Thursday, May 26, 2016

Wataalam wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) Watambulika SADC

Na Samwe Mtuwa – GST

Watalaam watatu wa Taaluma ya Sayansi ya Miamba na Madini kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ambao ni Alphonce Michael Bush, Masota Matthew Magigita na Zortosy Mpangile Maganga, wametambuliwa rasmi na Taasisi ya Japan, Oil, Gas, and Metal Cooperation (JOGMEC) ambapo sasa wanaweza kutoa mafunzo ya Utalaam wa Utafiti wa Rasilimali Madini kwa kutumia   Visawe vya Mbali (Remote Sensing) katika nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC).

Mmoja wa Wataalam hao ambaye ni Meneja wa kitengo cha Maktaba ya Kumbukumbu ya GST, Masota Magigita, alisema kuwa utambuzi huo umekuja baada ya Taasisi hiyo ya JOGMEC kutoa Mafunzo ya muda mfupi na mrefu, Semina na Warsha mbalimbali  kwa watalaam wa  GST, juu ya kufanya tathmini ya maeneo yenye uwezekano wa kuwepo kwa madini.

“Tathmini hii hufanyika kwa kutumia uchambuzi wa picha zilizopigwa kwa satelite pamoja  na ukusanyaji wa takwimu za Jiosayansi baada ya kufanya kazi za ugani (field work) ili kuboresha kanzidata ya Taasisi,” alisema Magigita.

Magigita aliongeza kuwa kupatikana  kwa ujuzi huo wa kusoma na kutafsiri picha na takwimu za visawe mbali zilizopigwa kwa mfumo wa satelaiti (satelite) kutasaidia kuongeza ufanyaji wa kazi za utafiti wa madini nchini na ufanyaji tathmini kwa kina.

Alisema kuwa ujuzi huo pia utasaidia katika Sekta ya utafiti na uchunguzi wa kujua chanzo au vyanzo vya uharibifu wa mazingira mfano ongezeko la Makazi ya watu pamoja kupungua kwa misitu  hasa katika mabadiliko ya uso wa dunia.
Aidha alisema ujuzi huo utatolewa kwa Watalaam wengine wa GST ili waweze kupata uelewa zaidi katika uchambuzi wa taarifa na picha zilizopigwa kwa kutumia satelaiti.

Magigita aliongeza kuwa ushirikiano wa GST na Taasisi hiyo ya JOGMEC umekuwepo   kwa zaidi ya miaka Sita ambapo JOGMEC hutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi kwa watalaam mbalimbali wa GST.

“Ushirikiano wetu ulianza  mwaka 2009 ambapo tumekuwa tukipewa  mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi juu ya utoaji mafunzo kuhusu  utafutaji wa madini kwa kutumia visawe mbali (remote sensing),” alisema Magigita
Akielezea kuhusu faida za ushirikiano huo,  Magigita alisema kuwa kuna faida mbalimbali ikiwemo kubadilishana ujuzi, maarifa na uwezo wa kufanya tafiti za Jiosayansi ili  kuboresha kanzidata ya GST kwa kuongeza ujuzi, ukusanyaji na  utunzaji  wa takwimu za  upatikanaji wa madini mbalimbali yanayopatikana nchini.

Alisema kuwa Sambamba na mafunzo hayo taasisi ya  JOGMEC  pia ina mpango wa kushirikiana na GST katika  kazi za ugani na ukusanyaji wa taarifa  za Jiolojia  utakaofanyika Tanzania  na uchakataji taarifa hizo za jiolojia utafanyika nchini Botswana.

Vilevile alisema kuwa  JOGMEC ina mpango wa kushirikiana na  GST kuendesha Semina za Kimataifa  juu ya Maendeleo Endelevu katika  Sekta ya Madini nchini Tanzania. 

Mafanikio ya Wataalam wa Wakala huo ambao upo chini ya Wizara ya Nishati na Madini,  yamemfurahisha Waziri wa Nishati na  Madini, Profesa Muhongo ambaye alituma Ujumbe Mfupi wa Simu na kueleza kuwa Tanzania inasonga mbele kwa kasi kubwa.

No comments: