Wednesday, July 13, 2016

WANYAMA WAHARIBIFU AINA YA NGEDERE WAHARIBU MAZAO YA WANANCHI WA MKALAMA.

Ni Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ibaga,tarafa ya Kirumi,wilayani Mkalama wakiwa kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mbunge wa jimbo la Iramba Mashariki,Bwana Allan Kiulla kwa lengo la kufanya mrejesho wa maamuzi mbalimbali waliyopitisha katika kikao cha Bunge lililomalizika mwezi uliopita.
 Ni Mbunge wa jimbo la Iramba Mashariki,Bwana Allan Kiulla akisaini kitabu cha wageni katika Kijiji cha Ibaga mara tu baada ya kuwasili katika uwanja wa mkutano wa Kijiji hicho.
Ni Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ibaga,wakiwemo wanawake na wanaume wakimsikiliza Mbunge wa jimbo la Iramba Mashariki,Bwana Allan Kiulla

Na,Jumbe Ismailly,Mkalama.
ZAIDI ya ekari 250 za mazao mbali mbali yakiwemo mahindi,mtama,karanga na alzeti katika kata ya Ibaga,tarafa ya Kirumi,wilayani Mkalama yameharibiwa na wanyama waharibifu waitwao ngedere na hivyo kusababisha wakulima wengi kutofikia malengo waliyojiwekea ya mavuno yao waliyotarajia.

Ngedere hao wanaokadiriwa kufikia zaidi ya 20,000 wamekuwepo katika kata ya Ibaga,tarafa ya Kirumi,Wilayani Mkalama na kuendelea kuwasumbua wakulima wa mazao hayo kwa kipindi cha takribani kati ya miaka saba hadi minane sasa.

Akitoa ufafanuzi wa swali lililoulizwa kwa Mbunge wa jimbo la Iramba Mashariki,Allan Kiulla na mkulima wa Kijiji cha Ibaga,Mwendomgelwa Kingu aliyetaka kufafamu serikali imejipangaje kuondoa kero ya wanyama hao waharibifu,diwani wa kata ya Ibaga,Salumu Abdallah Lindi alibainisha kuwa kero hiyo inatokana na Halmashauri ya wilaya ya Mkalama kutokuwa na wataalamu wa idara ya wanyamapori wa kupambana na wanyama hao waharibifu.

Aidha Lindi akizungumza katika mkutano ulioitishwa na mbunge huyo kwa lengo la kuwashururu wananchi kwa kumchagua ikiwa ni pamoja na kusikiliza kero zao zinazowakera uliofanyika katika Kijiji cha Ibaga,alisema wanyama hao wanaokadiriwa kufikia 20,000,wana zaidi ya miaka saba hadi minane kwenye eneo hilo na wanaendeleo kula mazao ya wananchi.

Kwa mujibu wa mwakilishi huyo wa wananchi tangu alipoingia madarakani mwaka 2015,alishatoa taarifa kwa afisa mazingira wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama bila mafanikio.
“Tangu nimeingia madarakani nikiwa kama diwani nilishawasiliana na afisa mazingira wa wilaya lakini mpaka sasa hivi hakuna juhudi zozote zile zilizochukuliwa dhidi ya kukabiliana na ngedere hawa”alisisitiza diwani huyo.

Hata hivyo Lindi alitumia fursa hiyo kuiomba serikali ya wilaya hiyo ikiangalie kilio cha wananchi wa kata ya Ibaga na kuhakikisha inamtuma haraka afisa mazingira ili aweze kwenda kwenye maeneo hayo na kuangalia uwezekano wa kukabiliana na ngedere hao ambao kwa kiasi kikubwa wanawaathiri wakulima wao.

Alisisitiza kwamba wakulima wa maeneo hayo wamekuwa wakiutumia muda wao mwingi kufukuzana na ngedere hao na kuacha kabisa kushiriki katika shughuli mbali mbali za mendeleo ya vijiji vyao.

Katika swali lake la msingi kwa Mbunge wa jimbo la Iramba mashariki,mkulima wa Kijiji cha Ibaga,Mwendomgelwa Kingu alimuomba mbunge huyo kuhakikisha wataalamu wa idara ya wanyamapori wanafika katika kata hiyo kwenda kuondoa kero ya wanyama hao waharibifu wa mazao.

“Hapa tumeingiliwa na wanyama wametoroka porini,naomba wahusika waje kwa njia yeyote ile wawarudishe porini kwa kutumia utaalamu wao wanyama hawa wanaitwa ngedere”alifafanua mwananchi huyo na mkulima wa Kijiji cha Ibaga.

Huku akimshirikisha Mungu katika kula kiapo,Kingu aliweka wazi kuwa pamoja na kutumia nguvu zao kulima mazao hayo,lakini akaonesha masikitiko yake kutokana na kugawana mapato ya mazao hayo na wanyama hao.

“Ukweli tunagawana mapato yetu hasa karanga na mahindi naomba kama mbunge wetu hili utatusaidiaje,yaani humo wameenea mwote humu tunagawana sana mavuno yetu,ukiwa kama mbunge hawa wanyama wametoroka”alifafanua mkulima huyo.

Akijibu hoja za wananchi wa Kijiji cha Ibaga kyhusu wanyama hao waharibifu,Mbunge wa jimbo la Iramba mashariki,Allan Kiulla aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kuwatumia viongozi wao kwa kuwapelekea matatizo yanayowakabili ili waweze kuyashughulikia.

“Sasa tutumie serikali zetu hawa si ndiyo tuliowachagua sisi wenyewe,hebu tuwaamini tuwatume kazi…..sawa basi tutafuatilia kwa karibu wilayani,tutafikisha na mimi leo napita wilayani ntafikisha ujumbe wenu huu,sawa jamani?alihoji Mbunge Kiulla.

Kwa upande wake diwani wa viti maalumu,Tarafa ya Kirumi,Habiba Issah Kununta alimthibitishia mbunge Kiulla kwamba suala la ngedere linawasumbua kwa kiasi kikubwa wananchi wa kata hiyo.
Hata hivyo mwakilishi huyo wa wananchi aliweka bayana kuwa wanyama hao waharibifu wamekuwa wakila mahindi,kwani mara tu wakulima wanapopanda mbegu,wanyama hao hufukua na kuanza kuzila mbegu hizo.

Alibainisha Habiba akiwa kama diwani wa viti maalumu Tarafa ya Kirumi alishawahi kwenda wilayani Iramba kabla ya kugawanywa kuwa wilaya mbili na kutoa taarifa mara mbili na walipogawanyika alitoa taarifa mara moja,lakini jibu alilopewa ni kwamba Halmashauri haina afisa mali asili wa wilaya,kitendo kinachoendelea kuwaumiza sana wananchi.

Akizungumzia uharibifu wa mazao hayo kwa niaba ya serikali,Afisa Tarafa wa Kirumi,Juma Salumu Sima alielezea jitihada zilizochukuliwa na serikali kuwa ni wananchi wenyewe kulinda mashamba yao ili wanyama hao wasiendelee kuvamia mashamba hayo pamoja na kutoa taarifa kwenye idara ya wanyamapori ili waweze kufika haraka kuwaondoa wanyama hao.

“Kuhusu na suala la uharibifu wa wanyama hawa ngedere katika eneo hili la Ibaga,kweli uchunguzi umefanyika zaidi ya ekari 250 zimeharibiwa na wanyama wale sababu wao wanakula kwa kuchimba karanga ambazo tayari zimeshakomaa na kula alzeti iliyokomaa na mahindi mashambani”alifafanua afisa tarafa huyo.
Aidha Sima aliweka bayana kwamba kufuatia tathimini iliyofanyika,ni zaidi ya ekari 250 zimeharibiwa na wanyama hao aina ya ngedere.

Kwa mujibu wa Sima juhudi walizochukua ni pamoja na wananchi wenyewe kulinda mashamba yao na kwamba wakulima hao wamekuwa wakiutumia muda wao mwingi kwa kazi ya kukabiliana na wanyama hao na kuacha kushiriki katika shughuli mbali mbali za mendeleo.

Hata hivyo kwa mujibu wa afisa tarafa huyo ni kwamba tayari wamekwishatoa taarifa wilayani kwenye idara inayoshughulikia wanyamapori ili waweze kwenda kuwasaidia kuokoa maisha ya watu na mali zao kutoendelea kuharibika kutokana na mashambulizi hayo ya ngedere.

No comments: