Tuesday, June 7, 2016

Mwarobaini wa kukatika kwa umeme Arusha wapatikana Ni baada ya kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha KIA, Wateja zaidi ya 89,000 waunganishwa

Na  Greyson Mwase, Arusha

 Imeelezwa kuwa kukamilika kwa kituo cha  kupoza umeme  cha KIA kilichopo karibu na  Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kilimanjaro  International Airport) kumepelekea tatizo  la kukatika kwa umeme kuisha katika mkoa wa Arusha na baadhi ya maeneo  ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro na kuongeza kipato   kwa wakazi wa mkoa huo.

Kauli hiyo ilitolewa na Meneja wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mkoa wa Arusha Mhandisi Gaspa Msigwa,  kwenye ziara ya waandishi wa habari kutoka  vyombo mbalimbali  vya habari nchini katika miradi ya  TEDAP na mradi wa usafirishaji umeme kutoka Iringa  hadi Shinyanga katika msongo wa kilovolti 400 (BITP) inayofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).
Sehemu ya kituo cha kupoza umeme cha KIA 132/33kV kilichopo mkoani Kilimanjaro kama kinavyoonekana pichani.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kuona hatua za utekelezaji, mafanikio na changamoto za miradi hiyo pamoja na kupata maoni ya wanufaika wa miradi hiyo.

Akielezea mradi huo Mhandisi  Msigwa alisema ujenzi wa kituo hicho uliogharimu Dola za Marekani Milioni 7, ulianza mwaka  2011 na kukamilika mapema   Desemba mwaka  2013.

Alisema   kabla ya ujenzi wa kituo hicho, umeme ulikuwa unasafirishwa kutoka katika kituo cha Kiyungi kilichopo mkoani Kilimanjaro hadi jijini Arusha umeme ambao  ulikuwa hautoshelezi katika matumizi ya  majumbani na katika  viwanda vidogo.
Meneja Miradi ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme kutoka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mhandisi Emmanuel Manirabona (wa pili kutoka kulia) akielezea mafanikio ya kituo cha kupoza umeme cha KIA 132/33kV kilichopo mkoani Kilimanjaro.

Aliongeza kuwa  pia kulikuwepo na tatizo la kupotea kwa  umeme mwingi kutokana na  kusafirishwa katika umbali mrefu.

Alisema kuwa  tangu  kukamilika kwa kituo hicho  wateja zaidi ya 89,000 waliunganishiwa umeme ambapo mpaka sasa wanapata umeme ambao ni wa uhakika.

Alisema kutokana na ongezeko la wateja pamoja na kupatikana kwa umeme wa uhakika katika mkoa huo, TANESCO imeweza kukusanya  shilingi bilioni tisa kwa mwezi tofauti na kipindi cha awali ambapo makusanyo  yalikuwa  yanafikia wastani wa  shilingi bilioni  nane kwa mwezi.
Meneja wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mkoa wa Arusha Mhandisi Gaspa Msigwa ( wa pili kutoka kulia) akielezea hali ya upatikanaji wa umeme mkoani Arusha kutokana na kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha KIA 132/33kV kilichopo mkoani Kilimanjaro.

Aliendelea kusema kuwa kukamilika kwa kituo hicho kumehamasisha kuongezeka kwa  ujenzi wa nyumba pamoja na  kuanzishwa kwa viwanda vidogo katika mkoa wa Arusha.

Wakati huo huo Julius Urassa ambaye ni msimamizi wa kampuni inayojihusisha na uzalishaji wa kokoto ya Ravji Aggregate Limited iliyopo wilayani Arumeru mkoani  Arusha alisema kuwa  kabla ya kukamilika kwa kituo hicho  hali ya umeme  katika mkoa wa Arusha haikuwa nzuri.

“ Kabla ya kuwepo kwa kituo cha KIA, umeme ulikuwa unakatika mara kwa mara na kuathiri  uzalishaji  katika kiwanda chetu; lakini sasa tunapata umeme wa uhakika,” alisema.

Aliogeza kuwa kutokana na upatikanaji wa umeme wa uhakika, kampuni yake ina uwezo wa kuzalisha  tani 100 za kokoto kwa siku tofauti na zamani ambapo walikuwa na uwezo wa kuzalisha kati ya  tani  40 hadi  60 za kokoto kwa siku.
Msimamizi wa kituo cha KIA 132/33kV, Isaack Sarakikya (katikati) akionesha jinsi vifaa vya kuongozea mitambo vinavyofanya kazi.

Naye  Meneja wa Kampuni inayojihusisha na utengenezaji wa matofali kwa njia ya umeme  ya Melck Hardware iliyopo  Maji ya  Chai nje kidogo ya  jiji la Arusha, Hansi Said alisema kuwa  hali ya umeme katika mkoa wa Arusha imetengemaa hali iliyopelekea uzalishaji  kuongezeka katika kampuni yake.

Alisema kutokana na upatikanaji wa umeme  wa uhakika, kampuni yake ambayo hutengeneza matofali kulingana na oda kutoka kwa wateja, imeongeza uzalishaji kutoka  wastani wa  tofali 700 hadi 2,000 kwa siku.

Naye  John Augustino mkazi wa Arumeru mkoani Arusha aliongeza kuwa  tangu kuanza kupatikana kwa umeme wa uhakika, hali ya maisha katika  familia yake imeboreka kutokana na kuuza bidhaa zaidi ya maziwa tofauti na mwanzo katika duka lake.

“Bidhaa za vinywaji  hususan maziwa  yalikuwa yanaharibika kutokana na  kukatika kwa umeme, lakini  kwa sasa tunapata umeme wa uhakika, hali inayochangia kuuza bidhaa bora zaidi,”alisisitiza.
Meneja Miradi ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme kutoka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mhandisi Emmanuel Manirabona akielezea jinsi kifaa cha kuongozea mitambo ya umeme kinavyofanya kazi mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani).
Meneja Miradi ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme kutoka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mhandisi Emmanuel Manirabona ( katikati) akielezea namna ya uwekaji wa nyaya za umeme chini ya sakafu kwa lengo la kuimarisha usalama katika kituo cha KIA 132/33kV kilichopo mkoani Kilimanjaro.
Sehemu ya mitambo ya kampuni inayojishughulisha na uzalishaji wa kokoto ya Ravji Aggregate Limited iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha ambayo ni moja ya wanufaika wa umeme kutoka katika kituo cha KIA 132/33kV.
John Augustino mkazi wa wilaya ya Arumeru mkoani Arusha akielezea mchango wa kituo cha KIA 132/33kV katika ukuaji wa uchumi wa wakazi wa mkoa huo.

No comments: