Monday, May 9, 2016

WANANCHI WA KITONGOJI CHA PERA CHALINZE WAANZA KAMPENI YA KUPAMBANA NA MLIPUKO WA KIPINDUPINDU

Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Chalinze Hussein Mramba akizungumza na wafanyabiashara mbali mbali wa kitongoji cha Pera Chalinze katika mkutano ulioandaliwa kwa ajili ya kujadili namna ya kupambana na mlipuko wa ugonjwa kipindu pindu.
 Baadhi ya wafanyabishara katika kitongoji cha pera Chalinze wakiwa katika Mkutano huo wa kujadili masuala ya usafi pamoja na kupambana na kipindupindu. 

KATIKA kuunga  mkono juhudi za serikali katika kupambana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu  wafanyabiashara  mbali mbali katika kitongoji cha Pera halmashauri ya Chalinze  Mkoa wa Pwani  wameungana na kuanzisha kampeni maalumu kwa ajili ya kutokomeza  taka zote  zinakuwa zikitupwa ovyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti  katika kikao  kilichoandaliwa kwa ajili ya kuweza kujadili  mambo mbali mbali  kuhusiana na suala la usafi pamoja na kupanga mikakati ya kuweza kuhakikisha wanapambana  vilivyo na mlipuko wa ugonjwa wa kipindu pindu.

Wafanyabishara hao akiwemo Rashid Kirumbi,William Mshauri  Pamoja na Mwanaidi Tambiligogo walisema kwamba kwa sasa wanafanya kazi zao katika wakati mgumu sana kutokana na  kitongoji  hicho cha pera hakina eneo la kutupia taka hivyo kusababisha kuzagaa kwa uchafu mwingi ambao  unaweza kuleta madhara makubwa kwa  wananchi wa eneo hilo.

Aidha walisema kwamba kwa sasa katika eneo hilo la pera hakuna eneo maalumu  kwa ajili ya kutupia taka ukizingatia na wafanyabiashara hao wanazalisha taka nyingi kwa siku hivyo hivyo kuwapa wakati mgumu pindi wanapotaka kutupa taka.

“Hapa kitu kikubwa kikao hiki kimeandaliwa kwa lengo a kuweka mikakati ya kupambana na mlipuko wa magonjwa hususan ugonjwa wa kipindupindu ambao kwa sasa umeongia katika eneo hili kwa  hiyo sisis kama wafanyabiashara inatubidi tuhakikishe kwamba tunafanya usafi katika maeneo yetu ambayo tunafanyia biashara na hili suala inabidi wote kwa pamoja tushirikiane na  serikai yetu,”walisema wafanyabiashara hao.

Pia walibainisha kuwa kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanatafuta eneo maalumu la kutupia taka hizo, pamoja na kuwa na gari ambalo litakuwa likipita katika maeneo mabali mbali kwa ajili ya kuweza kuzikusanya taka hizo la kwenda kuzipeleka dampo.

Nao wajumbe wa serikali ya  kitongoji hicho cha pera akiwemo Simon Mbena pamoja na Nadhil Abdallah walisema  kwamba kwa sasa hali ya ugonjwa wa kipindu pindu katika eneo hilo ni mbaya hivyo kunahitajika juhudi za makusudi katika kufanya usafi katika sehemu za biashara na majumbani ikiwemo sambamba na kutenga eneo kwa ajili ya  dampo maalumu la kutupitia  taka hizo.

Awali akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Chalinze Hussein Mramba amekiri kutokuwepo kwa  eneo la serikali lililotengwa katika kitongoji hicho kwa ajili ya matumizi ya  kutupa taka,na kubainisha kwamba  tayari kuna wagonjwa watano wa kipindu pindu ambao tayari wamesharipotiwa hivi karibuni  katika eneo la Chalinze.

Mramba alisema kwamba nia ya serikali ni kuweza kuhakikisha kwamba wanapambana na ugonjwa huo wa kipindu pindu hivyo atashirikiana bega kwa began a wananchi wa kitongoji hicho cha pera ili kuweza kulitafutia ufumbuzi suala hilo na kuongeza kuwa kwa sasa wapo katika hatua za awali za kutafuta eneo maalumu  kwa ajili ya  kutupia taka.

KITONGOJI hicho cha Pera kilichopo katika mamlaka ya mji mdogo Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani hakina dampo la kutupia taka, na kupelekea wafanyabiashara na wananchi kuamua kuzitupa sehemu yoyote hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kuzagaa kwa uchafu huo ambao umedai unasababisha kutokea kwa magonjwa ya mlipuko hasa katika kipindi hiki cha masika.

No comments: