Na John Nditi, Morogoro
MOTO mkubwa umeteketeza Jengo la Idara ya Uzalishaji la Kiwanda cha 21st Century Textiles Ltd ambapo zamani kabla ya kubinafsishwa na Serikali kilijulikana kwa jina la Morogoro Polyester Textile Ltd ambapo bado haikujulikana hasara iliyopatikana.
Moto huo ulianza majira ya saa 12: 45 asubuhi ya Julai 19, mwaka huu kwenye Kiwanda hicho kilichopo eneo Viwanda Kihonda, Manispaa ya Morogoro.
Kufuatia kutokea kwa moto huo, Kikosi cha Jeshi la Uokoaji na Zimamoto kwa kushirikiana na Polisi walifika eneo la tukio mara moja na kuanza kazi ya kuzima moto uliokuwa ukiwaka kwa nguvu juu ya paa la Jengo hilo .
Kamanda wa mkoa wa Morogoro , Jeshi la Uokoaji na Zimamoto, Ramadhan Pilipili, alisema licha ya kuwahi eneo la tukio, bado walikabiliana na ugumu wa kuingia ndani hivyo kulazimika kutoboa ukuta kwa kutumia katapira ili kupata nafasi ya uwazi ya kurusha maji ndaniya jengo ili kuuzima.
Hivyo alisema , ndani ya jengo hilo kulikuwa na marotoba ya pamba ambayo yalishika moto na kuwawia vigumu kuingia ndani na kulazimika kwanza kutoboa sehemu za ukuta wa jengo ili kupenyeza maji yatakayowezesha kuuzima moto huo.
Kamanda wa mkoa wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto alisema jitihada za kuuzima moto huo zilikuwa zinaendelea hadi majira ya saa tisa alasiri ambapo pia waliungana na timu ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuezesha zoezi la kuuzima moto huo.
Katika tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei aliungana na viongozi wengine na vikosi hivyo ili kuona moto huo unadhibitiwa ili usiweze kuleta madhara makubwa zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe aliyefika kujioenea tukio hilo alitumia fursa hiyo kuuagiza uongozi wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto mkoa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika viwanda.
Dk Kebwe alisema , lengo ni kuona maeneo ya viwanda vinakuwepo vifaa vya dharura vinavyofanya kazi ya kuzima moto unapojitokeza ikiwemo na maeneo mengine ya majengo ya matumizi ya mkusanyiko wa kazi.
“ Maeneo kama haya ya viwanda ni lazima kuwepo na vitu vya tahadhari , kama sehemu za kuchota maji , vifaa vya kuzimia moto viwemo ndani ya viwanda na maeneo mengine ili moto unapozuka iwe ni rahisi kuwahi kuuzima” alisema Dk Kebwe.
Mbali na hayo, pia mkuu wa mkoa alimwagiza Kamanda wa Polisi wa mkoa kulimaisha ulinzi eneo hilo ili kuzuia vibaka na wezi kuweza kuiba mali zilizopo.
Naye Meneja Uzalishaji Kiwanda cha 21st Century Textiles Ltd, Clemence Munis , alisema kuwa moto huo ulitokea kwenye Idara ya usokotaji wa nyuzi za nguo baada ya moja ya mashine zake kutoa cheche na kurukia katika marotoba ya pamba na kisha kuwaka moto uliokwenda kunasa kwenye nyanya za umeme.
Munis alisema wakati wakianza kuchukua hatua za kuzima kwa kutumia vifaa vya kuzima ndani ya kiwanda , walikiarifu Kikosi cha Jeshi la Uokoaji na Zimamoto pamoja na Polisi wa mko ambao walifika katika kipindi cha muda mfupi kiwandani hapo.
“ Moto umetokea majira ya saa moja kasorobo asubuhi ya leo ( Julai 19) sehemu ya uzalishaji baada ya kutokea hitirafu ya umeme kwenye mashine ya kusokota pamba “ alisema Munis.
Kiwanda hicho kina majengo na idara mbalimbali ikiwemo ya usokotaji, useketaji na umaliziaji wa nguo na mashine zinazotukika kwa kazi hizo.
“ Nawapongeza Jeshi la Ukoaji na Zimamoto Morogoro, wamefika kwa wakati ndani ya dakika 10 na kuanza kuzima moto wakishirikiana Polisi , wananchi na wafanyakazi wakiume na ninatumai zoezi litafanyikiwa kwa haraka na mali nyingi kuokolewa” alisema Munis.
Munis alisema hakuna madhara ya kibinadamu , isipo kuwa moto huo umetekeleza marotoba ya pamba ,nguo na mashine zilizokuwepo katika idara hiyo ambapo bado kiwango cha gharama halisi ya hasara iliyotokana na moto huo kujulikana .
“ Bado hatuajua hasara kamili , isipokuwa moto huu umetekeleza mali nyingi hasa marotoba ya pamba, nguo na mashine eneo la idara ya ufumaji wa nguo ...na hii itajulikana baaada ya kufanyika kwa tathimini “ alisema Munis.
Kiwanda cha 21st Century Textiles , kimuundo ni kampuni tanzu ya Mohamed Enterprises ( TANZANIA) LTD – (MeTL) na ilianza uzalishaji mwaka 2005, baada ya kununua katika zoezi la ubinafsishaji mali za kampuni ya umma iliyojulikana kwa jina la MOROGORO POLYESTER TEXTILES LTD.
No comments:
Post a Comment