Friday, July 22, 2016

MAWAZIRI WA MAJI AFRIKA WAFANYA ZIARA WILAYANI BAGAMOYO

Na Eleuteri Mangi

Mawaziri wanaoshiriki mkutano wa kumi wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa nchi za Afrika wametembelea chanzo cha maji cha Ruvu Chini uliopo Bagamoyo Mkoani Pwani kwa lengo la kujionea namna Tanzania ilivyojizatiti katika kuhakikisha wananchi wanapata maji ya uhakika wakati wote.

Akizungumzia ziara hiyo, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwewe amesma kuwa mradi wa Ruvu Chini unahudumia baadhi ya wakazi wa wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na wakazi wa mkoa wa Dar es salaam.
Mhandisi Kamwewe aliwaambia Mwaziri hao kuwa chanzo hicho cha maji kinauwezo wa kuzalisha maji yapatayo lita milioni 275 kwa siku ambapo jiji la Dar es salaam peke yake wakazi wake wapatao zaidi ya milioni tano wanatumia maji kiasi cha lita milioni 450 kwa siku.

Kiasi kingine cha maji mengine ambayo yanatumika jijini dare s salaam Mhandisi Kamwewe alisema kuwa yanazalishwa katika chanzo cha maji cha Ruvu Juu ambapo zinazalishwa lita milioni 186 kwa siku.

Mhandisi Kamwewe aliongeza kuwa ili kuhakikisha wananchi wanapata maji ya uhakika kwa wakazi wa mikoa ya Pawani na Dar es salaam kwa manufaa ya maendeleo yao na kwa ujmla taifa.

Aidha, Serikali inaendelea kuhakikisha miundombinu ya maji inakuwa imara na bora wakati wote ambapo kwa sasa uboreshaji wa mabomba unafanyika mara kwa mara ambapo mabomba ya zamani yanaendelea kubadilishwa na kuimarishwa matanki ya maji yaliyopo eneo la chuo kikuu cha Ardhi, Kimara na Kibamba.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mawaziri wa Maji waliotembelea mradi huo wa Ruvu Chini Mhe. Anna Shiweda kutoka nchini Namibia amesema kuwa wamefurahishwa na Tanzania jinsi ilivyojipanga kuwahakikishia wananchi wake wanapata maji kwa maendeleo yao na wame wamevutiwa kwa jinsi chanzo hicho cha maji kilivyo na vifaa vya kisasa.

Akizunguzia upatikanaji wa maji katika nchi yake, Mhe. Anna amesema kuwa nchi yao ni miongoni mwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo eneo kubwa linakabiliwa na ukame ambapo wakazi wa nchi hiyo maji hupatikana kwa zaidi ya kilometa 250.

“Mkutano wetu umekuwa wa manufaa sana, tumefurahishwa na Tanzania kwa namna ilivyojidhatiti kuwapatia wananchi wake maji, tumejifunza na tunayachukua mawazo haya kwa manufaa ya nchi zetu” alisema Mhe. Anna.

Mhe. Waziri Anna amesema kuwa Namibia ina changamoto ya kuwa na ukame ambao unalikumba taifa hilo lenye idadi ya watu zaidi ya milioni 2.3, kutoka Tanzania wamejifunza mambo muhimu kupitia mkutano huo na Namibia imejipanga kutumia teknolojia inayotumia Tanzania ili nao waweze kuwahudumia raia wake waweze kupata maji safi na salama.

Maonesho ya wiki ya maji yanayofanyika Dar es salaam yanahudhuriwa na Mawaziri wa Maji kutoka nchi 38 zikiwemo Tanzania ambayo ni mwenyeji wa maonesho hayo, Sudan, Kongo, Lesotho,Madagaska, Burundi, Namibia, Nigeria, Rwanda, Senegal, Togo, Liberia, DRC na Zimbabwe.

Nchi nyingine zilizoshiriki ni pamoja na Libya, Kenya, Misri, Ivory Coast, Cameroon, Msumbiji, Zambia, Sudan Kusini, Bukina Fasso, Afrika Kusini, Mali, Ethiopia, Benin, Mauritania, Uganda na Djibouti.
Meneja wa Mtambo wa Ruvu Chini Mhandisi Emmanuel Makusa akiwaelezea baadhi ya Mawaziri wa Maji wa nchi za Afrika waliotembelea mtambo huo kujifunza namna Tanzania inavyojidhatiti kuwapatia maji wananchi wake.
Baadhi ya Mawaziri wa Maji wa nchi za Afrika wakitembelea maeneo mbalimbali ya mtambo Ruvu Chini kujifunza namna Tanzania inavyojidhatiti kuwapatia maji wananchi wake.
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwewe akiwaeleza baadhi ya Mawaziri wa Maji wa nchi za Afrika namna mradi wa Ruvu Chini unavyowahudumia baadhi ya wakazi wa wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na wakazi wa mkoa wa Dar es salaam.
Mhifadhi wa Mji Mkongwe wa Bagamoyo Noel Laswai akiwaeleza baadhi ya Mawaziri wa Maji wa nchi za Afrika namna mji wa kale wa Kaole ulivyokuwa tangu karne ya 13.
Mhifadhi wa Mji Mkongwe wa Bagamoyo Noel Laswai akiwaeleza baadhi ya Mawaziri wa Maji wa nchi za Afrika mti aina ya mpingo unaohifadhiwa katika eneo la Kaole namna unavyotumiwa ambao mti huo una zaidi ya miaka 30.
Waziri wa Mji wa Namibia Anna Shiweda na Waziri wa kutoka nchini Libya Assayed Abdurrahaman Naji wakiangalia baadhi ya mabaki ya viumbe vinavyoishi baharini katika ufukwe wa Bagamoyo wakati wa ziara ya kujifunza namna Tanzania inavyotunza rasilimali zake kwa mnaufaa ya sasa na baadaye.
madhari za baadhi ya maeneo ya fukwe za wilaya ya Bagamoyo zinavyovutia kwa utalii na michezo mbalimbali. (Picha na Eleuteri Mangi-MAELEZO)

No comments: