Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika hafla ya kukabidhiana magari tisa yenye thamani ya Shillingi Millioni mia nane na kumi kutoka Shirika la ICAP Tanzania kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika nchi nzima kuanzia mwezi Septemba, 2016. Kushoto kwake ni Claud Kumalija mwakilishi wa katibu Mkuu wa Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Dkt. Fatuma Mrisho akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika hafla ya kukabidhiana magari tisa yenye thamani ya Shillingi Millioni mia nane na kumi kati ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Shirika la ICAP Tanzania kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika nchi nzima kuanzia mwezi Septemba, 2016. Kushoto kwake ni Claud Kumalija mwakilishi wa katibu Mkuu wa Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kulia kwake ni Dkt. Michelle Roland Mkurugenzi Mkaazi wa Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Magonjwa – (Centre for Disease Control and Prevention - CDC).
Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika wa Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Magonjwa – (Centre for Disease Control and Prevention - CDC) Dkt. Michelle Roland akikata utepe kuashiria kukabidhi rasmi magari tisa yenye thamani ya Shillingi Millioni mia nane na kumi kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika nchi nzima kuanzia mwezi Septemba, 2016.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa pamoja na mwakilishi wa katibu Mkuu wa Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Claud Kumalija wakionyesha ufunguo wa gari mbele ya waandishi wa habari na wageni waalikwa kuashiria kupokea magari tisa yaliyotolewa na Shirika la ICAP Tanzania kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika nchi nzima kuanzia mwezi Septemba, 2016.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akiwasha gari kama ishara ya kupokea magari tisa yenye thamani ya Shillingi Millioni mia nane na kumi kutoka Shirika la ICAP Tanzania kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika nchi nzima kuanzia mwezi Septemba, 2016. Hafla ya makabidhiano ya magari hayo imefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa (wa kwanza kulia) pamoja na wageni waliohudhuria katika hafla ya kukabidhiana magari wakiangalia baadhi ya magari yaliyotolewa na Shirika la ICAP Tanzania kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika nchi nzima kuanzia mwezi Septemba, 2016. Hafla ya makabidhiano ya magari hayo imefanyika leo jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL GHULA)
Na: Veronica Kazimoto.
OFISI ya Taifa ya Takwimu imekabidhiwa magari tisa aina ya Land cruiser yenye thamani ya Dola za kimarekani laki nne na elfu tano ($ 405,000) sawa na Shillingi za kitanzania Milioni mia nane na kumi (810,000,000/=) kutoka Shirika lisilo la kiserikali la ICAP linaloendeshwa na Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani kwa ajili ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utakaofanyika mwezi Septemba, 2016.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhiana magari hayo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amelishukuru Shirika la ICAP kwa msaada huo ambao utasaidia kupunguza gharama za kukodi magari kwa ajili ya kufanyia utafiti.
“Napenda kuchukua fursa hii kulishukuru Shirika la ICAP kwa kutupatia msaada huu wa magari tisa yenye thamani ya Shillingi milioni mia nane na kumi. Huu sio msaada mdogo kwani fedha ambazo zingetumika kukodisha magari ya utafiti, sasa zitatumika katika shughuli nyingine za kimaendeleo,” amesema Dkt. Chuwa.
Amesema katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), takwimu rasmi zinahitajika ili kupima utekelezaji wake na hivyo utafiti huu utakapokamilika utasaidia kutoa takwimu zitakazotumika kupima utekelezaji wa malengo hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la ICAP Tanzania, Dkt. Fernando Morales amesema utafiti huu unalenga kupima Viashiria na Matokeo ya UKIMWI nchini ili kujua ni kwa kiwango gani Tanzania imepiga hatua katika kupambana na ugonjwa huo.
Dkt. Morales amesema msaada huu wa magari utasaidia kurahisisha usafiri wa kutoka eneo moja la utafiti hadi lingine na kuweza kusaidia katika upatikanaji wa taarifa muhimu za utafiti huu.
Nae Mkurugenzi Mkaazi wa Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Magonjwa – (Centre for Disease Control and Prevention - CDC) Dkt. Michelle Roland amesema kutokana na utafiti huu kufanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya ukusanyaji wa takwimu, kutasaidia kupunguza gharama ambazo zingetumika kama utafiti huu ungefanyika kwa njia ya kutumia madodoso ya karatasi.
Ameongeza kuwa utafiti huu utafanyika kwa kutumia sampuli wakilishi ya kaya zipatazo 15,800 Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, na kuwafikia walengwa wapatao elfu arobaini (40,000) wakiwemo watoto wasiopungua elfu nane (8,000).
Matokeo yanayotarajiwa kupatikana katika utafiti huo ni pamoja na taarifa sahihi kuhusu hali ya maambukizi mapya ya VVU, upatikanaji wa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU hapa nchini na kutambua ni kwa kiwango gani huduma hizi zimesaidia katika kuudhibiti ugonjwa wa UKIMWI.
Utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utafanywa kwa pamoja na Shirika la ICAP Tanzania, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa Tanzania Zanzibar, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS), Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC).
No comments:
Post a Comment