Thursday, July 21, 2016

SERIKALI YASISITIZA DHAMIRA KUCHUKUA MAENEO YA MADINI YASIYOENDELEZWA

Baadhi ya viongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi Limited uliopo mkoani Katavi, wakimwongoza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (mwenye Suti ya Bluu-mbele) na Ujumbe wake, kukagua maeneo mbalimbali ya Mgodi huo wa Kati, akiwa katika ziara ya kazi mkoani humo hivi karibuni. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Katavi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (mwenye Suti ya Bluu), akisikiliza maelezo kutoka kwa mmoja wa wachimbaji wadogo wa madini katika machimbo yaliyopo wilayani Mlele mkoani Katavi, Salum Nassoro, alipokuwa katika ziara ya kazi mkoani humo hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (aliyeinama), akikagua mojawapo ya machimbo ya dhahabu ya wachimbaji wadogo yaliyopo eneo la Ibindu wilayani Mlele mkoani Katavi hivi karibuni. Wengine pichani kutoka Kulia ni Mbunge wa Mpanda, Sebastian Kapufi, Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Magharibi, Daniel Mapunda, Msimamizi wa machimbo husika, Mejah Kambaloya, maafisa kutoka wizarani, Alex Nduye na Mhandisi Yusuph Msembele.
Mmoja wa wamiliki wa Machimbo ya Dhahabu yaliyopo eneo la Kapanda, wilayani Mlele Mkoa wa Katavi, Peter Gobolo (wa pili kutoka Kulia) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (wa tatu kutoka Kulia) na Ujumbe wake, namna wanavyochenjua Dhahabu kwa kutumia vifaa vinavyoonekana pichani.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (aliyeinua mkono), akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini waliopo katika machimbo ya Kapanda wilayani Mlele mkoani Katavi, hivi karibuni alipokuwa katika ziara ya kazi mkoani humo.

Na Veronica Simba - Katavi

Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuyachukua maeneo ya uchimbaji madini kutoka kwa wawekezaji wakubwa wasiyoyaendeleza na kuwapatia watanzania wengine ili wayaendeleze kwa manufaa yao na ya Taifa kwa ujumla.

Tamko hilo la Serikali lilitolewa kwa nyakati tofauti, hivi karibuni na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani wakati wa ziara yake katika Mikoa ya Katavi na Rukwa, kukagua miradi mbalimbali ya sekta za nishati na madini.

Naibu Waziri alisema kuwa, Serikali imebaini kuna maeneo mengi ambayo yanakaliwa na watafutaji wakubwa wa madini pasipo kuyaendeleza hivyo taratibu, sheria na kanuni zitatumika kuyachukua na kuyagawa kwa wengine.

“Ni kinyume kabisa na kifungu cha 63a, b na c cha sheria ya madini ya mwaka 2010. Itabidi tuyachukue maeneo hayo ili tuwakabidhi watanzania wengine wanaoweza kuyaendeleza na tayari tulishaanza kufanya hivyo.”

Dkt Kalemani alimwagiza Kaimu Kamishna Msaidizi wa Madini, anayeshughulikia Kanda hiyo ya Magharibi, Daniel Mapunda, kuandaa orodha mpya ya wawekezaji na watafutaji wa madini ambao wamehodhi maeneo pasipo kuyaendeleza ili ifanyiwe kazi mapema.

Katika hatua nyingine, akizungumza na viongozi wa Serikali pamoja na wananchi wa maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Katavi, Naibu Waziri alibainisha kuwa Mkoa huo ni kati ya mikoa saba inayoongoza kwa utajiri wa madini nchini na pia ni kati ya mikoa ambayo madini yake hayajachimbwa ipasavyo.

Alisema, kwa sasa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) wanafanya utafiti kutambua mbale inayowezwa kuchimbwa kama ni dhahabu au madini mengine lakini pia wanafanya utafiti wa kijiokemia, kijiofizikia na kijiolojia ili kujiridhisha kama kuna madini ya kuweza kuchimbwa na wachimbaji wadogo.

“GST walifanya utafiti huo kwa mara ya mwisho mwezi Aprili mwaka huu, lakini Serikali tumewataka warudie tena mwishoni mwa mwezi Agosti ili kabla hatujaanza kuwagawia maeneo ya uchimbaji tuwe na uhakika.”

Aidha, Dkt Kalemani aliwataka wananchi wanaojishughulisha na uchimbaji mdogo wa madini kuunda vikundi kwa ajili ya kupata ruzuku ambayo imetengwa na Serikali. Hata hivyo alisema kuwa, ruzuku hiyo haitolewi kwa kila mtu isipokuwa wenye vigezo.

Alivitaja vigezo vya msingi kwa mtu kupata ruzuku hiyo kuwa ni pamoja na muhusika kumiliki leseni ya uchimbaji madini iliyo halali na kwamba wawe watanzania peke yao pasipo wageni, ambapo alifafanua kuwa leseni za uchimbaji mdogo ni za watanzania tu kwa mujibu wa kifungu namba 8 cha sheria ya madini ya mwaka 2010.

Akizungumzia kiwango cha fedha za ruzuku ambacho Serikali imetenga kwa mwaka huu, Dkt Kalemani alisema kuwa ni shilingi bilioni 6.68.

No comments: