 136 nchini lengo ni kushirikiana na serikali kuwa na kiwanda cha ngozi kila wilaya.
Kabla ya teknolojia hii, kati ya ngozi milioni 8 zinazozalishwa kwa mwaka, ni asilimia 40 pekee zilikuwa na ubora. Tekonolojia hii itaongeza thamani ya ngozi mbichi za ng’ombe, mbuzi na kondoo na kufikia shilingi bilioni 89.5. Ngozi hizo zikisindikwa zitakuwa na thamani ya shilingi bilioni 300 kwa mwaka. Viwanda hivyo vikikamilika vitatengeneza bidhaa kama viatu, mabegi n.k vyenye thamani ya shilingi trilioni 3 kila mwaka.
Matarajio yetu ni kuwa kila kiwanda kitaajiri wafanyakazi rasmi 100 na wengine 500 wasio rasmi, hivyo wilaya zote zitaweza kutoa ajira kwa watu 81,600.
Ndugu waandishi wa habari, wasilisho lingine litakuwa la ugunduzi wa chanjo ya kuku yenye uwezo wa zaidi ya asilimia 80 kudhibiti magonjwa matatu ya kideli, ndui na mafua kwa kuku. Chanjo hii ipo katika hatua za mwisho kukamilika na kinajengwa kiwanda Morogoro kwa ajili ya kutengeneza chanjo hiyo. Tanzania kuna jumla ya kuku milioni 60 kulingana na takwimu za wizara ya kilimo hivyo endapo utatokea ugonjwa wa mlipuko na chanjo hiyo ikatumika, tutaokoa jumla ya kuku milioni 48 wenye sawa na thamani ya shilingi bilioni 2.8.

Tume pia imefadhili utafiti kwenye kilimo cha pamba ili kuongeza uzalishaji na kuwezesha viwanda vya nguo kupata mali ghafi ya kutosha. Awali mkulima angeweza kuvuna wastani wa kilo 800 kwa ekari moja lakini kwa kutumia kilimo cha kitaalam na mbegu zilizofanyiwa utafiti ataweza kuvuna wastani wa kilo 1,100 ikiwa ni ongezeko la kilo 300. Bei elekezi ya pamba ni shilingi 1,000 kwa kilo hivyo endapo mbegu mpya hii itaingizwa sokoni, mkulima atakuwa na ongezeko la shilingi laki 3 kwa kila ekari moja.  
Tume imefadhili utafiti wa kilimo cha mpunga katika kituo cha utafiti cha kilimo Dakawa. Wataalam wamegundua mfumo wa kilimo shadidi ambacho kupunguza matumizi ya mbegu kwa asilimia 80 ambapo awali ekari moja ilipandwa kilo 18 lakini sasa ni kilo 3 tu zinatosha kupanda shamba la ekari moja. Uzalishaji utaongezeka ambapo awali mkulima alivuna magunia 15 kwa ekari moja lakini sasa atavuna magunia 32.
Utafiti pia umefanywa kwenye kilimo cha mihogo na kugundua aina mbili za mbegu ambazo ni Kiroba kwa kanda ya kusini na Mkombozi kwa Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini. Mbegu hizi ni kinzani kwa magonjwa ya batobato na michirizi kahawia ambayo yanashambulia mihogo ya asili na kuzorotesha uzalishaji. Mbegu hizi za kisasa hutoa mavuno mengi. Jumla ya mbegu milioni moja zilitolewa kwa vikundi vya wakulima katika mikoa ya Mtwara na Mwanza. Wakulima wameongeza kipato kutokana na uzalishaji kuongezeka. Habari njema zaidi ni kuwa kiwanda cha kutengeneza  wanga utokanao na mhogo kitajengwa Mtwara au Lindi.
Ndugu waandishi wa habari, kuwa na taifa la viwanda ni lazima uzalishaji wa malighafi uongezeke mara dufu. Tume ya Sayansi na Teknolojia imefadhili utengenezaji wa mashine ya kuchakata mkonge. Mpaka sasa mashine imetengenezwa na ipo kwenye majaribio ya ndani. Mashine ina uwezo wa kuchakata majani ya mkonge 3,300 kwa siku. Mashine hii ni kwa ajili ya wakulima wadogo wadogo ambao wamekuwa wakitumia njia za zamani kuchakata mkonge. Mwezi Novemba itaanza kutumika kwa wakulima ambapo kwa kutumia mashine hii watapata nyuzi zenye ubora unaotakiwa.
Tume imejikita katika kuhawilisha teknolojia mpya kama vile teknolojia za kisasa zinazotumika kuendeshea mitambo viwandani (mechanotronics), teknolojia ya ndege zisizokuwa na rubani (drones), na teknolojia nyinginezo zinazotolewa kwa sasa
Ili nchi yetu iwe ya uchumi wa kati, katika sekta ya uendelezaji, uhawilishaji na ubiasharisha wa teknolojia, mambo kadhaa yanatakiwa kufanyika ikiwa ni pamoja na:

Kuanzisha na kuimarisha atamizi, kama ambavyo Tume ilivyoanzisha na kuimarisha atamizi ya DTBi. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011 atamizi imeanzisha kampuni 40 ambazo zimezalisha ajira kwa takribani vijana 300 na  ajira zisizo za moja kwa moja (indirect) 8,500 kwa mwaka. Atamizi hii inazalisha takribani dola milioni 1.5 kutokana na waatamizi kuuza huduma zao

Aidha, Atamizi hii imezalisha, kulea na kubiasharisha bunifu mbalimbali kutoka kwa vijana hususani katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kama vile mifumo bora na rahisi wa ulipaji kodi za serikali za mitaa, ulipaji huduma za maji na umeme, udahili wa wanafunzi wa vyuo vikuu, usikilizaji wa kipindi cha Bunge kupitia simu ya mkononi, ulipaji tiketi za mabasi kupitia simu ya mkononi.

Tangu mwaka 2010 mpaka sasa, serikali imeboresha uwezo wa watafiti 517, kwa kugharamia gharama za masomo kwa ngazi za shahada za uzamili na uzamivu. Kati ya hao, 445 wamehitimu masomo yao na sasa wamerejea katika vituo vyao vya kazi ili kuendelea kulitumikia taifa kupitia utafiti.
Ndugu waandishi wa habari, hayo ni baadhi tu ya mafanikio ambayo tume imeyapata. Malengo ya tume ni kuhakikisha inaendelea kutoa ushauri wenye tija kwa serikali kutokana na matokeo ya sayansi, teknolojia na ubunifu. Karibuni sana katika kongamono hilo.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Dr. Hassan Mshinda
Mkurugenzi Mkuu
Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia
22/08/2016



No comments: