Umoja wa Mataifa na Shirika la Afya Duniani ( WHO), ni baadhi ya Taasisi za Kimataifa ambazo zimeanza kutekeleza kwa vitendo sehemu ya mapendekezo na ushauri uliotolewa na Jopo la Ngazi ya Juu kuhusu Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya.
“ Tumeanza kutekeleza baadhi ya mapendekezo ya Jopo lililokuwa chini ya Uenyekiti wa Rais Mstaafu wa Tanzania, Mhe, Jakaya Mrisho Kikwete. Mhe. Rais nakushukuru sana kwa uongozi wako, ushiriki wako na mchango wako. Nimefarijika kwamba umeweza kuungana nasi katika mkutano huu kutokea Senegal, kuzungumzia mapendeko ya Jopo lako”. Akasema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Ban Ki Moon, ameyasema hayo, jana ( jumatatu) wakati wa mkutano usio rasmi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ulioandaliwa na Rais wa Baraza hilo, Bw Mogens Lykketoft kwa lengo la kupokea Ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu uimarishaji na usanifu wa huduma za Afya Kimataifa: utekelezaji wa mapendekezo ya Jopo la Ngazi ya juu kuhusu Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya.
Baadi ya mambo ambayo yameanzwa kutekelezwa kwa mujibu wa Katibu Mkuu yanahusu Shirika la Afya Duniani ambapo katika mapendekezo yake, Jopo limeainisha kutambua kuwa WHO inabaki kuwa taasisi kiongozi linapokuja suala la afya wakati wote na hususani wakati wa majanga ya dharura ya milipuko ya magonjwa.
“ Jopo limependekeza kuwa uwezo wa WHO katika kuitika yanapotokea majanga ya dharura ya kiafya unatakiwa kuimarishwa wakati wote na kutokana na mapendekezo ya Jopo WHO imeanzisha mpango wa dharura, unaokipa chombo hicho uwezo wa kuwajibika kwa haraka na kwa wakati pale unapotokea mlipuko wa ugonjwa”. Amebainisha Ban Ki Moon.
Pendekezo la pili mbalo limeanza kufanyiwa kazi na Umoja wa Mataifa ni lile la kuimarisha mifumo ya Umoja wa Mataifa hususani wakati wa matukio ya dharura yanayohusu milipuko ya magonjwa hivyo kuwa na uwajibikaji wa pamoja kupita Taasisi zake.
“ Tatu nimeridhishwa na hatua ya Banki ya Dunia ya kuzindua mpango wa dharura wa uwezeshaji wa kifedha pale yanapotokea majanga ya dharura ya kiafya, ni mpango ambao utatoa uhakika fedha dhidi ya majanga na utafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na WHO”. Ameeleza Ban Ki Moon.
Akielezea zaidi kuhusu mapendekezo yaliyopendekezwa na Jopo lililoongozwa na Rais mstaafu Kikwete. Ban Ki Moon amesema.
“ Mwezi April mwaka jana, niliunda Jopo la Ngazi ya Juu kuhusu ya Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya ili litoe mapendekezo ya namna ya kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa katika kuzuia na kudhibiti changamoto za majanga ya kiafya katika siku za baadaye.Mwezi februari mwaka huu, Jopo liliwasilisha Ripoti yake ikianisha mapendekezo 27 yanayotakiwa kufanyiwa kazi kuanzia ngazi ya taifa, kanda na kimataifa”.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, ameyataja baadhi ya maeneo ambayo yamesisitizwa na Jopo kuwa ni pamoja na, kuifanya mifumo na miundo mbinu ya utoaji wa huduma za afya kuwa imara na katika hali ya utayari wakati wote kukabiliana na majanga ya dharura, umuhimu wa tafiti za kisayasi, uhakika wa raslimali fedha ya kutosha na uwezeshaji kupitia miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Ban Ki Moon, mapendekezo ya Jopo hilo yamepitiwa kwa uangalifu mkubwa kupitia majadiliano miongoni mwa, na baina ya Taasisi za Umoja wa Mataifa.
Na baada ya majadiliano hayo, Mkuu huyo wa UM ameandaa taarifa yake ambayo imepewa kichwa cha : Uimarishaji wa Mifumo ya Afya ya Kidunia: Utekelezaji wa Mapendekezoya Jopo la Ngazi ya Juu kuhusu Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya.
“ Jopo lililongozwa na Mhe Kikwete limetupatia mapendekezo ya msingi na yenye tija ambayo kwayo ni kwa namna gani mifumo ya kijamii, kitaifa na kimataifa itakavyoweza kwa njia sahihi kujiandaa kukabiliana na majanga ya dharura ya kiafya katika siku za usoni. Mimi binafsi ninataka kujihusisha kikamilifu katika utekelezaji wa mapendekezo ya Jopo hili” akasisitiza Katibu Mkuu.
Na katika kuhakikisha kwamba utekelezaji wa mapendekezo ya Jopo yanasimamiwa na kufuatiliwa kwa ukaribu, Ban Ki Moon ameunda Kikundi kazi kitakachojulikana kama Global Health Crises Task Force ambacho moja ya majukumu yake makuu yatakuwa ni pamoja na kufuatilia, ku- ratibu na kuunga mkono utekelezaji wa mapendekezo ya Jopo.
Kikundi kazi hicho kitaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw, Jan Eliasson, Mkurugenzi Mkuu wa WHO. Dr. Margareth Chan, Dr. Jim Yong Kim Rais wa Banki ya Dunia, na Dr. David Nabarro, ambaye ni Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030) na Makubalino kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi ( Paris Agreement ).
Kwa upande wake, akiongea kwa njia ya mtandao video ( Video Conference) kutoka nchini Senegal,Mwenyekiti wa Jopo, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na kumshukuru, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kwa kumkabidhi jukumu hilo pia alianisha baadhi ya mambo kadhaa ambayo Jopo lake liligundua wakati wa utekelezaji wa hadidu za rejea.
Baadhi ya mambo ni pamoja na, WHO kuchelewa kutamka haraka na kwa wakati kwamba kuibuka kwa ugonjwa wa Ebola kulikuwa ni janga la kimataifa na lilotakiwa kuchukuliwa hatua za haraka kuzuia maafa yaliyojitokeza.
Kwamba, WHO haina raslimali fedha jambo ambalo inabidi itegemee zaidi michango na hisani za mataifa makubwa.
Kwamba, nchi nyingi hususani zile zinazoendelea mifumo na miundo mbinu ya utoaji wa huduma za afya zikiwamo za afya ya msingi bado ni dhaifu mno kiasi kwamba kwa vyovyote vile ilishindwa , inashindwa na itashindwa kukabiliana na changamoto za majanga ya dharura ya milipuko ya magonjwa kama vile ilivyokuwa kwa Ebola na sasa Zika na tishio la Homa ya ugonjwa wa manjano.
Rais Mstaafu Kikwete katika maelezo yake, amesititiza kwamba, udhaifu huo hauishi katika nchi moja moja bali pia unakwenda hadi ngazi ya Kikanda na Kimataifa.
“ Jopo letu limegundua kwamba, maisha ya mamilioni ya watu yatakuwa katika hatari kubwa sana na dunia itakuwa katika mashaka makubwa pale ambapo janga kubwa la magonjwa ya dharura yatakapoibuka na kukuta mifumo na miundo mbinu ya utoaji wa huduma za afya haijaimarishwa vya kutosha kukabili changamoto hiyo”. Amesisitiza Rais Mstaafu
Akaongeza Kikwete kwa kusema “ Ni matumaini yangu kuwa mapendekezo 27 yaliyotolewa na Jopo nililoliongoza yatatusaidia kufika huko tunakotaka kufika. Uungaji mkono wako binafsi Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ukichagizwa na utashi wa kisiasa wa viongozi mbalimbali katika ngazi ya juu kadri itakavyowezekana utasaidia sana katika ufanya mambo yaende”.
Ni katika kutambua uzito wa dharura itokanayo na magonjwa ya milipuko, MwenyeKiti wa Jopo Kikwete amesema Jopo limependekeza pia kwamba kwanza, kuanzishwe Baraza la Ngazi ya Juu Kuhusu Majanga ya Dharura ya Afya ya Jamii, na pili, kuitishwa kwa Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu Majanga ya Kiafya mwaka 2018.
No comments:
Post a Comment