Monday, July 4, 2016

HOJA YA HAJA KUTOKA LILONGWE, MALAWI: WANASIASA WETU KWA NINI MNATAKA KUTUANGAMIZA?

Na George Simon, Lilongwe
Ankal, nipe lau nafasi. nipate kusema na Watanzania wenzangu kuhusu mustakabali wa nchi yetu Tanzania. Thank you in advance....
NIKIWA mbali na nyumbani nimejitahidi kuwa mvumilivu lakini naona uvumilivu unanishinda. Nakufikiria nyumbani kwangu, nawafikiria ndugu zangu, nazifikiria shughuli zao, biashara zao, utalii, ufugaji, kazi za wasanii, vijana waliojipatia ajira ya kusindikiza wageni kwenye vivutio (tour guides) na wengine wengi.
Kwa kweli naona giza nene mbele yangu. Imekuwa bahati mbaya tu kwamba sioni kama hili ninaloliwaza mimi nikiwa nje ya nchi linazungumzwa na ndugu zangu waliopo nyumbani hasa vijana ambao ndio tegemeo la taifa na ndio nguvu kazi inayotegemewa.
Naandika haya nikiwa natafakari harakati za kisiasa zinazoendelea nchini mwangu hasa kwa wanasiasa waliopo upinzani ambao wengi wao ni wabunge wanaoendesha fukuto la mapambano dhidi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Naomba niweke wazi kuwa japokuwa mimi sio mwanasiasa lakini ni mfuatiliaji mkubwa wa shughuli za wanasiasa tena kwa sababu nipo nje ya nchi hujikuta kazi hii ya kufuatilia shughuli za kisiasa zinazoendelea nyumbani inanigharimu muda mwingi na fedha.
Kwa hili ninaloliona kuwa ni harakati za wanasiasa wa upinzani kuendesha fukuto la mapambano dhidi ya serikali ya Rais Magufuli ambayo imejipambanua sio tu nchini Tanzania bali duniani kote kuwa imeamua kurekebisha makosa yaliyofanywa na serikali katika awamu zilizopita, linanishangaza sana.
Nashangaa zaidi pale napoona mapambano yenyewe yanalenga kuvuruga amani na utulivu vitu ambavyo ni tunu ya Watanzania. Nashangaa sana kuwasikia wanasiasa walio kwenye upinzani wanaendesha siasa za kichochezi, zisizo na heshima na zisizokubalika.
Najiuliza hivi ni kweli wanasiasa wa upinzani wamekosa kabisa mbinu za kisiasa za kujijenga mbele ya watanzania mpaka wanaamua kuendesha kampeni za kuvuruga amani?
Sasa leo nimeona niwaulize kwa nini wanasiasa wa upinzani wanataka kutuangamiza?Nakumbuka pale Arusha ninapotoka kila mtu hapo nchini ni shuhuda wa matokeo ya hizi harakati za wanasiasa wa upinzani zisizo na tija.
Si Arusha tu bali na mikoa mingine ya Kaskazini hasa Kilimanyaro na Manyara ambako nako wananchi wamewachagua wabunge wengi wa upinzani. Napata mashaka makubwa kama staili hii ya siasa za kukurupuka haitaathiri na mikoa hiyo.
Sio siri uchumi wa mikoa hii niliyoitaja unabebwa kwa kiasi kikubwa na utalii. Moja ya mambo muhimu kwa utalii kushamiri ni kuwepo kwa amani na utulivu, sasa nashindwa kuelewa wabunge wetu ambao kila siku mnahubiri siasa za vurugu mnataka kutuua njaa? 
Mnataka kuwatisha watalii waache kwenda kwenye vivutio vyetu ili tukose hela? Mnataka kampuni za utalii zipunguze ajira kutokana na kupungua kwa wageni? Mnataka bidhaa za sanaa kama vile vinyago, shanga, nguo za kijadi na bidhaa nyinge zikose soko? Mnataka watalii wahamie nchi jirani? Mnataka tuanze kuwafuata watalii nchi jirani ili tukafanye biashara?
Mimi nadhani wananchi wenzangu wa Arusha, Manyara na Kilimanjaro sisi ndio tuwe wa kwanza kuwaambia wabunge wetu wa upinzani, hapana. Tuwakataze kufanya siasa za vurugu, tuwakataze kufanya uchochezi na kutaka kuwatumia vijana wa nchi hii kupambana na dola bila sababu za msingi.
Tanzania ni nchi inayopiga hatua za kimaendeleo, tuunge mkono juhudi za maendeleo na pale ambapo kuna juhudi za kukwamisha maendeleo tukatae. Haiwezekani leo wanasiasa waanze kutaka kutuaminisha kuwa kwa sababu mmesusa kukaa bungeni kwa hiyo Tanzania isikalike. 
Nani aliwaambia wawe wanatoka bungeni? Ni kanuni ipi imevunjwa? Haya ona sasa mnafanya mambo ya kitoto kabisa Bungeni. Mbunge uliyeaminiwa na wananchi ukawawakilishe unafika bungeni tena mbele ya vyombo vya habari unaonesha ishara za matusi dhidi ya wabunge wenzako ambao ni watu wazima tena wenye umri wa Baba yako na Mama yako! 
Ni kweli tunahitaji demokrasia lakini kama ni ya mtindo huu hapana, mimi nafsi yangu inakataa. Inakataa kwa sababu huko ni kujenga taifa lisilo na heshima na adabu. Kwa umasikini wa nchi yetu hatupaswi kuzungumzia vurugu tunapaswa kuzungumzia maendeleo na maendeleo yatapatikana kwa kufanya kazi sio kupiga maneno ya kisiasa kila siku. 
Na ili tuweze kufanya kazi ni lazima kuwe na utulivu na utulivu hauwezi kuja kwa watu kila siku kupanga mipango ya kuandamana na kupambana na polisi. Na ndugu zangu vijana niwambie ukweli wanaowahimiza muandamane wana hali nzuri ya uchumi.
Wanamiliki mahoteli makubwa, wana kampuni kubwa za biashara, wengine wana hifadhi kubwa za fedha na mali nyingine na zaidi wao ni wabunge na wanalipwa na bunge fedha nzuri.
Wanatembea kwenye magari mazuri, kuishi majumba ya kifahari, kula vizuri na kuvaa vizuri. Ni hawa hawa ambao utalii wetu, biashara zetu, ajira zetu na hata usalama wetu vikitoweka wao hawapati madhara yoyote.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliwahi kusema siku zote tutumie akili za mbayuwayu yaani “Akili za kuambiwa changanya na za kwako.” Nionavyo wakati wa kuchanganya akili za kuambiwa na za kwetu umefika. Ni muhimu tuanze kuangalia jambo gani jema na jambo gani la hovyo.
Rais Magufuli ameshasema sasa tujielekeze kufanya kazi, basi tufanye kazi; amesema tulipe kodi, ni vizuri tulipe kodi; ameamua kuelekeza fedha nyingi za umma kwenye maendeleo (40% ya bajeti ya 2016/2017) ni vizuri tuunge mkono.
Polisi wanasema mikutano na maandamano yamezuiwa kwa sasa kwa sababu ya viashiria vya vurugu, tutii sheria. Tusipofanya hivyo na tukachagua kukiuka maelekezo ya polisi kitakachofuata tunakijua, sasa ni kutumia akili yako tu kwamba ama unatii sheria kwa kutoshiriki mikutano ya hadhara na kuandamana ama unashughulikiwa na polisi.
Viongozi wetu wanaohimiza mapambano dhidi ya polisi nitafurahi sana nikiwaona wao wapo mbele kukabiliana na polisi kuliko kuwatumia na kuwatanguliza vijana wakati wao wakiwa wamejificha majumbani mwao ama mahotelini mwao.
Uchaguzi umekwisha waliopata urais wamepata, waliopata ubunge wamepata na waliopata udiwani wamepata. Kinachonipa faraja ni kuwa vyama vya upinzani vimeongeza idadi ya wabunge na madiwani pia. 
Nilichoelewa mimi kutokana na uchaguzi wa mwaka jana ni kuwa nguvu ya upinzani imeongezeka na imekuwa ikiongezeka tangu uchaguzi wa mwaka 2010. Sasa hakuna sababu ya kutumia mbinu haramu, wapinzani wapange mipango yao uchaguzi ujao watasonga mbele zaidi kama watanzania watawakubali lakini kwa mtindo huu nina wasiwasi uchaguzi ujao wakapoteza nguvu yao.
Naomba kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli kwa juhudi anazozifanya kuiweka sawa Tanzania. Mzee we endelea tu, siku zote kwenye kazi ya kumtibu mgonjwa mwenye kidonda inahitaji ujasili hasa wakati wa kusafisha kidonda na kukitia dawa ile inayouma. 
Katika kazi hiyo mtu atapiga kelele sana lakini mwisho wa siku kidonda kitapona na atasimama kwa furaha na kicheko. Sisi watanzania wenye hamu na kuona kero zinazotukabili zinashughulikiwa tupo nyuma yako na tunakuunga mkono. 
Na nakuhakikishia vijana wengi ninaozungumza nao huko nyumnai kwa sasa nao wanafikiri tofauti, wengi wanasema bayana kuwa wakiitwa kwenye maandamano hawataenda labda wale vijana wao wanaowasafirisha kutoka mikoa mingine kwenda kufanya fujo kwenye mikoa mingine.
Natamani ningekuwa Tanzania ili nikaombe kazi ya kusaidiana na polisi wakati wa kuwashughulikia vijana wanaosafirishwa kwenda kufanya fujo sehemu nyingine maana sasa hamna namna.
Tena kwa kuwa mimi ni mtanzania mwenye uchungu na nchi yangu nawaombeni polisi mkimkamata mtu anayekataa kutii amri kwa kushinikizwa na hawa jamaa wanasiasa wasio na mikakati hakikisheni akitoka rumande anakuwa kijana mwema zaidi kwa Taifa lake. 
Maana mimi huwa sielewi mtu analala rumande halafu akitoka bado anakuwa jasiri wa kuongea na kuonesha yeye ni shujaa. Polisi kwani vipi? Huko polisi kumekuwa hoteli ya nyota tano? Unalala polisi halafu unatoka unashangilia wapi na wapi?
Ni lazima tujenge taifa lenye nidhamu, tukiendelea na mtindo huu wa kuwa na taifa ambalo mtu anaamua tu kumtukana Rais, anajiona yeye ndio anajua kila kitu, anadharau serikali na vyombo vya dola eti kwa sababu anajivunia elimu aliyoipata kwa fedha za walipa kodi wa nchi hii, hatutafika kabisa kabisa.
Haiwezekana leo mtu anamtukana Rais kwa uwazi tena kwenye kupitia vyombo vya habari, kana kwamba hiyo haitoshi anakwenda kuchapisha pia tisheti zenye kumtukana Rais na zinasambazwa mitaani. 
Tanzania sio nchi ya kihuni, Tanzania ni nchi yenye heshima na heshima hii imejengwa kwa jasho jingi. Wapo watu wameumia kuhakikisha Tanzania inafikia hapa ilipofika.
Kwa kweli kama Mheshimiwa Rais Magufuli unayasoma haya ninayoaandika naomba nikuhakikishie hata sisi tuliopo nje ya nchi tunaumizwa sana na vitendo vinavyofanywa na wanasiasa wetu wa upinzani. 
Tunashindwa kuwaelewa wakati dunia nzima inakusifia kwa hatua makini unazochukua wapo watu waliopo humo humo ndani wanazibeza na kutaka kuwaaminisha watanzania kuwa hufai. Hawatafanikiwa.
Na hao jamaa wanakusakama humo humo Tanzania tu wa kivuka mpaka nje ya Tanzania hakuna atakayewasikiliza. Na wao wenyewe wanalijua hili vizuri kabisa na hawawezi kuthubutu kufanya hivyo.
Nimalizie kwa kuwataka viongozi wengine wote wakiwemo mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na vyombo vyote vya dola kusimama kidete kutekeleza majukumu yao. 
Uzuri wa awamu hii ya tano hakuna kufanya mambo kwa mipango mipango. Maana tulikotoka baadhi ya viongozi waliogopa kuchukua hatua kwa kuhofu kuwagusa marafiki na jamaa wa vigogo - safari hii hicho kitu hakuna. Kila kitu kinafanyika kwa mujibu wa sheria na Rais Magufuli ameshasema atakayevunja sheria ashughulikiwe bila kujali ni nani.
Nawatakieni watanzania wote mafanikio makubwa katika safari ya kuelekea uchumi wa kati kupitia uchumi wa gesi na viwanda.

5 comments:

Anonymous said...

The mdudu, Asante sana yaani siamini kama kweli unatoka ARUSHA mbona unabusara hakika maneno yako tayari mbona vijana wengi tushaamua kuwa nyuma ya rais wetu mpendwa John Pombe Magufuli na serikali yake yote kwa ujumla again asante sana mkuu kwa hekima zako

Anonymous said...

Upizani wameonyesha dhahiri yakwamba wanachokipigania sio kwa ajili ya Tanzania na watanzania bali ni maslahi yao binafsi anaepigania maslahi ya Tanzania na watanzania kwa vitendo sio kwa matusi tunamjua. Mtu anathubutu kumwita raisi aliechaguliwa na wananchi kwa njia ya demokrasia dikteta kwa kisingizio cha demokrasia,kwenye chi inayoongozwa kidikteta kweli utathubutu kumwita raisi wa nchi dikteta alafu bado unaranda mitaani? Kwa watu wanatakiwa kuwa makini na kauli zao za kipuuzi.

Anonymous said...

Asante sana mdau kwa makala haya. Ombi langu ni kwa vyombo vya habari vyenye mapenzi mema na Tanzania kusambaza makala haya kila kona kadri inavyowezekana ili jamii yote ijipambanue na wavuruga Amani nchini. Naema tena asante sana tena sana.

Anonymous said...

Asante sana mdau kwa makala haya. Ombi langu ni kwa vyombo vya habari vyenye mapenzi mema na Tanzania kusambaza makala haya kila kona kadri inavyowezekana ili jamii yote ijipambanue na wavuruga Amani nchini. Naema tena asante sana tena sana.

Anonymous said...

Kwa upande wangu nimefarijika sana kusoma makala hii na nadhani tatzo kubwa watu fulani kuonekana wanajua kushinda wengine,kama kweli spika ni tatzo ina maana hamna spika hata mmoja alishafanya jambo jema au wao wanajiona wako sahihi kushinda watu wengine,wito wangu kwa vijana mwanasiasa akikuhamasisha kuingia barabarani mwambie familia yake iko wapi pamoja na yeye awepo mstari wa mbele ili wote mkaandamane hata kaa hata siku moja kukuambia ukaandamane,Mtu anakuambia mkaandamane hali ya kuwa yy anaongelea hotelin na akiwa na ulinzi mkubwa na ww unakimbia bila kujiuliza mara mbili ukivunjwa miguu atakuja kutoa pole ya ujumla kama mko kumi au zaidi baada ya hapo ndg yangu hicho kilema ni chako si cha mwenyekiti na familia yako ndio itakayokuhudumia.TUBADILIKE TUMEPATA MTU SAHIHI KWA MUDA SAHIHI,TUMWACHENI APIGE KAZI RAIS WETU MPENDWA JPM NAMKUBALI SANAAAA