Na Dixon Busagaga wa Michuzi Blog,aliyekua Muleba, Kagera.
JUMLA ya Sh. Milioni 226 zimetumika kwa ajili ya
kujenga zahanati katika kijiji cha Ikuza wilayani Muleba mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa Diwani wa kata ya Ikuza, Fortunatus
Matta ni kwamba Zahanati hiyo ilijengwa na Shirika la Hifadhi za Taifa
(TANAPA), kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Muleba na Wananchi.
Alisema ili kukamilisha ujenzi huo, TANAPA ilitoa
Sh. Milioni 101, halmashauri ikatoa Sh. Milioni 80 huku wananchi wakichangia
Sh. Milioni 22.
“Tunaishukuru sana TANAPA kwa kupitia Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha
Rubondo, ambayo inapakana na kijiji chetu kwa kuonyesha nia kusaidia mradi huu
wa ujenzi kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi wetu,” alisema.
Alisema ujenzi wa jengo hilo kutaleta matumaini kwa
wananchi ambao walikuwa wanatumia kilomita 83 kwa ajili ya kufuata huduma za
afya kwenye kituo cha Afya cha Kanisa la AICT kilichopo Kasenyi.
Aidha, alisema licha ya jengo hilo kukamilika
lakini bado kumekuwa na tatizo la kupata watumishi, vifaa tiba na dawa.
Wakizungumza na waandishi wa habari, wananchi wa
kijiji cha Ikuza, wameishukuru TANAPA kwa kuwajengea Zahanati hiyo.
Mkazi wa kijiji hicho, William Lugaga alisema:
“Nashukuru Mungu, hakuna mwanamke yeyote ambaye aliwahi kuzama kwenye ziwa kwa
ajili ya kufuata huduma za afya.”
Kwa upande wake, Peragia Samson alisema wakinamama
wanapata shida sana wanatumia muda wa saa tatu kwa ajili ya kufuata huduma ya
Afya.
“Wakinamama wanajifungulia njia kabla hata ya
kufika hospitali na wengine kwenye boti,” alisema.
Naye, Kisanti Joseph alisema naona uchungu kuona
wanawake wajawazito wanapotaka kujifungua lazima wapande boti kwenda Kasenyi.
“Kuna wanawake wengine wanajifungulia kwenye
boti…hii yote ni kukosa huduma ya Afya,”alisema.
No comments:
Post a Comment