Friday, June 10, 2016

Vodacom yaja na Gulio la Simu halisi za gharama nafuu

Gulio la simu Expo litakalofanyika katika viwanja vya posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam kesho Jumamosi na Jumapili wiki hii litawawezesha wateja wa Vodacom Tanzania na wananchi kwa ujumla kujipatia simu za uhakika zenye gharama nafuu ikiwemo simu za bure kwa wateja watakaonunua vifurushi vya aina mbalimbali vya muda wa maongezi na intanenti.
Akiongea juu ya gulio hilo,Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom Tanzania,Rosalynn Mworia alisema kuwa lengo la gulio hili ni kuwawezesha wateja wa kampuni kuweza kupata maelezo kuhusu huduma za kampuni ikiwemo kuweza kununua simu halisi zenye viwango vinavyotakiwa kwa gharama nafuu kuanzia simu za shilingi elfu 18/- na kuna ofa ya wateja kujipatia simu za bure kabisa.

“Gulio hili la Vodacom Simu Expo limekuja katika wakati mwaafaka ambapo tarehe ya mwisho ya kuzima simu zisizo na viwango inakaribia hivyo tunawakaribisha wateja wetu wote watembelee gulio hilo na kuweza kujipatia simu zenye viwango vinavyostahili kwa gharama nafuu ambapo pia watapata fursa ya kupata maelezo ya huduma zetu mbalimbali” Alisema.

Alisema katika gulio hilo pia kutakuwepo na watoa huduma mbalimbali ambao watashughulikia matatizo ya simu za mkononi pamoja na huduma zinginezo kwa wateja watakafika kwenye gulio hilo.

Mworia alisema katika Simu Expo pia yanakaribishwa makampuni yanayouza simu nchini kushiriki na kuhakikisha yanatoa punguzo maalum kwa wateja  kwa ajili ya kuwanufaisha wateja hususani katika kipindi hiki cha mwisho ambacho Mamlaka ya Mawasiliano(TCRA) inakaribia kuzima simu zisizokidhi viwango,hatua ambayo itawaathiri baadhi ya watumiaji wa simu kwa kuachwa nje ya mtandao.

Kuhusiana na ofa ya kujipatia simu ya bure alisema kuwa mteja atakayenunua kifurushi cha muda wa maongezi wa dakika 330 za kupiga mitandao yote chenye jumbe fupi za maneno 2000 na MB 500 za intanent ambacho kinadumu kwa mwezi mmoja atajipatia simu yenye thamani ya shilingi 18,000/-,wakati atakayenunua  kifurushi cha dakika 550 cha kutumia mitandao yote chenye jumbe fupi za maneno na MB 500 atajipatia simu  yenye thamani ya shilingi 25,000/-.

Pia alisema kuwa wateja watakaonunua kifurushi cha dakika 1000 cha kupiga mitandao yote chenye jumbe fupi za maneno 10,000 na MB 500 za internet kinachodumu kwa kipindi cha mwezi mmoja atajipatia simu ya bure yenye thamani ya shilingi 50,000/-

Alisema ofa ya simu za bure inawahusu wateja wanaotumia simu za Smart phone wanaoishi jijini Dar e Salaam ambao tayari wamefahamishwa kuhusu ofa hii kupitia jumbe fupi za maneno na pindi watakaponunua vifurushi kwa mujibu wa maelekezo waliyopewa wataweza kujipatia simu bure za aina ya Smart Phone ITEL 1406.

“…Tunawaomba wateja wetu na wananchi wote wafike katika viwanja vya Kijitonyama ili waweze kujipatia simu nzuri na za kisasa wazipendazo kwa punguzo la bei hadi asilimia 50 kwa baadhi ya simu na kupata ofa ya simu za bure kwa kununua vifurushi,” alisema

No comments: